WAKATI mgogoro wa kodi ya pango kati ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Taasisi ya Moyo Tanzania (THI), nyaraka za kumchafua mwanzilishi wa THI Dk Ferdinand Masau zimesambazwa katika mtandao zikidai kuwa hana sifa ya kufanya upasuaji wa moyo.
Lakini Dk Masau amekanusha tuhuma hizo jana akisema ni za kubuni zenye ni ya kumchafulia jina lake kwa kuwa yeye ana sifa zote zinazostahili.
Nyaraka za kumchafua Dk huyo zilizosambazwa katika mtandao na watu wasiojulikana zinaeleza kuwa jina la Dk Masau halipo katika Bodi ya Madaktari ya Jiji la Texas nchini Marekani ambako yeye anadai alisomea.
Mwandishi wa taarifa hizo aliandika: "Nimeongea na wahusika wa Jimbo la Texas, kitengo cha Texas Medical
Board, pamoja na shule ya Dk. Masau, kitengo cha Texas Heart Institute, na nimethibitisha kwamba Dk. Masau hakuwahi kuwa mganga Houston, Texas.
"Jina lake halipo katika waganga waliowahi kuruhusiwa kutibu mtu Texas na kwamba elimu ya upasuaji moyo aliyoipata Texas Heart Institute sio "accredited program." Hata wakati anajifunza, hakuruhusiwa kugusa mgonjwa wa moyo ila kuangalia tu wanavyopasua.
Mwandishi huyo ambaye hakuweka bayana nia ya kufuatilia taarifa hizo, aliongeza kuwa, "Nimewasiliana na kampuni ya wanasheria ya Houston, Hartley Hampton P.C. kuangalia kama wanaweza kushughulikia hili suala. Wanajadili maombi yangu hadi hivi sasa tunavyozungumza,"
Dk Masau kwa upande wake, aliiambia Mwananchi Jumapili jana kuwa ameziona tuhuma hizo kwenye mtandao na kwamba tayari amezijibu kupitia barua pepe kwenda kwa mtu aliyemuulizia kuhusu tuhuma hizo.
"Nisingependa kujiingiza kwenye malumbano au majadiliano yao na wala sipingi wao kuendelea na mijadala yao na hasa kwa vile wote siwajui na wanatumia majina ya kuficha," alisema Dk Masau.
Alisema watu kama hao ni wahuni wana lengo kumchafulia jina ingawa yeye anaamini kuwa atapigana vita hivyo mpaka mwisho bila kuchoka.
Alipoulizwa kama ana mpango wa kurudi kufanya kazi Texas na kuungana na familia yake kutokana na upinzani unaomkabili tangu alipoanzisha taasisi hiyo, alisema hana mpango wa kurudi huko kwani bado ana wito wa kuokoa maisha ya Watanzania.
Alisema Watanzania wengi wenye matatizo ya moyo wanateseka na kufa kwa kukosa huduma hiyo, hivyo ni wajibu wake kuwasaidia na ndiyo maana alirudi nchini na kwamba kama angehitaji kufanya kazi huko asingerudi kabisa.
Kuhusu elimu yake, Dk Masau alisema wakati anakwenda Taasisi ya Moyo Texas, alikuwa ameshamaliza masomo yake ya udaktari na kusajiliwa na Baraza la Madaktari Tanzania (MCT) mwaka 1995 kama mtaalamu mwenye Shahada ya Udhamiri katika upasuaji wa moyo, kifua na mishipa ya damu.
Alifafanua kuwa wakati akiwa hapa nchini aliwahi kufanyakazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) katika fani hiyo hadi alipoamua kwenda Texas mwishoni mwa mwaka 1996.
Alisema safari yake ya kwenda huko ilidhaminiwa na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Jamii cha Texas Houston Januari 1997 hadi Juni 2000 na katika kipindi hicho alishiriki katika kufanya upasuaji wa moyo zaidi ya 1,800.
"Wakati nikiwa Texas sikuwa chini ya Bodi ya Madaktari wa Texas
na hivyo sikuhitaji kuwa na leseni kutoka huko na wala sijawahi kuwasiliana nayo, kwani ingekuwa na maana tu kwangu iwapo ningetaka kubaki na kufanyia kazi huko Texas. Mimi lengo langu lilikuwa ni mafunzo na kurudi nyumbani," alisema Dk Masau.
Dk Masau alisema bado anaendeleza ushirikiano mzuri na Texas Heart Institute na Texas Children's Hospital kiasi kwamba bado anashirikiana nao katika kufanya upasuaji pale anapoomba au kuhitaji na kwamba taasisi hizo mbili ni miongoni wa wafadhili wakubwa wa taasisi yake.
Kwa mujibu Dk Masau yeye ni mwanachama Chama cha Kimataiafa cha wapasuaji wa moyo ‘Society of Thoracic Surgeons' na mmoja wa wajumbe katika Kamati maalumu ya Chama hicho ‘Workforce of International Relationship of the Society of Thoracic Surgeons' tangu mwaka 2002 hadi mwaka huu.??
"Nimekuwa mwenyekiti wa Taifa ya kamati ya uandaaji wa Mkutano
Wa Tano wa kimataifa Barani Afrika unaohusu semina ya upasuaji wa moyo wa mwaka 2008 chini ya Mkurugenzi wa Mafunzo Prof Charles Yankah wa Taasisi ya Moyo Berlin, Ujerumani (BHI) na Chuo Kikuu cha Berlin pamoja na Dk. Willie Koen kutoka Christian Barnaard Memorial Hospital, Cape Town, Afrika Kusini.?
Katika hatua nyingine, alisema mwezi ujao amealikwa kuwa mgeni rasmi kushiriki katika mkutano wa ushirikiano wa nchi za Ulaya na Amerika unaohusu wataalam wa upasuaji wa kifua na mishipa ya damu unaolenga kujadili uwezekano wa kupata taarifa za awali kuhusu kuanzisha mfuko wa jamii ya wapasuaji wa kifua unaotambulika kama Mfuko wa Moyo Afrika (AHF).
Katika siku za karibuni Dk Masau amekuwa katika mgogoro na NSSF inayotaka kuhamisha wagonjwa katika taasisi yake kwa madai kwamba amekuwa halipi pango, jambo ambalo yeye analipinga na mgogoro huo bado uko mahakamani.