Mkuu ni kina Nani ambao hawataki kuwataja waislam kama walichangia kupatikana Kwa Uhuru mbona kina Bibi Titi wanajulikana vizuri Tu? Lakini pia je ni faida gani inapatikana kama wakitajwa na hasara ipi inapatikana wasipotajwa waislam?
Na mwisho kabisa je ulitegemea uone wakristo wengi kwenye huo mchakato kama ulikuwa unafanyika pwani ya Dar es salaam tena kariakoo? Wote tunajua pwani zote zina wingi wa waumini wa Imani ya kiislam hivo kama mchakato huo ungefanyika kaskazini ni wazi ingekuwa ngumu kuona Muslims
TATIZO KATIKA UTAFITI NA UANDISHI WA HISTORIA YA TANU1962
May 26
UTANGULIZI
Msomaji wangu jina lake Madagascar baada ya kusoma moja ya makala zangu niliyoeleza kuwa mradi wa kwanza wa kuandika historia ya TANU ulikuwa mwaka wa 1962 watafiti na waandishi wakiwa Abdul Sykes na Dr. Wilbert Klerruu, nilieleza kuwa Abdul Sykes alijitoa na Dr. Klerruu akabakia kukamilisha kazi, aliniandikia kutaka kujua sababu ya Abdul Sykes kujitoa.
Madagascar,
Kleruu alikuwa hana moja alijualo katika historia ya AA.
Abdul Sykes kwanza alikuwa na mswada wa kitabu alioandika baba yake.
Mswada huu ulikuwa kumbukumbu za baba yake akieleza historia ya vipi babu yake Sykes Mbuwane alikuja Germany Ostafrika kama askari mamluki chini ya Hermann Von Wissman.
Ndani ya mswada huu anaeleza maisha yake chini ya utawala wa Wajerumani hadi WW I akiwa askari ndani ya jeshi la Kamanda Von Lettow Vorbeck.
Anaendelea kueleza utawala wa Waingereza baada ya WW I 1918.
Anaeleza alivyounda African Association 1929 baada ya kukutana na Dr. Kweggiyr Aggrey 1924.
Anaendelea kueleza kilichomsukuma kuunda Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika 1933 kikiwa chama pembeni ya AA.
Hapa katika miaka ya 1930s anaeleza juhudi za Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika katika kujenga shule ili Waislam kama Wamishionari wawe na shule zao akiweka msisitizo wa Qur'an kusomeshwa kama somo katika shule.
Kleist anaeleza ushawishi wa Waislam katika taasisi hizi mbili AA na Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na nguvu iliyozuka katika kukabiliana na ukoloni.
Abdul haya licha ya kuwa yameandikwa na baba yake lakini kazaliwa na kukua ndani ya historia hii na baada ya WWII na akiwa askari wa KAR ndani ya Burma Infantry akawa anaandika vipi vita hivi vilivyowasaidia Waafrika kujitambua na kuamua kudai uhuru wa Tanganyika.
Yeye binafsi alikuwa na mchango wake katika kuwakabiliaba na Waingereza kwanza kupitia Dockworkers Union kisha haada ya kuchukua uongozi wa TAA 1950 akiwa na Dr. Vedasto Kyaruzi.
Kipindi hiki ndicho kipindi muhimu sana katika historia ya TAA kwani vijana wengi kutoka Makerere College walijiunga na TAA mjini Dar-es-Salaam pale New Street.
Hiki ndicho kipindi cha bongo za kizazi kipya cha wakati ule akina Hamza Mwapachu na viongozi wengine kutoka Kanda ya Ziwa kama Ali Migeyo, Saadan Abdu Kandoro na Paul Bomani wakaanza kukusanya nguvu zao pamoja kumkabili Gavana Edward Francis Twining.
Abdul na Hamza Mwapachu wanaweka msingi wa kuunda TANU na kutafuta kiongozi mmoja kuongoza harakati za uhuru.
Abdul yeye alimtaka Chief David Kidaha Makwaia ndiye aje TAA waunde TANU.
Mwapachu yeye mtu wake alikuwa Julius Nyerere lakini mwaka wa 1950 Nyerere alikuwa hajulikani wakati Chief Kidaha alikuwa mjumbe wa LEGCO toka mwaka wa 1945.
Abdul Sykes 1950 tayari alikuwa kijana maarufu na kiongozi wa TAA na alikuwa mjumbe katika TAA Political Subcommitee pamoja na Mwapachu, Kyaruzi, Sheikh Hassan bin Ameir na Steven Mhando kwa kawataja wachache.
Huu ndiyo mwaka Abdul Sykes alikwenda Nairobi kufanya mazungumzo na Jomo Kenyatta.
Hii kamati ndani yake alikuwapo Mwanasheria Earle Seaton akitoa ushauri nyuma ya pazia.
Hii ndiyo kamati akiwemo Dossa Aziz na John Rupia iliyokuja kuunda chama cha TANU 1954.
Lakini muhimu alieleza mkutano nyumbani kwa Hamza Mwapachu, Nansio, Ukerewe alipokwenda kaongozana na Ali Mwinyi Tambwe agenda kuu ikiwa kupata kauli ya Mwapachu kuhusu kumtia Nyerere kwenye uongozi wa juu kabisa wa TAA.
Hamza alimshauri Abdul kuwa Nyerere asaidiwe ashinde uchaguzi wa 1953 awe President na 1954 TANU iundwe.
Haya ndiyo Abdul aliyoandika katika kueleza chimbuko la TANU na Abdul akaeleza vipi alikuja kujuana na Nyerere 1952.
Inasemekana kuwa Julius Nyerere hakupendezewa na historia hii.
Abdul akajitoa katika ule mradi akamwacha Dr. Kleruu.
Naweka kitabu cha Abubakar Ulotu, ‘‘Historia ya TANU,’’ kitabu kilichotokana na utafiti na uandishi wa Dr. Wilbert Klerruu.
Hiki kitabu cha Abubakar Ulotu ni kutoka mswada wa historia ya TANU kilichokuwa kinaandikwa pale TANU Office na Abdul Sykes na Dr. Wilbard Kleruu mwaka wa 1962 Nyerere akihusika.
Kama nilivyoeleza hapo juu Abdul Sykes alijitoa katika uandishi wa historia ya TANU.
Dr. Kleruu akaendelea na uandishi hadi ukakamilika lakini TANU hawakuweza kukichapa kitabu kile.
Abubakar Ulotu akachukua mswada ule kwa siri na bila idhini ya TANU akachapa kitabu baada ya kufanya mabadiliko kidogo akaweka jina lake kama mwandishi.
Hivi sasa kipo kitabu cha maisha ya Julius Nyerere.
Muhimu kujua nini kimeandikwa kuhusu uasisi wa TANU na mchango wa Nyerere.
Waandishi wa kitabu hiki walifanya mahojiano na mwandishi kama picha zinavyoonyesha na walimtunuku nakala kwa mchango wake huo.