Ukumbi wa mikutano wa White House uliopo Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini hapa, jana ulizizima kiasi cha baadhi ya wajumbe kutokwa machozi, wakati Edward Lowassa aliposimama kwa mara ya kwanza na kujibu tuhuma mbalimbali za ufisadi zinazomkabili.
Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli, alikuwa mtu wa kwanza kusimama na kuchangia ajenda ya kujivua gamba iliyosomwa katika kikao hicho na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Pius Msekwa.
Kabla ya Lowassa kusimama na kuanza kutoa utetezi wake, Msekwa aliwaeleza wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kwamba, Kamati Kuu ya chama hicho ilikuwa imependekeza kurejeshwa kwa suala hilo katika Kamati ya Maadili. Katika maelezo yake Msekwa alisema, uamuzi wa kulirejesha suala hilo katika kamati ya maadili linafanyika baada ya watuhumiwa wawili, Lowassa na Andrew Chenge kutotekeleza maazimio ya kikao cha NEC kilichowataka wapime wenyewe vinginevyo chama kingechukua hatua dhidi yao.
Akizungumza akiwa mtulivu, Lowassa alianza kwa kuunga mkono uamuzi huo wa suala lao kupelekwa katika Kamati ya Maadili akieleza huo ndiyo utamaduni wa CCM anaoufahamu vyema tangu alipojiunga na chama hicho miaka ya mwanzo ya 1975 baada kumaliza elimu yake ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika hilo, pasipo kuwataja Lowassa alieleza kushangazwa na viongozi wa juu wa chama hicho kukaa kimya pasipo kuchukua hatua zozote wakati wote Nape na Chiligati walipokuwa wakipita na kumshambulia kwa tuhuma zisizo na ukweli wala ushahidi.
Akimuelekezea hoja zake Rais Kikwete, mbunge huyo wa Monduli Lowassa alisema viongozi hao wamekuwa wakimhusisha na tuhuma za ufisadi kupitia mkataba wa Richmond wakati rais akijua kwamba hakuna jambo alilofanya ambalo yeye Kikwete hakulifahamu au ambalo hakumtuma yeye.
Lowassa ambaye katika utetezi wake alikuwa ameshika mkononi hansard ya Bunge alisema, Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ambayo ilisababisha ajiuzulu uwaziri mkuu, Februari mwaka 2008 ilisema bayana kwamba alifikia hatua hiyo kutokana na makosa ya watendaji wa chini yake. Mbali ya hilo, Lowassa alirejea kauli za Kikwete mwenyewe ndani ya vikao vilivyopita vya NEC ambako alipata kukaririwa zaidi ya mara moja akisema kulikuwa hakuna ushahidi wa rushwa katika Richmond.
Kama hiyo haitoshi, aligusia pia matamshi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndani ya Bunge ambayo yalithibitisha kutokuwapo kwa rushwa katika mchakato ulioipa zabuni kampuni ya Richmond hata kufikia hatua za kutowaadhibu hata wale ambao majina yao yalitajwa moja kwa moja kwenye ripoti ya Kamati Teule ya Bunge. Baada ya kulijadili hilo, Lowassa alikumbusha historia ya neno ‘ufisadi' akisema lililetwa na CHADEMA kupitia mkutano wa Mwembeyanga na kuwataja viongozi 11 wa CCM akiwamo yeye kwa ufisadi.
Mwanasiasa huyo alisema, katika tamko hilo la CHADEMA, alijumuishwa katika orodha ya mafisadi akihusishwa na uamuzi wake wa kuuvunja mkataba wa City Water ambao hata hivyo baadaye serikali ilishinda kesi katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa mizozo ya uwekezaji. Alisema ni jambo la ajabu kwamba viongozi wa CCM walilidaka neno hilo na kuanza kulitumia kuwashambulia wenzao akiwamo yeye katika mambo ambayo hayakuwa na ukweli.
