Jeshi la Polisi mkoani Mara linawashikilia askari watano wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokuwa wamemaliza muda wao wa kujitolea, wakisubiri ajira za muda wa Kikosi cha Jeshi la Wananchi 27 KJ MAKOKO kwa tuhuma za mauaji ya mkazi wa Rwamlimi manispaa ya Musoma, Paulo Joseph, maarufu kama ‘Baga’ kwa madai ya kumshambulia kwa kipigo askari mwenzao.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi Longinus Tibashibwamu amethibitisha kushikiliwa kwa askari hao wa JKT, ambao pia wanadaiwa kuwakamata na kuwapiga raia wengine 5, akiwemo dereva wa gari ya abiria inayofanya safari zake kati ya Bweri na Mjini kati yenye namba za usajili T 108 CXK Michael Mrema.
Mkuu wa Kikosi cha Jeshi la Wananchi 27 KJ MAKOKO Kanali Mushashi amekutana na familia ya marehemu Paulo Joseph kwa ajili ya kutoa zpole juu ya kifo hicho huku akiahidi kushirikiana na wafiwa katika shughuli zote za msiba huo kwani waliohusika na mauaji ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 35, wapo chini yake.