Lebanon yaishutumu Iran kwa kuingilia masuala yake ya ndani
Chanzo cha picha, Reuters
Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati ameelezea kughadhabishwa kwake na kauli iliyotolewa na spika wa bunge la Iran juu ya mustakabali wa kusini mwa Lebanon.
Spika wa Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amejitolea kufanya mazungumzo na Ufaransa kuhusu azimio nambari 1701 la Umoja wa Mataifa, ambalo lilimaliza mzozo mkubwa wa mwisho kati ya Israel na Hezbollah mwaka 2006 na kuupa Umoja wa Mataifa mamlaka ya kulisaidia jeshi la Lebanon kudumisha amani.
Mikati alielezea kauli ya Iran kama "uingiliaji wa wazi katika masuala ya Lebanon na jaribio la kuanzisha ulezi usiokubalika dhidi ya Lebanon".
Hezbollah inachukuliwa kuwa wakala wa Iran - ambayo hutoa ufadhili wake mwingi na silaha - na kwa kambi yake kubwa ya wabunge bungeni, ina ushawishi mkubwa kwa serikali ya Lebanon.
Qalibaf alikuwa Lebanon wikendi iliyopita tu, alipokutana na waziri mkuu.
Mikati anasema ameomba baraza la mawaziri la Iran kutoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa hiyo - akiongeza kwamba mazungumzo yoyote kuhusu Azimio nambari 1701 yanapaswa kufanywa na serikali ya Lebanon.