WATU wanne akiwemo mkazi wa Magomeni
Mapipa, Muharami Abdallah maarufu kama
Chonji (44), wameburuzwa kortini kwa tuhuma
za kusafirisha dawa za kulevya zenye thamani
ya zaidi ya Sh milioni 281.
Mbali na Chonji, washitakiwa wengine ni
Abdul Chumbi (37), Rehamni Umande (45),
Tanaka Mwakasagule (35) na Maliki Maunda
(29).
Washitakiwa hao walifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakiwa
chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi na
kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu
Mkazi, Janeth Kaluyenda.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka
alidai washitakiwa hao wanakabiliwa na
mashitaka mawili ya kusafirisha dawa za
kulevya aina mbili.
Ilidaiwa kuwa Oktoba 21 mwaka huu,
washitakiwa wakiwa eneo la Magomeni
Makanya ndani ya Wilaya ya Kinondoni
walikutwa wakijihusisha na biashara ya gramu
4547.49 za dawa za kulevya aina ya heroin,
zenye thamani ya Sh 227,374,500 huku
wakijua ni kinyume cha sheria.