Mheshimiwa Raisi na Waziri Mkuu kwa moyo wa dhati napenda kuwapongeza kwa ujasiri mliokuwa nao wa kupambana na ufisadi uliokithiri katika nchi yetu ya Tanzania. Ninafahamu kwamba mko kwenye opersesheni tumbua majipu ila naomba sana mtembelee Hifadhi ya Ngorongoro maana na kwenyewe kuna majipu yanayohitaji tiba. Sababu ya mimi kuwaomba mtembelee eneo hilo ni hizi hapa;
1. UBADHIRIFU WA KUTISHA WA KAIMU MHASIBU MKUU BW. SEZARY SEMFUKWE
Mwanzoni mwa mwaka huu niliripoti ubadhirifu wa kutisha wa Mhasibu huyu wa kiasi kinachokadiriwa cha shilingi milioni 240 iliyopelekea mwandishi wa habari wa gazeti la mtanzania kumuhoji na kukiri ni kweli alizipokea pesa hizo. Haikuishia hapo kwani kwenye ripoti ya wakaguzi wa TAC ilionyesha kuna pesa zilizochotwa huku kukiwa hakuna viambatanisho sahihi na vilevile kulikuwa na milioni hamsini iliyotafunwa bila kuwa na maelezo yeyote.Niliambatanisha viamabanisho vyote na kuwaomba TAKUKURU wafuatilie jambo hilo lakini mpaka sasa hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa na Mhasibu huyu anaendelea kutafuna hela na kutamba kwamba hakuna mtu atakaye muweza. Nadhani wafuatiliaji wa suala hili toka TAKUKURU walipewa kidogo kidogo.
Jambo la kushangaza Mhifadhi wa Ngorongoro Dr. Manongi amekuwa mstari wa mbele kumlinda mhasibu huyu wakati ushahidi upo wazi. Sasa cha kujiuliza kama Dr Manongi na Bodi ya wakurugenzi waliweza kuwasimamisha kazi baadhi ya watumishi waliohusishwa na miamala ya shilingi milioni kumi( 10,000,000) kwanini huyu inashindikana? Waliunda Tume feki iliyokuwa inaongozwa na Mkaguzi wa wizara Mrs Flora Msami ili imsafishe mhasibu huyu lakini mwisho wa siku wafanyakazi wa Shirika hilo walimweleza ukweli kuhusu wizi unaofanywa na Bw. Semfukwe. Lakini cha ajabu ripoti haikuwekwa wazi ili wafanyakazi wafahamu nini kilichojiri.Tunafahamu Mrs Flora alikuja kwa ajili ya kupata pesa za kwenda kumtibu mwanao anayeumwa masikio huko India. Manongi nilikuhahikishia lazima hilo jipu litumbuliwe penda usipende maana waliokuwa wanakupa kiburi hawana mashiko tena katika nchi hii. Viambatanisho vya miamala iliyochukuliwa na Bw.Semfukwe nimeviweka.
2. MWENDELEZO WA AJIRA ZA UPENDELEO
Kama mtakumbuka kwenye moja ya makala yangu niliwaeleza Afisa utumishi wa Hifadhi hiyo Bw. Mackiros ni kihiyo na nilisema hivyo nikiwa na uhakika na ninachokisema. Na vilevile kwa kunukuu maneno ya bosi wa zamani wa Bw Mackiros pale chuo cha DUCE aliyesema hivi nanukuu ??uwezo wa Mackiros ni mdogo sana katika kuchambua mambo na kufanya uamuzi sahihi wenye hekima mwisho wa kunukuu.
Miezi 6 iliyopita Hifadhi hiyo ilitangaza ajira za mafundi wa gereji na waongoza mitambo waombaji wawe na sifa za elimu ya kidato cha nne. Kampuni ya PricewaterhouseCoopers (PWC) ilishinda tenda hiyo na ikafanya usaili na walioshinda wakaajiriwa.
Miezi mitatu baadae Shirika hilo hilo lilitangaza ajira kwa upande wa utawala na TEHAMA na manunuzi. Wenye sifa waliomba na kilichokuwa kinasubiriwa ni kufanyika kwa usaili. Ila cha kushangaza badala ya kufanyika kwa usaili Bw Mackiros pamoja na Mkaguzi wa ndani mwenye mbwembwe lakini fisadi Bw. Maleva waliondoka na kwenda vyuo vya uhasibu vya Arusha na Dar es salaam na kuchukua wanafunzi waliomaliza masomo ya uhasibu, manunuzi na TEHAMA kisha wakawafanyia usaili na kuleta majina yao kwenye uongozi wa shirika na kuyabariki then wakaajiriwa. Sasa swali la kujiuliza kama mlitangaza ajira kwanini hamkufanya usaili badala yake mkaenda kuchukua wanafunzi ambao ndo wamemaliza hata vyeti hawajapata na mbaya zaidi sio wale wanachuo waliokuwa waliofanya vyema katika masomo yao kuliko wengine. Ushahidi huu umepatikana kwa wahusika wenyewe na kuuliza kwenye vyuo husika. Hapa tunarudi kule kule kwenye lile suala la ajira za kujuana.
