Maumivu Yasiyo kwisha (Endless Pain)

Maumivu Yasiyo kwisha (Endless Pain)

MAUMIVU YASIYO KWISHA(ENDLESS PAIN)...!!

Sehemu ya Kumi na Tano...
.
#Ilipoishia: Baada ya purukushani za hapa na pale kati yangu na Magdalena ndipo mumewe alipotukuta na mawazo yake yakamfanya ahisi kuwa tulikua katika dimbwi zito la mapenzi kuendana na jinsi alivyotukuta.
.
Alifoka kwa nguvu kwa kingereza akimaanisha "Unafanya mapenzi na mgeni??? Tena hadharani???" - (Aliuliza kwa hasira sana huku akitutazama).
.
Nilistuka sana nikijua tayari msala mwingine umeshanikuta, kutazama pembeni ndipo nilipowaona Careen na Abdulrahman wakiwa nao wametoka chumbani kwa Peter baada ya kusikia kelele.
Nyuma yangu nako ilisikika sauti nzito iliyojawa hasira, "What?? "
.
Kutazama nyuma sauti inakotoka, ilikua ni baba yake Peter akija na mama yake Peter.
Hapo ndipo nilipotamani dunia ipasuke nidumbukie labda ningeweza kuuepuka msala huu.
Nilizidi kujilaumu kwa maamuzi yangu mabovu kila wakati, nilizidi kuziona athari za kuendeshwa kihisia, sababu nimekua mtumwa kwa Careen na sasa matatizo yote haya yananikumba kwasababu yake.
Nashindwa kuwa na maamuzi binafsi na matumizi mazuri ya ubongo, yote kwasababu yake.

