Habari za asubuhi wana JF?
Kumekuwa na tatizo la kiuandishi kwa watu wengi kuanzia humu JF mpaka kwingineko kote kwenye mitandao ya kijamii mwanzo nilidhani ni kujisahau lakini sasa naona kama imezoeleka na kuonekana kama ni maneno ya kawaida kwenye kiswahili na watu wala hawastuki kuona kama ni makosa,yaani makosa yakirudiwa rudiwa mara nyingi huzoeleka na kuonekana ni usahihi
Naomba nitoe mifano michache ya hayo maneno hapa chini;
Nisamee badala ya Nisamehe
Eshima badala ya Heshima
Asubui badala ya Asubuhi
Mdogo angu badala ya Mdogo wangu
Kiac badala ya kiasi
Awez badala ya Hawezi
Ujaacha badala ya Hujaacha
Uendelei badala ya Huendelei
Utamsikia Mtangazaji anasema Nyimbo hii badala ya kusema wimbo huu
Yako maneno mengi sana yanayopotoshwa na wadau wengi humu ndani,ombi langu tu ndugu zangu tubadilike tuandike maneno kwa usahihi wake kwa sababu humu ndani panapitiwa na wanafunzi kuanzia Shule za Msingi,Sekondari na hata Vyuo wanajifunza nini juu ya tunayoyaandika humu?
Eti hapo ndio tunawadharau Wakenya hawajui Kiswahili hawajui kiswahili wakati sisi wenyewe ndio tunavuruga tu.
Ni hayo tu wadau muwe na Jumapili njema
Asante!
FaizaFoxy Kauona huu uzi?
Mfano mwingine "kuoana" badala ya kuoa (mwanamme) au kuolewa (mwanamke). Katika Kiswahili hakuna kuoana, mwanamme anamuoa mwanamke. Sijui kama watu wanatafsiri moja kwa moja kutoka tamaduni ngeni kama za Waingereza ambazo watu wote "wanaoana" sawa, hakuna anayemuoa mwingine, au ndiyokukipelekaKiswahili kwenye mantiki za zama za leo, ambapousawa wa binadamu unatamalaki zaidi na hivyo habari za "kuoa" na "kuolewa" zinapitwa na wakati bila mjadala?
Kuna sheria moja ya fizikia huwa naipenda sana kuiongelea, ni ya fizikia, lakini ina mantiki hata kwenye lugha, kwa kweli, inamantiki kwa kitu chochote kilichopo katika muda, maana yake, ina mantiki kwa yote ulimwenguni.
Sheria hii, inasema kwamba
2nd Law of Thermodynamics
The Second Law of Thermodynamics states that the state of entropy of the entire universe, as an isolated system, will always increase over time. The second law also states that the changes in the entropy in the universe can never be negative.
Kwa kifupi, sheria hii inasema kwamba, katika mfumo uliojifunga, mambo yanaenda yakizidi kukongoroka na kuharibika na kukosa mpango mzuri kadiri muda unavyozidi kwenda meble.
Kwa maneno mengine, ili chumba kibakiekisafi, inabidikifagiliwe na kusafishwa kila baada ya muda fulani.
Ili mfumo uendelee kuwa mzuri, inabidi kazi ifanyike kuurekebisha.
Ili lugha iendelee kustawi, inabidi kazi ya kuistawisha ifanywe.
Ndiyo maana, hata ukifunga chumba kibaki kitupu, utaona vitu vinakongoroka, buibui zinatanda,vumbi linatapakaa,mambo yanakongoroka, wadudu wanazagaa.
Kwa nini naitaja hii sheria katika mjadala wa lugha?
Lugha nayo inafuata sheria hii.
Hata pale watu wanapojitahidi kuilinda isiharibike. Ukifuatilia somo la "etymology" (vyanzo vya na historia ya maneno) utaona hili. Ukisoma Kiswahili cha vitabu vya Shaaban Robert, na Kiswahili cha leo, kuna tofauti.
Sasa kuna tofauti moja ni ya kiasili tu, kutokana na watu wa lahaja tofauti kuunganika pamoja mijini. Labda zamani mijini tulikaa wenyewe watu wa mwambao wengi, na ndugu zetu waliotoka bara wachache waliweza kujifunza Kiswahili cha mwambao, na leo wamekuja watu wa bara wengi mjini, na wengine ambao wako bara wamepata nafasi ya kuwa online wengi.
Hapo utaona watu ambao kwa mfano, lugha yao ya asili ni Kisukuma, Kiswahili wamejifunzia ukubwani, wakiandika na kusema Kiswahili chenye makosa.
Pia, kama utamaduni, wengi hatuna tabia ya kukarafati mambo. Kama gari tutataka liende mpaka liharibike sana ndiyo tujue kuna kutengeneza, kama nyumba hata hatupaki rangi, tunasubiri mpaka kuta zitake kuanguka, kama ni lugha, tunaona hakuna haja ya kufundisha misingi sana, ukimkosoa mtu kwa nia njema kabisa ya kumfunza lugha, katumia lugha vibaya, unaweza kuona anakwambia "si umeelewa?"
Hili si katika lugha tu.
Lugha ni sehemu ndogo tu ya mmomonyoko huu. Ukiangalia suala zima la utaifa, tumeshaona kwamba kazi ya kujenga umoja wa kitaifa imemalizwa na kina Nyerere na Karume, sisi sasa taifa moja na tutaendelea kuwa taifa moja tu, wakati ukweli ni kwamba kazi ya kujenga umoja wa kitaifa haiishi, kila siku inatakiwa kupaliliwa upya, tuondoe ukabila, tuweke utaifa.
Bahati mbaya sana hatufikirii hivyo, ukabila unashamiri.
Siasa zinategemea wananchi wawe wajinga wasijue kudai haki zao, ujinga huu ni mtaji wa watawala.
Hivyo hata wahitimu wa vyuo vikuu hawajui lugha, si Kiingereza tu ambacho tutasema lugha "ya kuja kwa meli", bali hata Kiswahili.
Kiswahili ni tatizo, kuanzia rais mwenye Ph.D, mpaka watoto wauza maji barabarani.
Na hili tatizo ni dalili ya ugonjwa, si ugonjwa wenyewe.
Ugonjwa wenyewe ni tabia ya kuridhika kwamba "tumeshamaliza kazi ya kujifunza Kiswahili, huku kiwingine watu watajifunzia mitaani tu".
Ndiyo maana leo, Tanzania watu wanaongea Kiswahili kuliko Kenya, lakini ukienda vyuo vikuu vya kimataifa, Wakenya wanaofundisha Kiswahili ni wengi kuliko Watanzania.