Watuambie ni vigezo gani walivyotumia kwenda kwenye vyuo hivyo viwili wakati nchi hii ina vyuo vingi vyenye sifa zinazojitosheleza? Je hamuoni mliwanyima fursa wanachuo wengine waliosoma kwenye vyuo vingine bora nchi hii kama UDSM, Mzumbe, IFM n.k? Kama mliweza kutangaza ajira za fundi wa gereji aliyemaliza kidato cha nne kwanini mlishindwa kutangaza kazi ??sensitive?? na za professional kama hizo?
Hapa ndipo ninapoona umuhimu wa kupasuliwa majipu maana baadhi ya wakubwa wa Shirika hili wameshaona taasisi hiyo ni kama mali ya mama zao.
3. PENDEKEZO LA MUUNDO MPYA WA SHIRIKA NA ?SCHEME OF SERVICE?
Taasisi hii ipo kwenye mchakato wa kuunda muundo mpya wa Shirika na kuachana na ule wa zamani lakini ukikaa chini ukapitia miundo yote miwili utagundua kabisa muundo wa zamani ulikuwa bora na ulifanywa na watu makini wenye nia njema na Shirika kwa kipindi chake kuliko huu mpya. Na sababu kubwa ni kwamba muundo mpya umeongozwa zaidi na tamaa za wadau wa uundaji. Kama miaka ishirini iliyopita wakati wasomi sio wengi nchi hii ilionekana Mkuu wa Idara awe na shahada ya uzamili( ?MASTERS DEGREE?) lakini leo hii nchi ina wasomi wa kutosha unasema haifai awe na stahada( ?Bachelor Degree?) Kwa watu wenye kufikiria mbali tunaona kabisa kuna watu wanatengenezewa mazingira ya kuzishika nyadhifa hizo. Taarifa nilizo nazo mchakato huu ulifanyiwa kazi na wajumbe wachache wa menejimenti na hao ndio waliouharibu kabisa. Mfano mdogo ni Idara ya mambo ya kale ambayo kwa sasa anayekaimu ni Injinia Joshua mwankunda ili kuhakikisha hakosi nafasi hiyo ameweka kigezo kimojawapo cha mtu kuwa Mkuu wa idara ya mambo ya kale ni awe Injinia, Hivi jamani kama mainjinia wataacha kufanya kazi zao na wakaingilia kazi za mambo ya kale wenye professional hizo wakafanye nini?
Kuonyesha namna gani Bodi ya Ngorongoro ilivyo na watu upeo mdogo na wao bila kufikiria na wakabariki muundo huo na sasa inasubiri Wizara ya maliasili pamoja na hazina wapitishe. Ombi langu kwenu Wizara na hazina msipitishe huo uchafu maana mkicheza fagio la Magufuli lazima liwapitie. Na mbaya zaidi wafanyakazi hawajashirikishwa wakati muundo huo wakati ni kwa ajili yao sasa tujiulize mbona muundo wa awali wafanyakazi wote walishirikishwa? Ni kitu gani mnachokificha? Acheni upuuzi hilo Shirika ni la umma na kila mtanzania anahitaji kulifaidi.
4. BW. MWEYUNGE (KAIMU MWANASHERIA) KUSHIKILIA NAFASI MBILI KATIKA TAASISI MBILI TOFAUTI.
Katibu Mkuu wa Wizara ya maliasili na utalii alifanya uhamisho wa watumishi wawili wa TANAPA pamoja na mmoja wa Ngorongoro kwenda TAWA (Tanzania Wildlife Authority) Morogoro. Lakini cha kushangaza watumishi wa TANAPA wamesharipoti na kuanza kazi ila wa Ngorongoro Bw.Mweyunge anaendelea kushikilia sehemu zote mbili na kulipwa posho kinyume na utaratibu. Hivi yeye ni nani? Ina maana huko Ngorongoro hakuna watu wa kuzifanya kazi zake kwa ufanisi? Au anaogopa akiondoka lile eneo aliloligawa kwa LEOPARD TOURS ambalo lipo kinyume na utaratibu litawekwa wazi? Je ina maana yeye ni mtu muhimu kwa NCAA kuliko Loibook aliyekuwa TANAPA? Hiyo jeuri anaipata wapi ya kutunushiana misuli na Katibu Mkuu wa Wizara?
Wengi wenu mlisema nimepotea ila ninawahakikishia nimerudi tena kwa nguvu mpya ya kupasua majipu na ninawasihi mjipange maana ni lazima muisome namba.
Mwisho kabisa napenda kuwatakia kila la kheri Mheshimiwa Rais, Makamu wa Raisi, Waziri Mkuu pamoja na Watanzania wote wenye kupenda mabadiliko Mungu awabariki sana.