#Inaendelea:
Mumewe Magdalena alipandwa na hasira sana, hakutaka kunilazia damu, akanirukia na kunitwanga ngumi ya shavu.
Akaniongeza makonde lakini ilibidi niweke gadi ya mikono ili yasinipate usoni.
Wakati huo huo Abdulrahman na Magdalena walimuwahi na kujaribu kumzuia.
Tukawa ndani ya vuta nikuvute, Careen nae akaja kuongeza nguvu.
.
Baba Peter alikua na hasira, wala hakuja kutoa msaada, alikuja haraka na kuanza kunipiga mateke huku akifoka kwa kingereza, alimaanisha
"Umekuja kuharibu amani ya nyumba yangu".
.
Ikabidi mama Peter na Magdalena wapambane kumzuia baba Peter, na Careen na Abdulrahman wapambane kumnyofoa mumewe Magdalena.
.
Baada ya purukushani wote walifanikiwa kushikwa vizuri, Careen akamuachia mumewe Magdalena na kuja upande wangu.
.
Nilitamani upenyo nilioupata niutumie kukimbia, lakini nikahisi kuwa nikikimbia watahisi kuwa ni kweli.
Nikabaki naomba Mungu tu.
.
Mabishano yakawa yanaendelea kwa lugha ya kingereza yakiwa na maana ifuatayo:
Magdalena akaongea kwa nguvu akijaribu kumuelewesha mumewe "Unachohisi sicho, wala sikuwa nafanya nae ulichokuwa ukidhani".
.
Mumewe kwa hasira akajibu "Nachohisi sicho?!! Mikono yake ilikua inakushika nini??! Na wewe ulimshika nini? Na mlikua mnakombatiana kombatiana, unadhani mimi ni mjinga?? " - (Alizungumza kwa hasira kama mtu aliyetamani kumrukia mkewe).
.
"Haukuelewa kilicho kuwa kinaendelea, nilikua nimembana anieleze ukweli kuhusu Peter, hakutaka kuniambia, ndomana tukawa tunakunjana, hukuona shati yake nimekata vifungo??" - Alizungumza Magdalena kwa ukali huku kama anataka kulia.
.
Baba yake Peter akadakia "Hivyo vifungo vimekatika sasa hivi hapa" - (Akazungumza kwa kukanusha kauli ya Magdalena).
.
Sikutaka kuchelewa nami nikatetea "Vilikatwa na Magdalena "
Ghafla nikazimwa "Nyamaza mwana haramu mkubwa" - (Alikua ni mama yake Peter aliyetoa sauti ya ukali).
.
"Ni kweli mama, vilikatwa tangu mwanzo" - (Abdulrahman nae akatetea upande wa Magdalena).
.
"Havikukatwa kwa ugomvi, wamevikata kwenye mahaba, nimeshuhudia kwa macho yangu mawili" - (Alizungumza mumewe Magdalena).
.
Akataka kuruka ili amfate mkewe amshindilie japo makofi ya uso, lakini Abdulrahman alisimama vizuri kumzuia.
.
"Kama ni kweli mlikua mnagombana. Ulikua unamuuliza kuhusu Peter ili iweje? " - (Aliuliza Mama Peter).
.
Magdalena akamtazama mama yake, na kuamua kutoboa siri kuwa Peter alizimia baada ya kupokea message na picha kutoka kwa Chris.
.
''Kuna uwezekano Chris anajua kila kitu kuhusu Peter, na kuna siri kubwa kati ya Chris na Peter.
Na nilimbana ili anieleze, lakini hakuniambia chochote ndiomaana tukabaki tukigombana" - (Alimaliza kama hivyo Magdalena, kisha kuchukua simu ya Peter, na kufungua message niliyomtumia Peter na kumuonyesha mama yake, na mama yake akamuonyesha baba yake.
.
Kipindi hicho chote nilikua nimebaki kama msukule, sikujua nini cha kufanya, kila sekunde zilivyozidi kwenda nilizidi kutamani hata ningekua na mabawa nipeperuke, au hata ningekua mchawi niyeyuke.
Lakini haikuwezekana, kutazama mlango wa kutokea ulipo, ulikua umerudishiwa, nikapiga hesabu za haraka haraka kutoka niliposimama mpaka mlango wa kutokea, na kutoka mlangoni mpaka geti la fensi, nikaona hii ndio chance ya kutokea.
.
Nikapata akili ya haraka kuwa nikimbie, sababu hata nikibaki bado nitapata shida ya kuingizwa kwenye kesi ya kumsababishia Peter matatizo.
Nikahesabu kimoyo moyo, 1, 2, 3, lakini nikasita baada ya kukumbuka kuwa nisingeweza kupita getini wala nisingeweza kuruka ukuta kwajinsi ulivyo mrefu.
Nikabaki nimesimama pale pale huku nikisubiri kama mfungwa anaye ngojea msamaha wa Rais.
.
Wakahoji mengi sana kuhusu message zangu kwenye simu ya Peter, lakini niligoma kueleza chochote na kusema kuwa "Peter ni rafiki yangu, na Careen ni rafiki yangu, ndio maana nilimtumia Peter picha ya birthday ya Careen na ndio maana nikamwambia "I wish ungekuepo" sababu hakuwepo."
.
Careen alistuka baada ya kusikia nimemtumia picha Peter.
Lakini Magdalena akawa tayari ameshapata jambo.
.
Akasema "Kama nyinyi ni marafiki, kwanini wewe uliandaa party kwaajili ya Careen, na Peter aliandaa kwaajili ya Careen???!!! Kwanini hamkuandaa wote kwa pamoja.
Na iweje Peter azimie baada ya kuona picha uliyo mtumia.??"
.
Nilishindwa kujibu lolote, nilihisi kuna kitu Magdalena anajaribu kuchimba.
.
Hapo ndipo Careen alipo gundua kuwa kumbe Peter alimuambia aende Kiota kwaajili ya kumfanyia surprise.
.
Baba yake Peter akamtazama Abdulrahman na kumuuliza swali, "Chris na Peter ni marafiki??? "
.
Abdulrahman akajibu "Ndio".
.
Mama yake Peter akasema "Nadhani majibu ya maswali yetu kichwani, yako kinywani mwa Peter
Na hatuwezi kumuuliza chochote Peter kwasasa mpaka presha yake itakapo kaa sawa".
.
Sote tukatazamana, nikaanza kupata mwanga mwa matumaini, nikajua wazi kuwa sasa naweza kutoka salama.
.
Baba yake akanitazama na kunikazia macho, akasema "Uko huru leo, ila tambua lolote tutakalojibiwa na Peter, ndilo litakalofanya uwe huru zaidi au laanh".
.
Nilinywea sana ila nikaona afadhali, nilishukuru Mungu sana.
Abdulrahman akaniambia tuondoke, Careen akawa tayari na tukaanza kuondoka.
Ghafla mumewe Magdalena akaniita, nilipomgeukia akanisogerea na kuniambia "Usidhani umeponyeka, ukweli ukijulikana ndio nitajua cha kukufanya. Hizi sababu bado hazijanifanya niamini kuwa hauna mahusiano na mke wangu".
.
Nilibaki nikimuangalia tu, Abdulrahman akamfokea "Michael inatosha".
.
Nikageuka na kuanza kupiga hatua kuelekea kwenye gari la Abdulrahman.
Tulipanda na kuondoka, njia nzima tulikua mabubu na wala hakuna aliyemsemesha mwenzie.
Tulimshusha Careen Tabata, nami nikaletwa mpaka Hostel.
.
Pindi nataka kushuka kwenye gari, Abdulrahman akaniambia "Subiri Chris".
.
Akazungumza huku akichukua simu yake na kufungua Gallery, na kunionyesha picha ya msichana na kiNigeria.
.
Niliitazama ile picha na kumuona msichana mzuri tu.
Nikamtazama Abdulrahman, kiukweli sikuwa kwenye mood ya kuzungumza chochote.
Abdulrahman akaniambia ''Chris usijutie ulichotenda jana na rafiki zako, na hata kilichotendeka leo nyumbani kwa kina Peter".
.
Nikamtazama usoni kwa makini, nilihisi labda anataka kunipa moyo tu kwa maneno matamu, lakini nilitamani kumuuliza swali kuhusu picha ya msichana wa kiNigeria niliyeonyeshwa.
.
Akaniambia "Japo umepitia magumu, ila naona dalili zako za ushindi zinakaribia.
Sababu wazazi wa Peter wakishajua kuhusu jambo linalo endelea kati ya Peter na Careen. Basi jua kuwa mchezo umeshaushinda.".
.
.
Maneno yake yaliniachia maswali kichwani, nikawa bado natafakari, akaniambia "Na usidhani Magdalena anakuchukia, wala hakuchukii, Anataka kuujua ukweli kama Careen na Peter wana mahusiano au vipi.
Na hata alivyo alikwa kwenye party, alikuwa akihoji maswali mengi kuhusu Careen na Peter, na kuna sababu kwanini anahoji''.
.
Nilianza kupata shauku ya kutaka kujua kwanini Abdulrahman anayasema yote hayo, ikabidi nimwambie "Sijakuelewa bado, hebu nieleze vizuri"
.
Akaniambia "Peter anampenda Careen, lakini....wazazi wake Peter wa...wa...." - (Akakwamia hapo).
.
Nikapata shauku ya kutaka kujua wazazi wake Peter "Wa" wamefanyaje.?!
Nikarudia alikomwamia "Wa..???"
.
Akanipa jibu ambalo lilinifanya nisiamini masikio yangu, nilipata furaha ya ghafla, na kutamani hata niruke ruke ndani ya gari
.

