Kuna mshkaji wangu tunafanya naye kazi jana amekuja analalamika kuwa wakati akijisaidia haja kubwa anatokwa na damu. Sasa ameanza kupata wasiwasi kuwa anaweza kuwa na kansa ya njia ya haja kubwa.
Mimi kama mdau wa hapa ninapopaaminia naomba tumshauri huyu mshkaji wangu ili aepukane na janga hili. Yuko kwenye tension kwa kweli
Big Up Jf members kwa ushirikiano wenu
Kuwa makini na kutokwa damu njia ya haja kubwa
By Dk Christopher Peterson
Unaweza kuhisi una uvimbe umejitokeza nje ya njia ya haja kubwa wenye muwasho, maumivu na wakati mwingine ukiwa unajisaidia haja inatoka kwa tabu na kadri unavyotumia nguvu kuisukuma unahisi maumivu, ikitoka inakuwa na damu. Hili ni tatizo la afya ambalo kitabibu linaitwa Hemorrhoids.
Cha kusikitisha, wagonjwa wengi hawapati tiba sahihi kwa ama kuogopa, au kuona aibu kupata ushauri wa daktari kutokana na namna tatizo lenyewe lilivyo. Wachache huishia kununua dawa kutoka kwenye maduka yaliyopo mtaani bila ushauri wowote wa mtaalamu.
Jambo muhimu la kufahamu kwa kila mmoja ni kwamba, kutokwa damu sehemu za siri kunahitaji msaada wa daktari kuliko kutumia dawa bila kujua chanzo cha tatizo. Wanawake wanakuwa hatarini zaidi kupata ugonjwa huu hasa wanapokuwa wajawazito.
Inaelezwa, kadri mimba inavyokua, mfuko wa uzazi hupanuka na kuongezeka ukubwa hivyo kusababisha mkandamizo kwenye utumbo mpana.
Pia, wazee wapo kwenye kundi la hatari kwa sababu mfumo wao wa kinga mwilini dhidi ya magonjwa unapungua.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kuwa idadi ya wazee wanaopata tatizo hili duniani ni kubwa kuliko vijana na watoto, ingawa bado ni muhimu kuchukua taadhari
Wanaonyanyua vitu vizito ni waathirika pia, kwani kwa kufanya hivyo nguvu nyingi hutumika na kusababisha misuli kukaza hasa ya njia ya haja kubwa hivyo kuidhoofisha na kuvimba.
Wanaofanya zinaa kinyume na maumbile ni kundi jingine.
Mtu anapopatwa na tatizo hili, mara nyingi sehemu ya ndani ya ngozi kwenye njia ya haja kubwa inavimba na kutokeza nje. Huwa linatibika na kuzuilika kirahisi mgonjwa akimuona daktari mapema.
Tatizo hili linatokea wakati mishipa midogomidogo kwenye njia ya haja kubwa inatanuka na kusababisha ngozi ya sehemu ya ndani ya haja kubwa kutokeza nje, kutokana na maambukizi mbalilmbali.
Zipo dalili ambazo kila mmoja anapaswa kuwa makini nazo kukabiliana na ugonjwa huu, ambazo ni kutokwa na damu kusikoambatana na maumivu au maumivu ya kawaida, muwasho au maumivu ndani au nje ya sehemu ya kutolea haja kubwa.
Dalili nyingine ni uvimbe kwenye njia ya haja kubwa na ngozi ya ndani ya sehemu hiyo kutokeza nje. Yeyote mwenye moja ya dalili hizi anapaswa kumuona daktari haraka.
Baadhi ya maradhi kama vile saratani ya utumbo au ya njia ya haja kubwa, zinasababisha kutoka damu sehemu ya haja kubwa hivyo ni kosa kudhani kuwa ni tatizo tu la kawaida na kupuuzia kumuona daktari kwa msaada.
Kuharisha na uzito uliopitiliza, kukohoa kupita kiasi na mwili kukosa maji ya kutosha pia husababisha tatizo hili. Mwili unahitaji maji ili chakula kumeng’enywe vizuri hivyo upungufu wake husababisha ukosefu wa haja kubwa na inapotokea huwa ngumu kiasi cha kuleta msuguano unaosababisha michubuko, ambayo hurahisisha maambukizi kwenye njia ya haja kubwa.
Mgonjwa anayechelewa kupata matibabu hulazimika kufanyiwa upasuaji mdogo kumaliza tatizo alilonalo.
Kunywa maji ya kutosha ni njia rahisi ya kusaidia kuzuia ugumu wa kinyesi utakaoathiri kuchubua njia ya haja kubwa wakati wa kujisaidia. Namna nyingine ya kujiweka salama dhidi ya ugonjwa huu, ni kuhakikisha unapata mlo kamili utakaosaidia kujikinga au kuliondoa kama unalo.
Ulaji wa vyakula vyenye nyuzilishe kwa wingi; mboga za majani, matunda na vyakula visivyokobolewa mfano ugali wa dona kunarahisisha mmeng’enyo wa chakula na kuzuia utaoji wa kinyesi kigumu.