Umepita mwaka mmoja sasa tangu marehemu Rais Magufuli alipoishutumu maabara ya taifa kwa kutoa majibu ya vipimo vya sampuli za mapapai, kware na mbuzi kuwa positive, kwa maana kwamba vitu hivyo vilionekana kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona. Tukio hili liliidhalilisha sana nchi yetu na lilisababisha nchi yetu kuonekana kuwa ni kituko cha dunia kwasababu njia hii haikuwa njia sahihi ya kuhakiki ubora wa vipimo vinavyofanywa na maabara hiyo. Cha kusikitisha zaidi ni kuwa rais Magufuli alifanya hivyo baada ya kupokea ushauri kutoka kwa aliyekuwa katibu mkuu wa wizara ya Afya, Prof. Mabula Mchembe.
Haijulikani sababu hasa zilizomfanya Prof. Mchembe kutoa ushauri ule, lakini, athari za ushauri ule zilikuwa ni kubwa kuliko ambavyo watanzania wengi wanafahamu. Watumishi wapatao 12 wa maabara hiyo hatimaye waliachishwa kazi kinyemela. Prof. Mchembe akishirikiana na mkurugenzi wa idara ya kinga, Dr. Leonard Subi na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu, Deodata Makani, wamewaondoa wafanyakazi 12 kutoka katika maabara hiyo na kuleta wafanyakazi wengine. Hata hivyo njia iliyotumika kuwapata watumishi wapya ilionekana kuwa na hila na upendeleo.
Prof. Mchembe na wenzake walitumia fursa hiyo kuwaingiza jamaa zao katika ajira ya mradi kuchukua nafasi ya watumishi walioondolewa bila kufuata taratibu halali. Inasemekana ameleta jamaa zake wawili, mtu na mkewe, walioletwa kutoka Simiyu na kuingizwa katika ajira hizo.
Watumishi wengi wa maabara hiyo, ikiwa ni pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa maabara, Dr. Nyambura Moremi, walikuwa wakifanya kazi kwa mkataba kupitia mradi wa Laboratory Support Program unaofadhiliwa na PEPFAR kupitia CDC. Kwa kawaida watumishi hawa husaini mikataba yao ya mwaka mmoja kila ifikapo Oktoba kulingana na mwaka wa fedha wa Marekani ambao ndio wafadhili.
Mwaka jana Oktoba 2020 wafanyakazi hao walipewa mikataba ya mwaka mmoja kama kawaida (Oktoba 2020 mpaka Septemba 2021) lakini zoezi la kuwapatia mikataba watumishi hao lilisitishwa na mikataba kurudishwa kwa maelekezo ya Mkurugenzi wa Utwala na Rasilimali watu, Deodata Makani. Kilichofuata, watumishi hao waliamriwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali ikiwemo barua ya maombi ya kazi, CV, barua ya ajira, barua ya kukubali mkataba, barua ya kupangiwa kituo cha kazi, cheti cha kuzaliwa, vyeti vya elimu na barua ya kuomba kuhuisha mikataba.
Jambo la kushangaza ni kwamba nyaraka hizi zilikuwemo katika mafaili ya watumishi hao hapo wizarani tangu walipoajiriwa. Baada ya kuwasilisha nyaraka hizo, watumishi hao walipewa mikataba ya miezi mitano (5) tu kuanzia Oktoba 2020 mpaka Februari 2021 badala ya mkataba wa mwaka mzima kama ilivyo kawaida ya miaka yote. Hii ilimaanisha kwamba mikataba ya mwaka mmoja waliyosainishwa awali mwezi Oktoba 2020 ilifutwa kinyemela.
