JE, NINI HUKUMU KWA WANAWAKE KWENDA KUZIKA
Nimeulizwa kuhusu kujuzu au kutokujuzu kwa wanawake kusindikiza jeneza, NANUKUU:-
Alhabib naomba kuuliza. Nini hukumu ya wanawake kwenda kuzika? Asante!
JIBU
BISMILLAH
Wanawake, kimsingi, wanakatazwa kwenda kuzika, isipo kuwa ikitokea dharura, kwamba hakuna watu wa kumzika maiti isipo kuwa wanawake tu. Hapo hakuna junaha. Venginevyo inakatazwa.
Na makatazo haya ni makatazo ya Ukaraha mkubwa sana, si makatazo ya uharamu wa kupata dhambi, kama nitavyo fafanua baadae.
Msingi wa makatazo haya ni Hadithi Swahihi kutoka kwa Ummu 'Atwiyya رضي الله عنها isemayo:
((نُهِينَا عن اتِّباعِ الجنائِزِ، ولم يُعْزَمْ علينا)) متفق عليه
Imepokewa kutoka kwa Ummu 'Atwiyya رضي الله عنها akisema: "Tumekataza kusindikiza majeneza (kwenda kuzika), ila hakutusisitizwa (hatukutiliwa mkazo)." Muttafaq alayhi.
Wanazuoni wa Hadihi wamesema: Maneno ya Ummu 'Atwiyya :"Ila hatukusisitiziwa " maana yake tumekatazwa pasi na kusisitiziwa au kukaziwa na kuogogotozwa kwamba tukifanya hivyo tutapatilizwa kwa dhambi. Ndiyo maana wanazuoni, karibu wote, wamesema ni كراهة التنزيه Makatazo ya kujitakasa, au kujiepusha na uwezekano wa kutokea mambo ya haramu ndani yake. Imam An-Nawawy رحمه الله ameelezea vyema msimamo huo kama ifuiatavyo:
قال النووي رحمه الله في [شرحه على صحيح مسلم]: "معناه: نهانا رسول الله صلى الله عليه وسلم عن ذلك نهي كراهة تنزيه، لا نهي عزيمة تحريم، ومذهب أصحابنا أنه مكروه ليس بحرام لهذا الحديث".
"Maana yake: Tumekatazwa na Mtume ﷺ makatazo ya kujitakasa كراهة التنزيه na si makatazo ya kusisitiziwa uharamu wake. Na msimamo wetu sisi (Shafi'iyya) ni kuwa makuruhu kwa wanawake kwenda kuzika, na SI haramu kwa mujibu ya Hadihti hii." "Sharh Muslim."
Na amefafanua zaidi kwenye kitabu chake "Al-Majmu' kama ifuatavyo:
وقال في [المجموع]: "هذا الذي ذكرناه من كراهة اتباع النساء الجنازة هو مذهبنا، ومذهب جماهير العلماء، حكاه ابن المنذر عن ابن مسعود، وابن عمر، وأبي أمامة، وعائشة، ومسروق، والحسن، والنخعي، والأوزاعي، وأحمد، وإسحق، وبه قال الثوري".
"Msimaamo huu nilio utaja wa ukaraha wa wanawake kwenda kuzika ndio msimamo wa madhehebu yetu ya Shafii, na ndio msimamo wa wanazuoni wengi, kama alivyo simulia Ibn Al-Mundhir kutoka kwa (Maswahaba kama ) Ibn Mas'ud, Ibn 'Umar, Abu Umama na Aisha رضي الله عنهم , na vile vile ndio msimamo wa Masruq, Al-Hasan, An-Nakha'i, Al-Awza'i, Ahmad bin Hanbal, Ishaq bin Rahweha na Sufyan Ath-Thaywy." "Al-Majmu'" Kitab Al-Jana'iz.
Baadhi ya wafuasi wa Imam Abu Hanifa, hata hivyo, wanasema kuwa ni haramu kwa mwanamke kwenda kuzika. Dalili wanayo itumia ni Hadithi hiyo hiyo ya Ummu 'Atwiyya رضي الله عنها . Wao wanaona makatazo hayo ni makatazo ya uharamu. Ila hakuna dalili ya kuwepo adhabu kwa watakao fanya hivyo.
Kuna Hadithi mbili nyengine zenye kukataza wanawake kwenda kuzika, ila zote mbioli ni dhaifu kwa upande wa Isnadi zake. Imam An-Nawawy رحمه الله amezinukuu na kutoa ufafanuzi kuwa ni Hadithi dhaifu sana. Hadithi hizo ni hizi hapa.
1 - عن علي رضي الله عنه قال : خرج رسول الله صلي الله عليه وسلم فإذا نسوة جلوس قال : ما يُجلسكن ؟ قُلن : ننتظر الجنازة ، قال : هل تغسلن ؟ قُلن : لا ، قال : هل تَحْمِلن ؟ قُلن : لا ، قال : هل تُدلين فيمن يُدلي ؟ قلن : لا ، قال : فارجعن مأزورات غير مأجورات " ، رواه ابن ماجه بإسناد ضعيف من رواية إسماعيل بن سليمان الأزرق ، ونقل ابن أبي حاتم تضعيفه عن أعلام هذا الفن .
1- Imepokewa kutoka kwa Aliyy رضي الله عنه akisema: "Alitoka Mtume ﷺ akawakuta wanawake wamekaa kitako. Akawauliza: "Kilicho kukalisheni hapa ni nini?" Wakajibu: "Tunasubiri kuzika!" Alawauliza: "Je, nyinyi ndio waoshaji?" Wakajibu; "Hapana!" Alawauliza: "Je, nyinyi ndio mnao beba jeneza?" Wakajibu: "Hapana!" Akawauliza; "Je, nyinyi ndio mnao ingia kaburini kumlaza maiti?" Wakajibu: "Hapana!" Basi akawaambia: "Rudini makwenu mkiwa na dhambi, bila ya kupata thawabu!" Ameipokea Ibn Majah kwa Isnadi dhaifu, kupitia Isnad ya Ismail bin Sulayman Al-Azraq (hakubaliki). Na Ibn Abi Hatim amenukuu mabingwa wa fani hii ya Hadithi kuwa Ismail ni mtu dhaifu sana katika mapokezi ya Hadithi.
