Aliwashitaki kwa kumzaa na kumleta duniani bila ridhaa yake, alikuwa hataki kuzaliwa.
Mshtaki kabla hajazaliwa hakuwaambia wazazi iwapo anataka kuzaliwa au hataki; moja kwa moja wazazi wakachukulia kwamba ni hatua ambayo bila shaka ingempendeza mtoto wao.
Wazazi walihofu kwamba endapo mtoto wao asingezaliwa, basi angeweza kuchukia na kuwashtaki wazazi wake kwa kutompa haki ya kuzaliwa na kuishi.
Hii ndiyo kusema kwamba mwanadamu hana haki yoyote ya kulaumu kuzaliwa au kuwepo duniani kwa vile hata kutokuwepo kwake hakutokani na uamuzi wake wowote.
Kwanza huyo mwanadamu apingaye ni nani?
Je, ni viasili mojamoja vya atomu ambavyo huunda kila kiungo cha wajihi wake?
Je, ni pumzi aliyonayo, ambayo Ukatoliki unapotosha kwamba ni roho inayojitambua na yenye uwezo wa kuishi na kujitegemea yenyewe nje ya mwili?
Au ni hivyo vyote viwili?
Kama ni hivyo vyote viwili, inawezekana huyo mwanadamu akawanavyo kwa pamoja pasi kuwa hai?
Kwamba kama hivyo viasili vya mwili na roho ni vyake, maana yake ni kwamba alikuwa hai kabla ya kuwa hai, sivyo?
Na kama siyo vyake, kwa nini alalamike pale ambapo viasili hivyo vimefinyangwa pamoja na kumhuluku kiumbe mwanadamu?
Mwanadamu! Mwanadamu! Kama aishivyo Mungu Mwenyezi, kaa utambue kwamba umeanzisha ligi iliyo nje ya mawanda na upeo wako!
Haki pekee aliyonayo mwanadamu ni kumshukuru Mungu kwa kupata fursa ya kuzaliwa, kuwepo na kuishi.