Rais Samia Suluhu Hassan anao upole wenye kuweza kumdanganya mtu akadhania kuwa hajui alitendalo. Ni haiba yake ya usikivu inayowadanganya wengi kiasi cha kuja na imani nyingi potofu juu ya kile anachokwenda kukiamua.
Ni sifa nzuri kwa Rais wa nchi kuwa nayo, kutoyumbishwa na mawazo pamoja na maoni mengi ambayo baadhi yake yanalengo au nia ovu zilizojificha. Kukaa kimya na kutafakari kinachoendelea ni jibu pia lenye busara nyingi kwa mtu mwenye nafasi ya juu kabisa ya maamuzi ya kitaifa.
Rais Samia ni mrithi wa JPM, kwani kisingetokea kifo cha JPM leo hii angeendelea kuwa makamu wa Rais. Hivyo hawa wanaokuja na mizigo ya lawama, kebehi na matusi wakumbuke kuwa Rais Samia na Hayati JPM ni kitu kile kile, wanashinda wakikariri namna mbalimbali za kutekeleza ilani ya CCM. Wanakabidhiwa na chama matarajio, maoni na malengo ya kutimiza katika kipindi fulani.
Ukimya wa Rais katika suala zima la uwekezaji wa DPW ni jibu tosha kabisa la kiongozi mkuu wa nchi. Kwani kipindi cha ukimya kinatumika katika kutafakari maamuzi atakayokuja kuyafanya siku za mbeleni na kutafakari faida na madhara yake kwa muda mrefu kwa Taifa letu.
Naamini ile kauli aliyoitoa siku anaongea na wafanyabiashara na ikapokelewa kwa makofi inakwenda kutekelezwa kwa vitendo. Kwamba ndani ya miezi sita atakuwa anasoma kile kinachofanyika bandarini, mifumo ya bandari na ile ya serikali ya mitandao itakuwa inasoma kitu kimoja.
Maana yake wale wote wanaofaidika kwa mgongo wa ufanisi mbovu pale TPA siku zao zinahesabika, watafute wataalam wa biashara ili waweze kupata ushauri juu ya mwenendo mzima wa biashara zao kuanzia kipindi cha baada ya miezi sita tangu kikao kile kifanyike.
Ile mirija ya wizi inakwenda kukatwa rasmi. Ile tabia ya maduka mengi ya mijini yanayouza bidhaa mbalimbali kuuza kitu kile kile kwa bei ndogo wakijivunia kutolipa kodi pale bandarini kwa kweli hali hiyo inakwenda kufikia ukomo.
Tabaka la wafanyabiashara linashindwa kuongezeka kwani wanashindwa kukuza mtaji wakiumizwa na kodi na wakati huo huo wachache kati yao wakifaidika na misamaha ya kodi pale TPA. Tabia hiyo ya uonevu kwa wafanya biashara inaleta ushindani usio wa haki katika soko la biashara.
Hao wachache wanaoneemeka kwa migongo ya wanasiasa wachache waliowahi kushika madaraka ya juu ya Taifa hili ni lazima wajipange upya na kuja na mikakati mipya wakati huu wa ufanyaji biashara tofauti kabisa na mazoea dhalimu yanayowabeba.
TPA inaingiza hazina trilioni 7 kwa mwaka, lakini kwa ufanisi wa mitambo mipya ya DPW inaweza kuja na ufanisi wa mpaka trilioni 26 hizo ni pesa nyingi zenye kuweza kuondoa shida nyingi za wakati huu. Hakuna sababu kwa mawaziri wetu kwenda Ulaya na kuanza kupigia magoti binadamu wenye vipaji kama sisi eti tunaomba misaada!.
Lazima nimpe maua yake hayati JPM aliyejenga SGR ili ije kuchukua mzigo mpana wa kutoka DRC na Rwanda ambao utaineemesha bandari yetu na kuongeza pato halisi la taifa. Aliona mbali licha ya kupigiwa makelele mengi ya matusi na dhihaka za kila aina, alikuwa ni kiongozi jasiri na mwenye akili pamoja na jeuri ya mwafrika halisi.
Hivyo Rais Samia aendelee tu na huu ukimya wake, hana haja ya kusikiliza sana kelele za madalali wa hawa matajiri wanaotajirikia bandari yetu kuwa kama ilivyo. Hana sababu ya kujiona anakwazwa kwa kuwa rais anayeletewa maneno mengi ya dharau na upuuzi wa ubaguzi kwamba yeye ni Mzanzibari pamoja na Waziri wake.
Tupo wengi wenye kuelewa tija yake haswa ni ipi na tupo wengi wenye kuridhishwa na maono anayoyasimamia ambayo ameyarithi kutoka kwa RIP JPM. Kebehi na shutuma nyingi za wanasheria na tabaka la wasomi ni sehemu tu ya uoga wa mabadiliko unaotusumbua watanzania, wengi wao wapo kwenye pay roll ya matajiri wakwepa kodi pale TPA.
Mheshimiwa Rais endelea na ukimya huo huo, unacho kishindo chenye neema nyingi kwa Tanzania ijayo.