Mungu anaonekana kupitia kazi zake na uumbaji wake. Biblia inasema:
“Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake.” (Zaburi 19:1). Uumbaji wa dunia, uzuri wa maumbile, na mpangilio wa sayari ni ushuhuda tosha kuwa yupo Mungu aliye hai.
Fahamu tena kwamba Mungu alijifunua kwa njia ya manabii na mitume waliopokea maono, ufunuo, na maagizo kutoka kwake. Biblia ni ushuhuda wa mawasiliano ya Mungu na wanadamu.
Ingawa hakuna mtu aliyemuona Mungu ana kwa ana, watu walimuona Yesu Kristo, aliyekuja kwetu na "kuvaa" mwili wa kibinadamu. Yesu Kristo alisema: “Aliyeniona mimi amemwona Baba.” (Yohana 14:9)
Kwahiyo kutokumuona Mungu sio uthibitisho kwamba hayupo. Ni kama vile tusivyoweza kuuona upepo lakini athari ya upepo tunaiona. Matendo ya Mungu tunayaona: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye dhambi wanaokoka nk nk. Anza leo kumtafuta Mungu kwa imani utaona atakavyojidhihirisha kwako.