Je Chris amepewa jibu gani!??! Na hiyo picha ni ya nani!?? Na Magdalena ana sababu zipi za udadisi wake???

Usikose sehemu ya 16
#Itaendelea


Maumivu Yasiyo kwisha (Endless Pain)
 
MAUMIVU YASIYO KWISHA(ENDLESS PAIN)...!!

Sehemu ya Kumi na sita...

#Ilipoishia:
Abdulrahman alinipa picha ya msichana wa kiNigeria, na kunipa maneno kadhaa yenye kunitia moyo, lakini sikumuelewa hata kidogo nini alichokuwa akimaanisha.
.
Ndipo Abdulrahman akanitobolea siri kuwa Peter anampenda Careen, lakini wazazi wake wameshamchagulia mchumba kutoka katika familia ya kitajiri, nchini Nigeria.
Na kivyovyote vile, Peter hana uwezo wa kupingana na chaguo la wazazi wake.
*************
#Inaendelea:
Nilipatwa na furaha ya ghafla, moyoni nikaingiwa na amani nikijua kuwa kumbe shida zote nilizopitia zilikuwa na matunda mbele yake.

Lakini nikakumbuka jambo na kumuuliza Abdulrahman, "Kwani Peter hajui kama ameandaliwa mchumba??? Na wewe rafiki yake kwanini hukumwambia?? Na kwanini Magdalena anachunguza sana??? ".

Nilimtupia maswali mfululizo huku nikiwa nimemtupia jicho kavu, huku nikisubiri nipewe majibu yenye mashiko.

Abdulrahman akatafakari kwa sekunde kadhaa na kuniambia "Mchumba ametafutiwa hivi karibuni kipindi tayari ameshampenda Careen, na bado wameliweka siri.
Na siwezi kumwambia hii siri."

Akanyamaza kimya kidogo na kulamba lips, akafungua kinywa tena na kusema "Kuhusu Magdalena, anajaribu kuchunguza kama Careen na Peter wana mahusiano ili ayavunje, sababu nae anataka kaka yake amuoe binti wa kitajiri, chaguo la wazazi wake.''

Maneno yaliniingia vilivyo na kuanza kupata picha kwanini Magdalena alikua akinikazia nimweleze ukweli.
"Shit, ningejua ningetoboa siri pale pale. Shenzi "- Nilijisemea kimoyo moyo.
.
Nilianza kupata amani na kuendelea kuamini kuwa kweli kila jambo ndani ya maisha yetu, hufanyika kwa kusudi maalumu.
Nikaagana na Abdulrahman, na kwenda kupumzika hostel.

