Kusinzia ni jambo la kawaida kwa mwanadamu aliyechoka. Lakini kusinzia wakati wa ibada, hasa wakati Neno la Mungu linafundishwa, sio jambo la kawaida kiroho. Ni dalili ya mashambulizi ya kipepo, yanayolenga kuzima roho yako usipokee Neno la uzima.
Ukweli huo unathibitiswa na Marko 1:23. Imeandikwa hivi:
“Na mara palikuwapo katika sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapiga kelele.”
Hiyo inaonyesha kuwa mapepo hayana aibu ya kuingia hata ndani ya nyumba ya Mungu. Kwahiyo mtu kama hayuko macho kiroho, anaweza kuvamiwa na mapepo hata akiwa kanisani.
Kusinzia Kanisani ni mapambano ya roho na mwili. Yesu aliwaambia wanafunzi wake:
“Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.” (Mathayo 26:41)
Wakati mwingine mwili huchoka, lakini mara nyingi, hali hiyo hutumiwa na adui kukukwamisha usisikie sauti ya Mungu. Pepo hutumia udhaifu wa mwili kufanya usinzie na kuziba masikio ya kiroho.
Kwanini pepo wanawafanya watu wasinzie Kanisani? Hiyo ni njama ya shetani. Katika Luka 8:12, Yesu alisema:
“...Ibilisi huja akaliondoa lile neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka.”
Kusinzia wakati wa mahubiri ni njia ya adui ya kuzuia mbegu ya Neno la Mungu kuingia moyoni. Kumbuka, imani huja kwa kusikia Neno la Kristo. Kwahiyo kama mtu anasinzia saa ya Neno ni wazi hawezi kuwa na imani. Na pasipo imani hatuwezi kumpendeza Mungu. Hiyo ndiyo furaha ya shetani na mapepo yake.
Pepo wanaoleta usingizi ni wa hila, sio wa kumfanya mtu apige makelele kama waliopagawa na mapepo ya magonjwa. Pepo anayeleta usingizi huja kwa utulivu. Anakuletea usingizi wa taratibu, unahisi ni usingizi wa kawaida, kumbe ni mtego wa kukufunga rohoni. Huo ni usingizi wa kiroho. Pepo watakuacha uendelee tu kuwa “mtu wa kwenda kanisani” lakini hutakuwa na nguvu wala tunda la Roho.
Mpaka hapo naamini umeona kuwa kusinzia kanisani siyo jambo la kupuuzia. Ni dalili ya mashambulizi ya kiroho, yanayolenga kukunyima nafasi ya kusikia sauti ya Mungu, kukufanya uwe baridi kiroho na hatimaye uanguke. Kwahiyo ukiona dalili za kusinzia, usikubali usingizi ukutawale: Kemea kwa Jina la Yesu. Dalili zikizidi, funga na kuomba kama tunavyoshauriwa katika Mathayo 17:21. "Pepo wa namna hii hawezi kuondolewa ila kwa maombi na kufunga."