Hadihi ya pili inanasibishwa kutoka kwa Abdullah bin 'Amr bin Al-Aas رضي الله عنهما . Imam An-Nawawy ameinukuu kama ifuatavyo:
وأما حديث عبد الله بن عمرو بن العاص رضي الله عنهما أن النبي صلي الله عليه وسلم قال لفاطمة رضي الله عنها : ما أخرجك مِن بيتك ؟ قالت : أتيت أهل هذا البيت ، فرحمت إليهم مَيتهم قال : لعلك بلغت معهم الكُدَى قالت : معاذ الله أن أكون بلغتها ، وقد سمعتك تذكر في ذلك ما تذكر ، فقال : لو بلغتها معهم ما رأيت الجنة حتى يراها جدّ أبيك ، فرواه أحمد بن حنبل وأبو داود والنسائي بإسناد ضعيف .
Ama Hadithi ya Abdullah bin Amr bin Al-Aas رضي الله عنهما kwamba Mtume ﷺ alimwambia Fatma (bin Muhammad) رضي الله عنها : "Nini kilicho kutoa nyumbani kwako?" Akajibu: "Nilienda kuwazuri watu wa nyumba hii, kuwapa pole ya kufiwa na mtu wao!" Mtume ﷺ akamuuliza: "Usiniambie uliwafuata kusindikiza jeneza hadi eneo la Kuda!" Fatma akajibu: "Mwenyezi Mungu aniepushe kufanya hivyo. Nitawezaje kufanya hivyo baada ya kukusika kusema uliyo yasema!" Mtume ﷺ akamwambia: "Lau kama ungeli fuatana nao kusindikiza jeneza hadi huko, usingeliweza kuiona Pepo mpaka aweze kuiona Babu wa Baba yako!" Yaani lau kama ungeli fanya ivyo basi ingelikuwa muhali kwako kuiona Pepo. Ameipokea Ahmad bin Hanbal na Abu Daud na Nasai, wote kwa Isnad dhaifu.
وهذا الحديث ضعّفه النسائي وابن عبد الهادي .
Hadithi hii ameidhoofisha Nasai na Ibn Abdul Hadi. (Mwisho wa kumnumuu Imam An-Nawawy رحمه الله . "Al-Maju'"
Na kwa vile wanazuoni wote wanakubaliana kuwa Hadithi dhaifu haiwezi kuwa dalili ya kuharamisha kitu au kufaradhisha kitu, basi hadithi hizo mbili zilizo tajwa hapo juu, moja kunasibishwa kwa Aliy bin Abi Twalib na ya pili kunasibishwa kwa Abdullah bin 'Amr رضي الله عنهم na ambazo zote mbili ni dhaifu kwa upande wa Isnad, haziwezi kutumiwa kuwa ndio makatazo ya uharamu kwa wanawake kwenda kuzika makaburini.
Naam itakuwa haramu kwa wanawake kwenda kuzika iwapo kushiriki kwao huko kutapelekea kuchanganyika naa wanaume kwenda kuzika, au kutawapelekea wakalizana na kumuomboleza maiti. Hapo uharamu utakuwepo kwenye mambo hayo mawili, ambayo ni haramu. Si kwa sababu ya uharamu wa wao kwenda kuzika. Na hakutakuwepo hata ukaraha, iwapo hakutakuwepo wanaume wa kumzika maiti isipo kuwa wanawake tu. Hapo ni wajibu juu yao kwenda kumzika; wajibu wa kutoshelezana.
Ila kumswalia maaiti ni sunna kwa wanaume na wanawake; hakuhisiki na jinsia moja dhidi ya nyengine; ilimradi taratibu za kutochanganyika "chooko kwa mbaazi" unafuatwa. Yaani utaratibu ule ule wa kuswali msikitni swala za Jamaa, wanaume safu za mbele na wanawke safu za nyuma. Au kila wamoja kumswalia maiti peke yao. Hakuna junaha.
صلاة الجنازة فرض كفاية، وتشرع للرجال والنساء؛ لقول النبي صلى الله عليه وسلم: (مَنْ صَلَّى عَلَى جَنَازَةٍ فَلَهُ قِيرَاطٌ، فَإِنْ شَهِدَ دَفْنَهَا فَلَهُ قِيرَاطَانِ، الْقِيرَاطُ مِثْلُ أُحُدٍ) رواه البخاري ومسلم
Swala ya maiti ni faradhi ya kutoshelezana, na ni inajuziwa kwa wanaume na wanawake, kutokana na maneno ya Mtume ﷺ : "Atakayemswalia maiti atapata thawabu wingi wa Qirati moja, na atanye enda kumzika atapata thawabu za Qirati mbili, na Qirati moja ni sawa na ukubwa wa Jabal Uhud." "Muttafaq alayhi."
والله أعلم
وبالله التوفيق
السيد عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم
Imejibiwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
I RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chochote, bali kuiweka –kama ilivyo- kwenye FB yako au kwenye WhatsApp au kwenye Kumbi za Mitandao ya Jamii za Kiislamu, kwa lengo la kuelimisha na kusambaza Dini. Changia kusambaza Ilimu ya Dini, ili mchango wako uwe Sadaka yako Endelevu: صدقة جارية.
kcwajawema@gmail.com