Kesho yake marafiki zangu walikuja kuniona na kunipa pole kwa yote yaliyotokea, Ivan alijisikia vibaya sana na kujilaumu mbele zangu kuwa yote hayo amesababisha yeye sababu ya wazo baya alilotoa afanyiwe Peter.
Nikamwambia usihofu, mimi ndiye mwenye makosa sababu nilikua na uwezo wa kukataa kutuma picha, na hata kukataa kwenda na Careen.

Ramadhan akaleta utani "Duh sema umechezea vitasa mpaka uso umeiva" - (Alizungumza kauli iliyojaa rejesta za mtaani, akimaanisha "umepigwa ngumi mpaka umekua mwekundu").

Wote wakacheka, Hasheem akaongeza "Ningekua mimi asingeweza kunipiga kizembe kama hivyo ".

"Mmmh mxieeew" - (Nikaguna na kusonya)

"We mbwembwe tu, ungefanyaje unadhani? "- (Ramadhan akauliza)
.
"Haaa, wehu nyie, nikubali kupigika kirahisi!??! ningetoka nduki kama Lamborghini hahahah "- (Hasheem akajibu huku akicheka)

Sote kwa pamoja tuliangua kicheko, na hili ni jambo kubwa ambalo najivunia kuhusu marafiki.
Haijalishi mna huzuni kiasi gani, bado utapata nafasi ya kucheka.
Tangu hapo nikaamini ile kauli ya wanasaikolojia kuwa kuwa na watu wanaoweza kukufurahisha, ni dawa mojawapo ya kuondoa upweke na huzuni.

Tulipika chakula cha mchana, tukala pamoja na mwisho wakaaga na kila mmoja kuondoka.
Nikarudi chumbani na kujaribu kuutafuta usingizi japo ilikua jioni, majira ya saa 10.

Pindi bado nautafuta usingizi kitandani, ndipo niliposikia mlango unagongwa.
Nikaamka na kwenda kufungua, kutazama alikua ni mwanafunzi mwenzangu anaekaa chumba kinachofata.
.
"Chris una mgeni nje " - Alizungumza Erick huku akigeuza na kuondoka.

Ikabidi nirudi ndani na kuvaa shati, kisha kutoka nje kutazama ni nani huyo.
Nikatoka nje na macho yangu yakakutana na Nasra aliyekuwa amesimama akinisubiri.
Ni mara yake ya kwanza kufika mahali napoishi tangu nijuane nae.

Nikamkaribisha ndani, na kumletea kinywaji.
Akanieleza jinsi alivyoelekezwa na Hasheem mpaka kufika.
Naye alikuja kunipa pole, pamoja na kuniletea dawa za maumivu za kujichua, pamoja na matunda.

Tukapiga story mbili tatu kama nusu saa, ghafla nikasikia mlango wangu unagongwa.
"Chris "- ilikua ni sauti ya Careen akiita.

Nikastuka, nikamtupia jicho Nasra na kumuona nae kakunja sura ghafla.
Nikajibu "Pita mlango uko wazi huo".

Careen akafungua mlango na kuingia, lakini alisimama ghafla, na kubaki ameduwaa kumkuta Nasra ndani.

Nilipata wasiwasi nikidhani labda Careen amestuka kumuona Nasra yuko ndani, lakini nilimuona akirudi hatua mbili nyuma na kuchungulia nje.
Nikapata wazo jipya kuwa huenda amekuja na mtu.

"Unamchungulia nani?! " - Nikamuuliza Careen.
"Anh ni Abdulrahman, nilimwacha anaongea na simu nje".

Akaingia ndani na kutusalimia, dakika mbele zilizofata, Abdulrahman akabisha hodi na kuingia ndani.
Nae alishangaa kumkuta Nasra ndani.

Nikawaletea vinywaji, na story ziliendelea.
Jambo lililomkera Nasra zaidi ni baada ya kuona Careen ananikabidhi dawa za maumivu tofauti na zake.

Akaropoka "Sidhani kama zinaweza kuwa nzuri kuzidi nilizoleta".
.
Wote tukamgeukia, Careen akajibu "Labda, sijajua".

Nikagundua kuwa Careen hakutaka kuleta mabishano, akamzima kijanja ili asiendelee na mada yake.
Story zingine zikaendelea na baada ya muda wote waliaga na kuondoka.

Wiki moja baadae, ikiwa ni siku ya Jumapili, nilipokea message kutoka kwa Abdulrahman aliniambia "Good News, Peter amehojiwa na familia, na ameeleza kuwa anampenda Careen".

