Habari ya siku nyingi ndugu zangu, ngoja niende kwenye hoja moja kwa moja
Masuala ya ugomvi na migogoro ya ndoa kwa wazazi wetu ni mambo ambayo huwa tunakumbana nayo mara kwa mara na kwa asilimia kubwa sana japo sio kila familia au kila mtoto huweza kuyapitia haya mambo.
Ila niwape angalizo ndugu zangu katika masuala ya matatizo ya kifamilia ya wazazi usije hata siku moja ukaegemea upande wa mtu mmoja hata kidogo, kubwa unaloweza kulifanya ni kumfariji tu yule aliyeathirika zaidi kuwa na moyo mmoja wakusimama naye na kuhakikisha msongo na kukata tamaa isiwe sehemu yake.
Ukimchukia baba na akajua sababu ya mama au ukimchukia mama akajua sababu ya baba nakuhakikishia ndugu yangu nenda hata kwa mwamposa na shehe unayemjua wewe hii laana itakutafuna sana tena sana utakuwa ni mtu wa hatua mbili mbele tatu nyuma pasipo hata kuwa na suluhisho.
Narudia tena Mzazi awe na kosa au asiwe na kosa ila ukaingilia ugomvi wao ukamchukua mmoja wapo na akakufuta katika akili yake na moyo wake umekwisha kabisa.
HIli suala halina tiba yoyote zaidi ya kwenda kujiungamanisha na mzazi wako tena kabla hajaondoka hapa duniani na kama haujajifungamanisha naye akaondoka katika maisha haya hata ungekuwa mlokole wakuhamisha milima kwa maombi utahusika tu kwenda kutambika kumuomba msamaha mzazi wako.
Ndugu zangu hili suala limekaa kiroho sana namna ambayo huwezi tambua kiwepesi wepesi, laana ya kuingilia ugomvi wa wazazi na mzazi akaju umeegemea upande mmoja na akakukatia tamaa hii laana hakuna kiumbe wakuitoa chini ya jua na ulimwengu mzima zaidi ya mzazi wako,
Lasivyo itaendelea kuwasumbua hadi watoto wako pamoja na wajuu zako,
Na mara nyingi hizi laana zao zikisha kukalia wewe katika maisha hautaona la maana lolote wala hautakuwa na ahueni mahusiano yatakusumbua kama sio mahusiano basi maendeleo itakuwa shida kama sio maendeleo kipato kugumu kama sio kipato kigumu basi ipo sehemu ya muhimu kwako utakwama na hautaweza kujinasua hata kidogo,
Ukienda kuombewa na kuroga kwa waganga utapata ahueni ya mwezi mmoja tu na wala hautapata jibu la moja kwa moja hata siku moja.
Laana Hii ikikuvaa inatoka kwa njia moja tu wewe kwenda kwa mzazi wako ili arudishe moyo wako tena kwa ajili yako.
Sababu kubwa ya laana ya mzazi kuwa na nguvu nikwasababu kiroho kwa hapa duniani wazazi ndio miungu yako , wawe hai wasiwe hai wazazi wako ndio alfa na omega wako hapa duniani,
Siku nyingine nitakuja kueleza aina za laana ambazo wazazi wanaweza kukuachia,
Ukiwa na swali lolote unaweza ukauliza jisikie huru kabisa.
NASISITIZA HAKUNA MTUMISHI WALA SHEHE WALA MUNGU WALA SHETANI ANAYEWEZA KUITOA HII LAANA.
Muwe na jioni njema...!
Kama mbariki Laana ni Mwenyezi Mungu basi naamini hata ukimpigia Magoti Yeye ambaye pia ndiyo Kawaumba hao Wazazi atakusamehe tu kwakuwa Yeye ndiyo kila Kitu.
Hii Kasumba ya kuamini kuwa ukiona hufanikiwi duniani au Mambo yako hayaendi basi huenda kuna Mzazi wako Mmoja au Wote wawili umewakosea ni ya Kipumbavu kwani tukiiamini sana ndiyo inaenda kuharibu hadi Saikolojia zetu na kujikuta hatufanyi la maana.
