Ritz, huwa nawatazama hawa watoto wa smart phones nawaona hawana ujanja wowote. Acha tu yaani, tunaongelea enzi hizo za watoto wa Oysterbay kufanya sherehe halafu sisi watoto wa upanga mashariki tunakwenda kwa miguu kwenye nyumba ya mtu fulani. Party ikimalizika kulikuwa hakuna mambo ya boda boda au bajaji, watu wakanyaga kwa miguu taratibu kutoka mitaa ya Obay, wanavuka salender Brigde wanakunja kushoto kuitafuta Aga Khan, wakivuka Gymkhana, yanakuwepo makundi mawili, mmoja linaelekea shaaban robert na jingine linakuwa ni la watoto wa mirambo na ohio kwenye maghorofa ya Railways.
Watu walikuwa wanazifuata party za usiku kwa miguu, lakini walikuwepo wezi wa magari ya baba, wanavizia wazee wamelala, wanaenda gereji wanalisukuma gari taratibu mpaka kwenye kona ya mtaa halafu ndio linawashwa. Mwenye gari mara nyingi hana hela ya mafuta, anafanya kuwaambia marafiki zake wachange ili waweze kwenda na kurudi nyumbani bila ya baba kushtukia mchezo asubuhi ya siku inayofuata.