Nikamjibu "Imekuwaje?? "
Akanijibu "Wazazi wamemkanya na kumuonyesha picha ya chaguo lao".

Niliruka na kufurahia sana nikijua tayari nimeshapunguza vizuizi vinavyo nikwamisha.
Abdulrahman akatuma message nyingine akisema "Careen amepigiwa simu na wamemuonya avunje mazoea na Peter kabisa".

Dakika mbili hizo hizo, simu yangu ikaita na nilipotazama kwenye screen nilikutana na namba ngeni.
Nilipopokea nikasikia sauti ya Magdalena.
Tukasalimiana na mwisho akaomba msamaha kwa kunishuku vibaya, pamoja na kuniletea kash kash nyumbani kwao.

Ghafla sauti ya Magdalena ikakata, na sauti ya kiume ikasikika ikikoroma kwa lugha ya kingereza, ikimaanisha "Na leo nimekukamata tena unazungumza na mke wangu".

Nilistuka baada ya kugundua ni Michael(mume wake Magdalena) ndiye aliyekuwa akinikoromea.
Nikabaki kimya, mapigo ya moyo yakizidi kunienda mbio.

Pindi nataka nikate simu tu, ndipo niliposikia anacheka na mkewe kwa nguvu, akasema "Chris muoga sana".
Ndipo nilipogundua kuwa nilikua nataniwa.
Nikajichekesha kinafki japo alinikera.

Michael aliniomba radhi kwa vurugu alizonifanyia, na aibu aliyoniletea siku niliyokuwa kwao.
Nikajisemea kimoyo moyo "Yani wewe ungekua karibu leo, ningekurudishia ngumi za uso".

Lakini nilishukuru Mungu baada ya ukweli kugundulika, nami kuwa huru.
Mazungumzo yakaisha, tukaagana na kukata simu.

Hazikupita hata dakika mbili, simu yangu ikaita tena, kutazama kwenye screen ilikua ni "PETER".
Sikutaka kuchelewa, nikaipokea, na kuisikia sauti ya mtu iliyojaa huzuni.

"Hey, asante kwa kuharibu furaha yangu.
Asante kwa kukatisha ndoto zangu.
Ila jambo moja tu, usidhani umeshinda.
Mechi bado inaendelea." - Peter akanyamazia hapo.

"Haaanh"- Nikaguna kwa dharau, kisha kucheka kwa nguvu sana.
Nikamjibu kwa dharau "Nilidhani umenipigia simu ili uniambie ni wapi, saa ngapi, tukutane ili nikuletee wigi na dera la kuvaa.".

Sikutaka kumkawiza, nikamuongeza "Bro, umeshashindwa mechi, usiniletee mikwara.
Subiri kesho nakuja na make up ili upendeze".
.
Nilipomaliza kusema kauli hizo, na simu nikakata hapo hapo.
Akapiga tena, nikakata.

Baada ya sekunde kadhaa, akanitumia message "Usilete dharau wakati bado hujampata, mechi bado inaendelea mpaka ajulikane mshindi nani".

Baada ya kuisoma ile message, kumbukumbu zikanijia kichwani kuwa kumbe hata mimi bado sijafanya lolote.

Pindi bado natafakari, nikaongezwa message nyingine "Nitahakikisha hakuna atakaye shinda mchezo huu, subiri na uone kitakachojiri".

Nilirudia kuisoma message mara mbili mbili, nikiwaza kile ambacho Peter anawaza kunifanyia.
Nikajisemea "Nilidhani mchezo umeisha, kumbe ndo kwanza unaanza
".

Usikose sehemu ya 17
#Itaendelea


Sehemu ya Kumi na saba soma hapa Maumivu Yasiyo kwisha (Endless Pain)
 
MAUMIVU YASIYO KWISHA(ENDLESS PAIN)...!!

Sehemu ya Kumi na saba
.
#Ilipoishia:
Nilimtamkia Peter kauli zilizojaa dharau na kumkatia simu.
Haikuchukua dakika, alinitumia message za kunitisha kuwa nisidhani mchezo umeisha, bado mechi kati yetu inaendelea na atafanya kila analoweza kuhakikisha kuwa simpati Careen.