Tupunguze huku Kutishana juu ya Wazazi Wetu na kuwaona kuwa Wao ni kila Kitu na kwamba hawakosei au hata Wao pia Wakitukosea hawapaswi Kujirudi Kwetu Watoto Kuomba Radhi hata kama siyo kwa Moja kwa Moja bali hata Kidiplomasia tu.
Migogoro mingi ya Wazazi na Watoto huwa inaibuliwa na Vyanzo vingi na kuna Watoto wengine Wanagombana na Wazazi wao kwa Kuchonganishwa na Ndugu, Jamaa na Marafiki au wemgine hata kwa Kurogwa au wengine hata Kufitinishwa na Ndugu zao wa Damu kabisa.
Sikatai kuwa kweli ukimkosea Mzazi wako huwezi pata Laana ila hata hiyo laana yenyewe huwa inaangaliwa na Mwenyezi Mungu kwa aina ya Kosa na tuache Kudanganyana hapa kuwa yaani Mzazi wako akiamua tu Kukulaani vile anavyojisikia basi hapo hapo inakupata.
Halafu nijuavyo Mzazi anayejitambua akiona yuko katika Mzozo au Mgogoro na Mwanae atafuta njia za Busara na Hekima hata kupitia kwa Ndugu au Marafiki zako ili mkae chini myamalize.
Kwa mfano unaweza kukuta labda Kibinadamu tu umemkosea Mzazi wako au hata hujamkosea popote ila kwa kuona kuwa Mzazi wako hana raha au futaha nawe ukataka kukaa nae chini myamalize lakini unakuta Mzazi huyo huyo hataki au anakukwepa huku akiendelea Kukuchukia. Je, hapa unadhani anayepata sasa Laana ya kweli ni Wewe Mtoto au Yeye Mzazi wako?
Na nijuavyo ni kwamba Laana mbaya duniani ni ya Mama Mzazi kwani Yeye ndiyo kwa 85% anakuhusu na pia Yeye ndiyo anajua Baba yako halisi ni nani. Laana za Baba huwa hazina Nguvu kwakuwa hata Kibaiolojia tu yeye ni mpandaji wa Mbegu kisha anasepa zake ila anayehangaika na hiyo Mbegu mpaka kuja duniani ni Mama na ndiyo maana unaambiwa ukimkosea tu Mama yako Mzazi wahi upesi mno ukampigie Magoti umuombe Radhi na mpeane Mikono na yataisha.
Mwanadamu kufanikiwa duniani Kimaisha hakutokani tu na Baraka za Wazazi wake bali pia ni Mipango yake, Malengo yake, Mikakati yake, Kujituma Kwake, Kujitambua Kwake na kubwa zaidi ni Kumuamini na Kumtumainia zaidi Mwenyezi Mungu kwani ana Falsafa yake Kuu ya kuwa huwa hawahi wala hachelewi katika Kumbariki Mtu au Mwanadamu.
Ni kweli tuwapende Wazazi wetu na hasa hasa tuwaombee sana kwa Mwenyezi Mungu na hata Wao pia wanatakiwa Kutupenda, Kutuombea na Kutusamehe Watoto wao pale ambapo kweli wanaona tumewakosea ila tuache Kutishana kuwa kama hufanikiwi Kimaisha hapa duniani basi huenda kuna mahala umemkosea Mzazi au Umewakosea Wazazi huu ni Uswahili na Upuuzi mkubwa mno.
Kwahiyo Watu wote duniani ambao wana Maisha magumu ni kutokana na Kukosana na Wazazi wao au Kuingilia Maugomvi yao? Je, hakuna Watoto ambao wana Mahusiano mazuri na Wazazi wao lakini bado tu Maisha yanawapiga? Je, hakuna Watoto ambao tunajua fika kuwa hawako vyema Kimahusiano na Wazazi wao lakini bado wana Maisha mazuri na tena Kutwa yanazidi tu kuwa mazuri?
Tunawashukuru Wazazi wetu kwa kutuleta hapa duniani, tunawapenda hata kama wapo wanaotuchukia na ndiyo maana wengine huwa kutwa tukiwa katika Dua au Sala zetu tunawaombea ila tusisahau kuwa mwenye Dhamana yako ya Kimaisha na ambaye akilipanga hata Watu wengine walipangue vipi, ipo Siku litaenda tu ni Mwenyezi Mungu ambaye ni Mungu wa Ibrahim, Isaka na Yakobo.