Alipofika hatua hiyo alihoji, Nape anapata wapi ‘moral authority' (uhalali wa kimaadili) wa kumtuhumu yeye kwa ufisadi hata kudai kwamba amekipotezea heshima chama hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Akifafanua, alisema matokeo ya kura alizopata Rais na yeye mwenyewe katika jimbo la Monduli unazidi asilimia 89 na kwamba wakati yeye (Lowassa) na wengine wakipambana kukijenga na kukipigania chama chao kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, Nape na wanasiasa wengine wanaomshambulia walikuwa katika harakati za kusajili Chama cha Jamii (CCJ).
Akirejea tuhuma dhidi yake ambazo hazina ushahidi huku akitumia neno la Kiingereza, ‘perception' Lowassa alimkumbusha Kikwete jinsi yeye (Kikwete) alivyozushiwa tuhuma za ukosefu wa maadili na mwanasiasa mkongwe Paul Sozigwa mwaka 2003. Lowassa alisema katika tuhuma hizo dhidi ya Kikwete ambazo ziliwasilishwa mbele ya kikao na Sozingwa kwa niaba ya Kamati ya Maadili, zilizimwa kwa hekima ya mwenyekiti wa CCM wakati huo Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
"Mheshimiwa Mwenyekiti naamini kama si hekima za mzee wetu Mkapa wakati ule, leo hii usingekuwa umekaa katika kiti hicho," alisema Lowassa ambaye alisisitiza ni makosa kuwahukumu watu pasipo ushahidi. Alisema kama kungekuwa na makosa aliyotenda, kanuni za CCM ziko wazi na zingefuatwa ikiwa ni pamoja na kuitwa katika kamati ya maadili ambako angehojiwa juu ya tuhuma hizo.
"CCM ninayoifahamu ni ile inayotenda haki na hakiwezi kumtuhumu mtu hadharani bila ushahidi kama walivyofanya Chiligati na Nape na kwa mujibu wa kanuni ni vibaya kumtuhumu bila vikao vya maadili ya chama," alisema.
Fredrick Sumaye amuunga mkono
Akichangia mjadala huo ambao hasa ulihusu uamuzi wa kurejesha hoja ya dhana ya kujivua gamba na tuhuma za ufisadi kwa kamati ya maadili, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliungana na Lowassa kuhoji busara ya kuitwa na kuhojiwa wakati tuhuma zimeishasambazwa nchi nzima. Sumaye alisema halikuwa jambo la busara kuwatuhumu watu na kutangaza tuhuma dhidi yao kabla ya kuthibitishwa kwa tuhuma zenyewe.
Alikwenda mbali zaidi na kuhoji iwapo kamati ya maadili itabaini kuwa Lowassa hakuwa na hatia, hatua gani zitachukuliwa dhidi ya Chiligati na Nape waliosambaza tuhuma hizo wakati viongozi wa juu akiwamo mwenyekiti wakiwa kimya? "Kama mtu ametuhumiwa kwa stahili hii nchi nzima, alafu uchunguzi ukibaini kuwa alionewa, watamfanyaje? Kama Nape na Chiligati wakibainika kuwa walimwonea, wachukuliwe hatua gani? alihoji Sumaye.
Maneno hayo ya Sumaye mara moja yalijibiwa na Rais Kikwete ambaye alisema hilo likithibishwa, kutakuwa hakuna njia isipokuwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Sumaye alipokaa aliinuka Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha ambaye naye alieleza kusikitishwa na hatua ya kuzusha tuhuma nzito dhidi ya watu wengine pasipo kuzithibitisha.
Mara tu baada ya mjumbe huyo kuzungumza, Rais Kikwete kwa ushauri wa Mkapa aliwaomba wajumbe kulimaliza jambo hilo akisema ‘imetosha'.
Wakati akifunga mjadala huo mmoja wa watu waliokuwa wamenyosha mkono wakitaka kuchangia alikuwa ni mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru. Akihitimisha mjadala huo kwa angalizo, Rais Kikwete alisema suala hilo linapelekwa katika Kamati ya Maadili ambako aliwataka kuwasilisha ushahidi wa vielelezo na siyo hujuma dhidi ya watuhumiwa.