#Inaendelea:
Nilibaki na mawazo juu ya Peter, anawaza kunifanyia nini.
Niliitazama safari yangu ya kumpata Careen kama safari iliyojaa shida, na misukosuko isiyo isha.
Nikajisemea kimoyomoyo "Siku nikimpata, lazima nifanye sherehe dadeck ".
Siku iliyofata, niliwahi chuo mapema na kukaa na Careen ndani ya darasa.
Alionekana mwenye huzuni sana na nilijua tu kauli za wazazi wake Peter zitakua zimemsononesha.
.
Nikamwambia "Magdalena alinipigia jana, wameniomba radhi".
.
Akanitazama kwa unyonge, na kuniambia "I wish nami ningepigiwa simu na kuambiwa maneno mazuri kama wewe.
Wamenisononesha sana, wamenitamkia kauli za ajabu sana.
Na mwisho wamenipa vitisho kuwa nivunje urafiki na mtoto wao".
.
Nilimtazama Careen kwa huruma sana.
Akaendelea "Potelea mbali, siwezi lazimisha urafiki.
Nilikua na rafiki kabla yake, na ninaye mpaka sasa.
Nafurahia bado upo nami Chris". - (Alizungumza kwa hisia sana huku akiwa amejawa na huzuni kubwa mno.).
.
Nikampa pole pamoja na kumpa moyo kuwa ndivyo binadamu walivyo, avumilie tu.
.
Kutupa jicho kwa mbele nilimuona Peter anachungulia ndani ya darasa kama anatafuta mtu hivi.
Akatazama huku na huko, mwisho akatuona na kutufata.
Akasalimia, na kuomba azungumze pembeni na Careen.
.
Careen akanyanyuka na kutoka nae nje ya darasa.
Nami nikaona nisipitwe na linalo endelea, nikanyanyuka na kunyata taratibu karibia na mlangoni.
.
Peter alikua akiomba msamaha juu ya kauli walizo zungumza ndugu zake, na kumuomba azipuuzie tu na urafiki wao uendelee.
.
Careen alimjibu " Hapana siwezi.
Nilikuheshimu kama kaka yangu, ila kwasasa sitaki ukaka wala urafiki na wewe.
Ndugu zako wamenitupia lawama kibao, na naomba nisiendelee kuongea na wewe, nilishaambiwa nikae na wewe mbali ". - (Careen akatoa kauli iliyojaa huzuni iliyochanganyika na hasira, akageuka na kutaka kuondoka)…
.
Peter akamuwahi na kumshika mkono, na kumuambia "Nisamehe mimi, nisamehe sana.
Halikua kosa lako japo wamekushutumu.
Ni kosa langu, kosa la moyo wangu kukupenda.
Ni kosa langu nilitaka kukusogeza karibu, ili uje kuwa wangu peke yangu, wa maisha yangu.
Najiona mjinga kukukosa, nailaumu familia yangu kwa kunikatiza ndoto yangu ". - (Alizungumza huku akilengwa na machozi).
.
Careen akamtazama usoni na kumjibu "Peter tusipotezeane muda.
Isije na ndugu zako wakanikuta hapa nimesimama na wewe mwisho ikawa nongwa.
Na nikukumbushe tu kuwa sijawahi, siwezi, na wala sitowahi kutamani kuwa nawe kimapenzi.
Ulikua kama kaka yangu, ila kwasasa hata ukaka hauna tena. Nitakuheshimu kama watu wengine ambao sijawahi kufahamiana nao.
Naheshimu mawazo ya wazazi wako, na natii onyo lao kwangu."
.
Akazungumza na kumwacha Peter amesimama.
Niliposikia anakuja ilibidi nibadilishe pozi na kujifanya kama nilikua najipiga selfie.
.
Careen akarudi darasani na kuchukua bag lake na kuelekea garden.
Peter alibaki amesimama pale pale nje.
Na mimi nikabeba bag langu na kutoka darasani pia huku nikiimba kiuchokozi.
"Kuachwa kuachwa aanh, kuachwa ni shughuli pevu.
Mbaya zaidi kwa unaye mpenda, wewe umesimama, yeye ameondokaaa hahahah "
.
Kisha nikacheka sana.
Peter akanitazama kwa hasira, nikaona huu msala, nikaongeza mwendo zaidi kuelekea garden pia.
.
Hatua kadhaa kabla sijafika kwenye benchi aliloenda kukaa Careen, simu yangu iliita.
Kutazama kwenye screen, ilikua ni simu kutoka kwa Abdulrahman.
.
Nikaipokea na kusalimiana nae, alionekana mwenye sauti iliyojaa huzuni na wasiwasi mwingi.
.
Akaniambia "Chris mambo yameharibika."
Nikamuuliza "Kivipi bro? "
.