Mwezi Januari, 2020 watumishi hao walipewa barua iliyoandikwa tarehe 22 Desemba 2020 ikiwa imesainiwa na katibu mkuu Prof. Mabula D. Mchembe. Barua hiyo ilinukuliwa kusema:-
“Kwa barua hii ninakutaarifu kuwa mara tu mkataba wako utakapokoma Wizara ya Afya haitakuongeza muda mwingine mpaka hapo taratibu za kiutumishi zitakapotolewa”
Ilipofika tarehe 13 Februari 2021, Deodata Makani aliitisha kikao na kuongea na watumishi wa mradi wa maabara. Watumishi walitaka kujua hatima yao baada ya tarehe 28 Februari 2021 (ambayo ndio ilikuwa tarehe ya mwisho ya mkataba wa miezi mitano). Katika kikao hicho, Deodata Makani aliwaambia watumishi kwamba nafasi za kazi za watumishi wa mradi wa maabara hazitotangazwa na kwamba watumishi hao wangeitwa kwenye usaili.
Ilipofika tarehe 17 Februari watumishi hao walipigiwa simu kuitwa kwenye usaili tarehe 18, 19 na 20 Februari. Siku ya usaili, mbali na watumishi wa mradi wa maabara, kulijitokeza watu wengine ambao haijulikani walitoka wapi au walipataje taarifa za usaili ule. Kabla ya kuanza usaili, Deodata Makani aliongea na watu wote waliofika kuhudhuria usaili. Baadhi ya watu hao walioonekana kuwa ni wageni kwa wafanyakazi wa maabara, waliuliza wameitiwa nini hapo, na wengine waliuliza ni nafasi gani za kazi walizoitiwa. Hii ilionesha dhahiri kwamba hawakuwa na taarifa kamili za kinachoendelea hapo jambo ambalo linaleta shaka juu ya njia iliyotumika kuwapata.
Baada ya zoezi la usaili, matokeo ya usaili huo hayakutolewa. Hata hivyo kwasababu wafanyakazi walikuwa wameshapewa barua zinazowajulisha kwamba baada ya tarehe 28 Februari mikataba yao haitaongezwa mpaka hapo taratibu za kiutumishi zitakapotolewa, walijua kwamba huo ndio mwisho wa ajira yao. Wengi hawakuchukua hatua yoyote kutafuta haki yao kwakuwa walikuwa wamekatishwa tamaa na utawala usioheshimu sharia na haki za binadamu chini ya utawala wa rais Magufuli. Baadae ilikuja kufahamika kwamba kuna watumishi wapya wamepelekwa katika maabara ya Taifa kuchukua nafasi za watumishi 12 wa maabara walionyimwa mikataba.
Watumishi walionyang’nywa ajira zao hawakuwahi kukutwa na makosa yoyote ya kinidhamu wala ya kiutendaji, wala hawakuwahi kupewa hata barua ya onyo. Haijulikani ni sababu gani zilizopelekea kuachishwa kwao kazi.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa miongoni mwa watumishi waliokatishiwa mikataba, wapo wataalam wenye uzoefu wa zaidi ya miaka mitano na waliopatiwa mafunzo mengi yanayoendana na kazi zao ikiwa ni pamoja na mafunzo yaliyoiwezesha maabara ya taifa kupata ithibati ya kimataifa (ISO accreditation). Mmoja wa waliokatishiwa mikataba alikuwa ni Biomedical Engineer aliyepata mafunzo ya kufanya Biosafety Cabinets Certification. Wataalam kama huyu wapo wachache sana hapa nchini. Inawezekana hawafiki hata watano. Mtaalam huyo alikuwa katika mchakato wa kuanzisha mafunzo ya namna hiyo hapa nchini kwa kupitia chuo cha MUHAS.
Wengine walioondolewa ni wataalam wa maabara wa fani tofautitofauti ikiwa ni pamoja na laboratory scientists, technologists, technicians, maafisa TEHAMA na madereva.
Mojawapo ya mapendekezo yaliyotolewa na tume iliyoundwa na rais Samia Suluhu Hassan kuishauri serikali kuhusu namna ya kushughulikia COVID-19 ilikuwa ni “serikali ikamilishe malipo ya madeni ya watoa huduma na watumishi waliokuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19”. Sambamba na pendekezo hilo, ingekuwa ni vyema na haki suala la watumishi walioporwa ajira zao liangaliwe pia na waliohusika na dhulma hii kuwajibishwa.