Mathayo 6
31Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ Au ‘Tutakunywa nini?’ Au ‘Tutavaa nini?’ 32Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.
- Usitumainie vya udhalimu wala usijivune kwa vitu vya wizi; ingawa utajiri wako utaongezeka, usiviwekee moyo wako.
Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia
mali kwa hila; huuondoa uhai wa wale wenye
mali.
Zaburi 73
1 Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli,
kwa wale ambao mioyo yao ni safi.
2 Bali kwangu mimi, miguu yangu ilikuwa karibu kuteleza;
nilikuwa karibu mguu wangu kuachia uliposimama.
3 Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna
nilipoona kufanikiwa kwa waovu.
4Wao hawana taabu,
miili yao ina afya na nguvu.
5 Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine,
wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine.
6 Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao,
wamejivika jeuri.
7 Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi,
majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hauna kikomo.
8 Hudhihaki na kusema kwa ukorofi,
katika majivuno yao wanatishia kutesa.
9 Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu,
nazo ndimi zao humiliki duniani.
10Kwa hiyo watu wao huwageukia
na kunywa maji tele.
11 Wanasema, “Mungu awezaje kujua?
Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?”
12 Hivi ndivyo walivyo waovu:
siku zote hawajali,
wanaongezeka katika utajiri.
13 Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure,
ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia.
14 Mchana kutwa nimetaabika,
nimeadhibiwa kila asubuhi.
15Kama ningesema, “Nitasema hivi,”
ningelikuwa nimewasaliti watoto wako.
16 Nilipojaribu kuelewa haya yote,
yalikuwa magumu kwangu kuelewa.
17 Mpaka nilipoingia patakatifu pa Mungu,
ndipo nilipotambua mwisho wao.
18 Hakika unawaweka mahali pa utelezi,
unawaangusha chini kwa uharibifu.
19 Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula,
wanatoweshwa kabisa na vitisho!