Akanipa jibu ambalo liliniacha mdomo wazi, alijibu "Peter ameshagundua yanayo endelea kati yangu na wewe Chris. Na walikua wanafanya uchunguzi kisiri siri yeye na Nasra".
.
Nilistuka sana, nikajiuliza mengi sana kichwani, lakini Abdulrahman akanipa majibu.
.
Akasema "Peter alinifata nyumbani kwetu, jana majira ya saa 4 usiku.
Alinikuta chumbani kwangu nikiwa nimepumzika.
Kwajinsi alivyokuja tu nilijua tu hayuko sawa na kuna kitu anataka kuniambia".
.
Abdulrahman alinieleza mengi sana kwenye simu ambayo yalinichanganya sana.
Na alinieleza yafuatayo:
*********
Peter: Ulienda kwa Chris week iliyopita??.
.
Abdulrahman alishindwa kukataa kwavile alikutana na Nasra mahali napoishi.
Akajibu " Yeah, Careen aliniomba nimsindikize akamuone Chris."
.
Peter akamtazama Abdulrahman kama anamtafakari, kisha kumuuliza tena "Vizuri. Na kwanini ulikua unamtetea Chris siku ya ugomvi nyumbani!??? "
.
Abdulrahman akaanza kuhisi Peter ameanza kumhisi kitu, akaanza kupata wasiwasi.
Akamjibu "Sikumtetea Chris, nilitetea nilichokiona ".
.
Peter akaguna "Mh" na kuanza kupiga hatua kumsogerea karibu zaidi Abdulrahman, akamuuliza "Abdulrahman, unadhani ni nani huyo ambaye amemwambia Chris kila jambo lililotokea nyumbani???"
.
Alimtupia swali huku anamtazama kwa umakini zaidi, na kumshika bega.
.
Abdulrahman akageuza shingo na kumtazama Peter, lakini alishindwa kutoa majibu.
.
Peter akaongeza swali lingine "Amejuaje kama nimeshashindwa?".
.
Abdulrahman akafikiria kwa dakika kadhaa na kumjibu "Na wasiwasi itakua ni Magdalena ".
.
Peter akajibu "Nilimsikia kipindi Magdalena anazungumza na Chris, hakugusia chochote zaidi ya kuomba msamaha tu".
.
Abdulrahman akazidi kupata wasiwasi, alianza kuona kuwa mambo yanaharibika.
Akamjibu "Peter inaonekana huniamini, inaonekana unahisi labda nimekua mnafki kwako.
Kama kuhusu Chris kujua mambo yaliyojiri, huenda hata Careen amemwelezea.
Au unataka kusema na Careen nae hawasiliani na Chris??
Kama huniamini sema bwana". - (Abdulrahman akazungumza kwa ukali sana, ili kujaribu kujiaminisha mbele ya Peter.).
.
Peter alimtazama kwa mshangao mkubwa, na kumjibu kwa hasira "Abdulrahman, niliacha kukuamini tangu siku uliyompeleka Chris Posta, kwa dokta Leonard.
Na bado ukamficha ndani ya gari huku ukinidanganya umekuja peke yako" - (Peter alijibu kwa hasira na ukali sana).
.
Abdulrahman akastuka baada ya kusikia maneno hayo.
Peter akaendelea kuzungumza kwa ukali "Sikuwa na kufatilia, na wala sikuja kukufuma ukiwa na Chris.
Nilikuja kwa mambo yangu, Thank God nikasema nipumzike ndani ya gari kwanza mpaka muda wa appointment utakapofika.
Ndipo nilipowaona wewe na Chris mnatoka kwa Dr Leonard."
.
Peter akakwamia hapo, akawa tayari ameshapandisha hasira.
Abdulrahman alinywea, akawa mdogo kama Piriton.
.
Peter hakutaka kuendelea tena kubishana na Abdulrahman, akaamua kutoa kauli za mwisho zenye kuuvunja urafiki wao wa miaka mingi.
Kwa sauti ndogo na ya upole, akazungumza "Sikutaka kuamini, nikakupa nafasi nyingine, lakini nilimuomba Nasra akufatilie kwa ukaribu zaidi.
Na ukweli wa yote nimeshaujua."
.
Abdulrahman akashusha uso wake chini kwa aibu, lakini Peter alizungumza kauli zilizomstua Abdulrahman zaidi.
Peter alisema "Wewe ndiye uliyepanga kuharibu party yangu, na ukampa Chris pesa ya maandalizi ya party.
Wewe ndiye unayetoa siri na mipango yangu yote.
Wewe ndiye mnafki namba moja kwangu.
Usijiulize nimejuaje hayo yote, dunia haina siri hasa ukiwa unatumia akili na pesa.
Kuanzia leo naomba tusijuane".
.
Peter alimaliza kuongea na kuondoka.
