Habari za asubuhi wana JF?
Kumekuwa na tatizo la kiuandishi kwa watu wengi kuanzia humu JF mpaka kwingineko kote kwenye mitandao ya kijamii mwanzo nilidhani ni kujisahau lakini sasa naona kama imezoeleka na kuonekana kama ni maneno ya kawaida kwenye kiswahili na watu wala hawastuki kuona kama ni makosa,yaani makosa yakirudiwa rudiwa mara nyingi huzoeleka na kuonekana ni usahihi
Naomba nitoe mifano michache ya hayo maneno hapa chini;
Nisamee badala ya Nisamehe
Eshima badala ya Heshima
Asubui badala ya Asubuhi
Mdogo angu badala ya Mdogo wangu
Kiac badala ya kiasi
Awez badala ya Hawezi
Ujaacha badala ya Hujaacha
Uendelei badala ya Huendelei
Utamsikia Mtangazaji anasema Nyimbo hii badala ya kusema wimbo huu
Yako maneno mengi sana yanayopotoshwa na wadau wengi humu ndani,ombi langu tu ndugu zangu tubadilike tuandike maneno kwa usahihi wake kwa sababu humu ndani panapitiwa na wanafunzi kuanzia Shule za Msingi,Sekondari na hata Vyuo wanajifunza nini juu ya tunayoyaandika humu?
Eti hapo ndio tunawadharau Wakenya hawajui Kiswahili hawajui kiswahili wakati sisi wenyewe ndio tunavuruga tu.
Ni hayo tu wadau muwe na Jumapili njema
Asante!
Pole mkuu, hata mimi Jumamosi iliyopita niliandika mada yenye kichwa cha habari "Mtihani wa Kiswahili kwa rais Magufuli". Unaweza kusoma kwa undani zaidi nilichoandika hapo chini.
Lugha yetu ya Kiswili ni moja kati ya lugha maaarufu hapa duniani na kwa sababu hii yapaswa tujivunie. Lakini si hivyo tu, yapaswa pia kuilinda na kuiendeleza ili izidi kuwa maaarufu. Kwa bahati mbaya nafikiri kama taifa tunapoteza mwelekeo wa kuienzi lugha yetu na mimi nikiwa kama mzalendo wa nchi yangu najisikia nina jukumu la kutoa mchango wangu.
Pamoja na tofauti za kifikra kwenye baadhi ya mambo kati yangu na rais Magufuli lakini kuna kitu kimoja kinatuunganisha, kupenda lugha yetu ya Kiswahili. Kwa sababu hii natuma ombi langu moja kwa moja kwa rais ili tuweze kuijenga lugha yetu na naamini kama akisoma ujumbe huu atachukua hatua. Wengine wanaweza kupuuza wito huu na kuona una umuhimu mdogo kwa taifa lakini si kweli kwa sababu nitakazo zielezea. Kwa mfano, moja ya sababu kwanini filamu, nyimbo na vitabu vya Kiingereza ni maarufu ni kwasababu lugha hiyo inaeleweka sehemu nyingi duniani. Ndio maana wasanii wao nao pia wanakuwa na mafanikio makubwa kwa sababu wana soko kubwa ukizingatia kuwa kazi zao zinanunuliwa sehemu mbalimbali duniani na kuingizia mapato serikali zao kutokana na kodi. Sababu hiyo hiyo pia ndio inawafanya wasanii wetu wafanye vizuri hususani hapa Afrika Mashariki kutokana na watu kuielewa lugha ya Kiswahili. Mpaka hapa utaona ni kwa jinsi gani lugha inaweza kuinua wasanii na kuchangia pato la taifa.
Lakini pia kuna changamoto zinazoikabili lugha yetu na ili kuhakikisha inaendelea kuwa lugha ya kuvutia kuna hatua inabidi zichukuliwe. Kuna changamoto kubwa mbili nimeona nizitaje.
1. Kutojivunia lugha ya Kiswahili
Watanzania tuna uwezo mkubwa wa kuongea lugha ya Kiswahili sanifu lakini cha kusikitisha kuna baadhi ya watu hawajivunii Kiswahili. Kwa mfanao kuna baadhi ya watu hawawezi kuongea sentensi moja bila kutia neno la Kiingereza. Kuna siku moja hapa Jamii Forums nilimkosoa bwana mmoja tena ni mwandishi wa habari kwa kuchanganya maneno ya Kiswahili na Kiingereza kwenye sentensi. Nilimwambia kama mimi ninakaa Ulaya kwa karibu miaka ishirini na nina mke na watoto ambao wanaongea Kiingereza nyumbani kwangu lakini bado naandika Kiswahili fasaha kwanini wewe usiweze? Akanijibu kwamba wakati mwingine ni rahisi kujielezea kwa lugha ya Kiingereza kitu ambacho sikubaliani nae kwa asilimia mia. Naelewa kuwa wakati mwingine unaweza kuazima maneno lakini kuna watu wanapenda kuazima maneno mengi ya Kiingereza bila ya ulazima. Ni kitu ambacho kinakera zaidi kuwaona watangazaji na watu maharufu wakitumia maneno ya Kiingereza pasipo na lazima na wao ndio kioo cha jamii.
2. Kukosekana kwa chombo madhubuti cha kuboresha Kiswahili
Aya hii ndiyo ningependa rais aingalie kwa makini zaidi kwakuwa inaihusu chombo kinachosimamiwa na serikali.
BAKITA kama chombo cha kusimamia Kiswahili Tanzania sidhani kama kinafanya kazi nzuri. Kazi wanayoifanya nina uhakika hata ukimpa mtoto wa miaka saba pia ataweza kuifanya. Nafikiri BAKITA ina watu wavivu na wakosefu wa ubunifu.
Yaani kila neno lazima lianze na ki…, kwa mfanao, kicharazio (keyboard), kitanza mbali (remote control) n.k. Nina uhakika hata ukiiambia BAKITA ibuni tafsiri ya rocket watakwambia kiendea mwezini, kazi ambayo hata mtoto wa miaka saba anaweza kuifanya. Au maneno mengine kama runinga (television), neno limekaa utafikiri la Kinyarwanda vile. Kwani mpaka kila neno liwe na kifanyia hivi, kifanyia vile... Lugha ni nzuri lakini kuna mijitu inataka kuiharibu kwa ajili ya uvivu wa kufikiri halafu inalipwa mshahara na pesa za walipa kodi.
Ningependekeza serikali iiangalie kwa karibu BAKITA na kuhakikisha inafanya kazi kwa ubunifu wa maneno mazuri ya Kiswahili. Pia kuchukua hatua ya kuwabadilisha wale wenye majukumu ya kubuni maneno mapya ya Kiswahili mara moja pale inapoonekana wanazembea.
Serikali kuwaadhibu waandishi wa habari na watangazaji ambao watashindwa kutumia Kiswahili sanifu. Kwa mfano, kuyapiga faini magazeti vya radio na runinga pale inapobainika wafanyakazi wao wanashindwa kuongea Kiswahili fasaha au wanapoazima maneno ya Kiingereza bila sababu ya msingi.
Huu ni mtihani wako rais Magufuli na naamini kwa sababu wewe ni mpenzi wa Kiswahili kama mimi hutaniangusha.