Prof Lipumba achukua fomu kuwania urais
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ametangaza rasmi azma yake ya kuchukua fomu ya kuwania kugombea nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Hii itakuwa ni mara yake ya nne kuwania nafasi hiyo kupitia chama chake kwa upande wa Tanzania Bara.
Profesa Lipumba alisema ameamua kuchukua fomu ya kuwania Urais ili kuhakikisha nchi inatoka katika tatizo la uongozi dhaifu pamoja na CCM iliyogawanyika.
Aliwaomba wanachama wa CUF pamoja na wananchi kumuunga mkono katika hatua yake hiyo.
"Wana CUF na wananchi wote mnatakiwa kuungana ili tuweze kufanya mabadiliko, hili CUF inaweza kufanya endapo itapewa ridhaa ya kupewa madaraka...Nawahakikishia kama tukiongoza nchi tutatembea juu ya maneno yetu na sio vinginevyo," alisema.
Akitangaza azma yake hiyo wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la chama hicho kilichofanyika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, Lipumba aliitupia serikali lawama kutokana na matatizo mengi yanayoikabili nchi.
Alisema hali ya nchi kwa sasa kuanzia kisiasa, kiuchumi na kijamii inatisha kutokana na Rais Kikwete kushindwa kuwajibika kiutendaji.
Lipumba alisema katika kujikomboa umefika wakati sasa kwa wananchi kuanza kazi ya kudai mabadiliko ya haraka ili nchi iondokane na hali duni iliyopo hivi sasa.
Alisema, wananchi wa kipato cha chini ndio wanaopata athari za kuyumba kwa uongozi baada ya bei za bidhaa mbalimbali kupanda mara nne ya bei ya huko nyuma pamoja na nafasi za ajira kupungua na kusababisha kundi la watu maskini kukua kwa kasi.
Mwenyekiti huyo wa CUF alisema, katika ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia imeonyesha kati ya Watanzania 100, watu 89 hawana ajira na hivyo inaonyesha dhahiri hata maelezo ya serikali inayosema watu wengi wamepata ajira kuwa ya uwongo.
Aliongeza kwamba katika kipindi chote cha CCM kuwepo madarakani hakuna sekta iliyoonyesha kuboreka na kutoa mfano wa huduma ya umeme, barabara, maji afya na elimu kuwa mbaya na hivyo kuhatarisha mwenendo wa ukuaji wa uchumi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI