Sehemu ya 3
Baada ya kufika Tarakea kwa shangazi aliniunganisha na mmeru mmoja baba wa makamu wa huko Kenya eneo moja linaitwa Oloitoktok kwa watu wa Rombo na maeneo ya jirani wanapafahamu hapo elimu ndio ilikuwa ishanipiga sandakalawe. Huyo mmeru alikuwa na mke na watoto wawili mke wake ni jamii ya Wakamba maeneo ya Taveta.
Nilianza kuuza duka la mahitaji ya nyumbani biashara kwa kweli ilikuwa nzuri ila kila huyo mwanamke wa Kikamba akija alikuwa na mtindo wa kuchukua pesa na kusema atarudisha ila harudishi, akija mumuwe anakana katakata hajachukua hivyo nakatwa mshahara wangu.
Sa nyingine ananipa nguo nivae yeye alikuwa anauza mitumba ikifika mwisho wa mwezi nakatwa kwenye mshahara wangu hata ukigoma kununua anasema nimekupa bure upendeze mwanangu ila tarehe ya salary ikifika nalimwa panga. Hicho kitu kilikuwa kinaniuma sana. Ikanibidi nimwambie mumewe ambaye ndio bosi wangu, kwa kweli maisha hapo Loitoktok niliyaona machungu sana maana nakumbuka msosi alikuwa hanipi mpaka mumewe arudi jioni ndio nakula, bado nilikuwa nasingiziwa kuwa nasumbua watoto wake nyakati za mchana, ile vita na mwanamke wa Kikamba ilinishinda ikabidi nikubali yaishe nikaomba kuondoka sikupewa hata mia kwani niliambiwa sidai kitu na bado nimesababisha hasara nyingi sana.
Ikanibidi niondoke hapo nakuelekea maeneo ya Taveta ambapo nilikutana na wafanyabiashara wengi sana watanzania ambao walikuwa wakileta maparachichi na ndizi kuja huu upande wa Kenya. Niliwaomba msaada maana hapo sasa nilikuwa nimeshaishiwa nikapandishwa kwenye Beckford ile kama kumbukumbu ziko sawa kwa nyuma kule, gari lilisafiri breki yake moshi mjini nikaambiwa tumefika.
Kwa hapo Moshi nilikuwa mgeni maana ni mjini hivo sio mzoefu. Nilizungaka huku na huku nikadakwa kwa kosa la uzururaji na kuambiwa mimi ni chokoraa, haswa kwa wakati huo machokoraa waliaminika kutenda uhalifu sana kwa Moshi.
Nilikaa ndani, na kila polisi wakinihoji ndugu wakwapi mimi nasema sina. Nilikaa kwa siku 3 nikaachiwa baada ya afande mmoja kusema angenichukua niende Mererani kwenye biashara yake kuuza maji maeneo ya Kazamoyo.
Niliuza maji kwa kutumia punda na hapo kwa kweli nilikuwa na hasira sana na maisha na niliona msaada sina tena maana ndugu wamenitenga na hata wadogo zangu sikuwajulia hali zao. Ile biashara kwa pale Mererani ilikuwa na hela maana nilikuwa nakaa kwa huyo afande na mke wake pia alikuwa askari ila wa magereza.
Nikaja kupata dili la kupeleka maji migodini huko, ila shida ikawa kwenye malipo ya hela mpaka shimo liteme ndio ulipwe na sa nyingine urushwe na bosi haelewi ni mtata sana, kuna muda anakushushia kipigo kizito sana ukichelewesha hela na huna pakwenda kushtaki anakuambia wazi wazi.
Nikaachana na hiyo kazi nikaingia kwenye uana polo na kwa nyakati hizo migodi ya Tanzanite ilikuwa inatema sana madini haswa mgodi wa Ray** na Lemak**. Ila kiujumla nilishindwa na haswa kutokana na kula msoto sana na magonjwa ya tumbo haswa typhoid ni kitu cha kawaida.
Na kwa nyakati hizo tofauti na sasa ilikuwa hulipwi hela ila mawe yakipatikana tajiri anachukua chake ndio na nyie mpate mgao ila inategemea na makubaliano.
Wengi sana tulienda na tulishindwa na wapo waliofanikiwa tukiwaona. Hivo nilipata kampani ya watu wa Ngarenaro nikaungana nao kwenda Arusha kujaribu bahati tena huko!
Je? Nini kitaendelea usikose kufuatana nami hadi mwisho.