Abdulrahman akabaki na maswali mengi sana kichwani kuwa ni nani ndani ya kundi letu, anatoa siri kwa Nasra au Peter.
********
.
Abdulrahman alinieleza yote yaliyomtokea, na kuniomba tufanye uchunguzi.
Tukaagana na kukata simu, lakini nami nilibaki na swali kichwani kuwa kati ya Hasheem, Ivan, na Ramadhan, ni nani anayetoa siri kwa Nasra na Peter?! .
.
Nikarudisha kumbukumbu nyuma, na kukumbuka siku ambayo Nasra alikuja mahala napoishi kwa mara ya kwanza, alisema Hasheem ndiye aliye muelekeza.
Nikajiuliza "Walianzia wapi story zao mpaka kufikia kuelekezana?".
.
Lakini pindi bado nimesimama natafakari, kwa mbali nikamuona Ivan akiwa anatoka na Nasra darasani.
Nikajiuliza "Au ni Ivan, kwa vile ana mazoea na Nasra?"
.
Pindi bado nipo ndani ya dimbwi la mawazo, nikastushwa na sauti ya Careen akiniita.
Nikasogea mpaka kwenye benchi alipokaa, na kumsikiliza.
.
Kwa upole, na sauti iliyojaa huzuni, akaniambia "Chris, unajua tangu jana nigundue kuwa Peter alikua ananipenda siku zote hizo, na kupewa kauli za ajabu na wazazi wake.
Nimejikuta nawaza mengi sana".
.
Careen alizungumza kwa hisia sana, akameza mate kidogo na kuendelea kuzungumza "Kuna muda nimewaza ni kheri nisingejuana nae, kheri nisingempa hata nafasi ya urafiki, labda asingenipenda na leo hii asingepitia maumivu sababu yangu".
.
Careen alianza kulengwa na machozi, alionyesha kiasi gani ameumia na jambo lililotokea kati yake na Peter.
Akaniuliza "Nitamkumbuka kwa mengi sana, amenifanyia mengi sana.
Nakumbuka kipindi nilichogombana na wewe, kipindi nilichoachwa na boyfriend wangu, Peter alikua kila kitu kwangu.
Alipambana kuirudisha furaha yangu.
Na hata ile semina tuliyo ombana msamaha siku ile, alinilazimisha yeye twende kwenye semina.
Siwezi kumsahau".
.
Nilibaki nimetulia tu nikisikiliza, nilianza kuuona umuhimu wa Peter ndani ya maisha ya Careen.
Na hakika haijalishi Careen atazungumza kwa ujasiri kiasi gani mbele ya Peter ili kukaa nae mbali kama alivyo onywa, lakini kamwe moyoni mwake hawezi kuisahau thamani ya Peter.
.
Nilikua nawaza mengi sana juu ya Careen na Peter, lakini ghafla nilistushwa na mkono wa Careen uliotua begani mwangu.
.
Aliyatamka maneno ambayo yalianza kuivuruga akili yangu, mapigo ya moyo yalizidi.
Nikaanza kukosa amani kabisa.
.
Careen alisema "Wakati wote huo niliokuwa nae sikujua kama ananipenda, nilidhani ananichukulia kama dada yake, kama nilivyokua namchukulia.
Hivi Chris, wanaume hamuwezi kumjali mwanamke bila kumtaka kimapenzi???".
.
Swali lilikua gumu sana kwangu kujibu, nikabaki nimenyamaza.
.
Hakuniacha nipumue, akaniongeza swali lingine "Mwanaume akionyesha kukujali, kukuheshimu, kukuthamini, kujitoa kwako kwa kila kitu. Ndio anamaanisha anakupenda??? "
.
Nikamtazama Careen usoni nikiwa naona kinywa kizito kujibu maswali yake.
.
Akaendelea "Kwajinsi nilivyopitia maumivu kwa boyfriend wangu aliyeniacha, sitamani tena kuwa na mwanaume wa aina yeyote yule".
.
"Chris, matendo yako yanafanana na ya Peter.
Naogopa usije pitia maumivu kama anayopitia Peter.
Naomba niambie ukweli leo, unanipenda??? ".
.
Kuendana na maneno aliyozungumza, na swali alilonipa.
Nilijikuta nimekaa kimya nisijue cha kujibu.
.
Anaogopa kupenda tena, itakuwaje nikisema nampenda.
Anasema hataki nipitie maumivu kama ya Peter, itakuwaje nikijibu nampenda.?
Nilibakisha maswali mengi kichwani, lakini Careen akaniambia "Chris, niweke wazi leo hii
."

Je Chris atajibu nini??? Na ni nani mnafki anayetoa siri za kina Chris
.
Usikose sehemu ya 18
#Itaendelea...


Sehemu ya Kumi na tisa soma hapa Maumivu Yasiyo kwisha (Endless Pain)
 
Back
Top Bottom