Inside10
JF-Expert Member
- May 20, 2011
- 29,909
- 32,414
TAARIFA KWA UMMA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linamshikilia Askari mmoja wa Jeshi la Magereza kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mwananchi mmoja tukio ambalo lilitokea Novemba 26,2024 majira ya saa 5:00 usiku huko katika Kitongoji cha Stendi, kata ya Mkwese Wilaya ya Manyoni Mkoa wa Singida.
Chanzo cha tukio hilo ni kwamba katika eneo hilo kuna wafuasi wa Chama cha Mapinduzi CCM walikuwa katika nyumba moja wakiwa na kikao chao cha ndani. Wakati kikao hicho kikiendelea walivamiwa na kundi la wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na vurugu kubwa kutokea ambapo askari magereza ambao wapo katika gereza ambalo lipo karibu na eneo hilo walipigiwa simu kujulishwa juu ya vurugu hizo ikabidi watoke kwenda kuona hali ilivyo huku wakiwasiliana na polisi, walipofika eneo la tukio walianza kushambuliwa kwa mawe jambo lililowalazimu kupiga risasi hewani kuwatahadharisha na kuwazuia watu waliokuwa wakiwashambulia kwa mawe.
Aidha, Katika purukushani hizo, risasi moja ilimjeruhi George Juma, (41), ambaye alikuwa mgombea wa kitongoji cha Stendi kupitia CHADEMA. Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ili kufanikisha kuwakamata wale wote waliosababisha vurugu hizo.
Jeshi la Polisi Singida linatoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kuendelea na shughuli za upigaji kura kuwachagua viongozi wao kwa amani na utulivu kwani Jeshi la Polisi liko imara katika ulinzi kipindi hiki cha kupiga kura na kutangaza matokeo kwa viongozi watakaochaguliwa.
Pia Jeshi la Polisi Singida linatoa onyo kwa mtu yeyote atakayevuruga zoezi la uchaguzi kwani halitasita kumchukulia hatua za kisheria.
Imetolewa na Amon Daudi Kakwale - SACP
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida.
Kuhusu kifo cha kada wa CHADEMA, soma LGE2024 - TANZIA - Manyoni: George Juma Mohamed, Mgombea wa CHADEMA auawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia tar 27, 11, 2024