Ukisoma historia ya Waisraeli, utaona jinsi Mungu alivyotoa mapigo kumi kwa Wamisri waliokataa kumtii. Mojawapo ya mapigo hayo ni majipu mabaya yaliyowakumba watu wa Misri (Kutoka 9:8–11). Hili lilikuwa onyo kwamba Mungu anaweza hata kutumia magonjwa kama fimbo ya kuwaadhibu wale wanaokataa kuishi katika njia zake.
Leo hii, tunashuhudia jinsi magonjwa ya zinaa (STDs) yanavyoenea kwa kasi. Wanasayansi wamejitahidi sana kutengeneza dawa, chanjo, na mbinu za kinga, lakini kila kukicha magonjwa mapya yanaibuka, kama vile UKIMWI (AIDS) ambao mpaka sasa bado hauna tiba kamili. Hata yale magonjwa ya zinaa yaliyokuwa yakidhibitiwa kwa urahisi zamani, sasa yamekuwa sugu dhidi ya dawa nyingi. Je, hii inaweza kuwa ishara kwamba wanadamu wanapopuuza sheria za Mungu, wanajitafutia mapigo yasiyo na suluhisho?
Mungu hapendezwi na uzinzi na uasherati, ndio sababu amesema wazi katika Maandiko kwamba wanaofanya dhambi hizo watakuwa miongoni mwa watu watakaotupwa motoni milele. Biblia inaonya sana tuikimbie zinaa na kujiepusha na uasherati. Mtu asiyeweza kujizuia, anatakiwa aoe au kuolewa badala ya kufanya uzinzi.
Maandiko yanatuambia tena kwamba "...yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye." Kwa mantiki hiyo, naamini hata magonjwa ya zinaa ni kiboko cha kuwarudi wanaopenda uzinzi na uasherati. Na wakiendelea kukaidi, ziwa la moto wa milele linawangojea.
Njia pekee ya kuepuka mapigo hayo ya sasa na yale ya milele, ni kutubu dhambi, kuacha uzinzi na uasherati, na kuishi maisha safi ya kumpendeza Mungu.
Inawezekana unatamani kuacha uzinzi lakini kila ukijaribu unashindwa. Yesu anakuita leo akupumzishe mzigo huo, unaokusumbua na kukulemea (Mathayo 11:28).