HABARI za uhakika zinasema kuwa baadhi ya marais na mawaziri wakuu wastaafu wa Tanzania wamegoma kwenda Butiama kushiriki vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM. Siku chache zilizopita, baadhi yao, chini ya Mzee Ali Hassan Mwinyi, walikuwa na kikao cha dharura kujadili namna ya kuinusuru CCM kutoka kwa mafisadi. Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye hawakualikwa. Wajumbe wa kikao cha Mwinyi waliazimia kutumia kikao cha Butiama kumlazimisha Rais Jakaya Kikwete achukue hatua mbili muhimu.
Kwanza, atumie mamlaka aliyonayo kuhakikisha vikao hivyo vinawavua uanachama wale wote waliotuhumiwa katika kashfa za EPA na Richmond. Pili, walitaka atumie nguvu hiyo hiyo, kumuondolea kinga Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, ili afikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili, na aweze kutoa ushahidi katika kesi ya Balozi Costa Mahalu ambaye amemtaja kama shahidi mkuu.
Ushauri walioupata kwa Mzee Joseph Sinde Warioba ni kwamba ikibidi, Mkapa aondolewe kinga kwa muda tu kwa ajili ya kesi ya Mahalu, halafu arejeshewe.
Katika kikao hicho, Mzee Mwinyi aliwashauri wenzake kwamba iwapo Kikwete atakataa kuchukua hatua hizo, itokee vurumai kubwa, hata kama itawalazimu kuivunja CCM na kuwa CCM A na CCM B. Wazo la CCM kuvunjika halikumpendeza Rais Mstaafu wa Zanzibar, Salmin Amour; kwa maelezo kuwa CCM ikivunjika itakuwa faida ya wapinzani, hasa Zanzibar.
Kwa hiyo, walikubaliana kuwa badala ya kuvunja chama, kama Kikwete hakubali ushauri wao, wao watagoma kushiriki kikao hicho. Alipokataa, kama walivyotarajia, wakaamua kutokushiriki.
Hata baada ya kuamua kutokwenda Butiama, hawakumtaarifu mwenyekiti wao (Kikwete). Alitaarifiwa na watu wa protokol walipokuwa wanaandaa usafiri wa wastaafu hao, huku kila mmoja akitoa udhuru wake papo hapo.
Baadhi yao, wakiwamo Mwinyi, Salim Ahmed Salim, Mkapa na Sumaye, wanasemekana kwenda nje ya nchi katika kipindi walichohitajika kwenda Butiama.
Sababu mojawapo ya Kikwete kukataa kuwachukulia hatua mafisadi wa EPA na Rihmond inasemekana ni hatua yake ya kuwalinda (au kuwaogopa) rafiki zake Edward Lowassa na Rostam Azizi ambao ni watuhumiwa wakuu wa Richmond. Na inasemekana sasa Kikwete amelazimika kuanza mkakati mpya wa kumbeba Lowassa, jambo ambalo limezua 'uhasama' kati yake (JK) na Spika wa Bunge, Samuel Sitta.
Kumeguka kwa wastaafu, hasa Mzee Mwinyi, kutoka kambi ya Kikwete, si habari ndogo. Inafikirisha na kuzua maswali magumu juu ya hatima ya chama na uongozi mzima wa Kikwete. Hadi habari hii inaandikwa, wastaafu walioonekana Butiama wakati kikao cha Kamati Kuu kinaendelea ni Rashid Kawawa, John Malecela na Gharib Bilal. Walio Butiama tuletee habari kuhusu Joseph Sinde Warioba na Cleopa Msuya.
Kutoka:
http://www.ngurumo.blogspot.com/