Hali ni mbaya—tena mbaya sana. Ni vigumu kuelezea kiwango cha uharibifu bila kushikwa na hasira kali. Tumeingia katika zama za giza, zama ambazo maadili yameanguka vibaya, na kizazi kipya kinazama kwenye kinamasi cha upotovu bila hata kupambana. Wale tuliowatarajia kuwaongoza—mababa wa kiroho, wazazi, wazee wa mitaa, viongozi wa jamii—wanashuhudia uozo huu kwa macho yao, lakini wamenyamaza kama waliolishwa sumu ya uwoga au walioshindwa na mapambano. Hakuna anayejali. Hakuna anayesimama kusema, “Hapana! Hili haliwezi kuendelea!”
Serikali? Hapana! Serikali haina jukumu la maadili. Serikali inaweza kuweka sheria, inaweza kuboresha miundombinu, inaweza kupiga vita ufisadi—lakini haiwezi kuwafanya vijana wapende heshima yao. Haiwezi kuwafundisha utu, haiwezi kuwalazimisha waishi kwa uadilifu. Hilo ni jukumu la jamii, la familia, la wale wanaotazama bila kusema neno huku kizazi kizima kikizama.
Leo nimekaa na vijana wa mtaani, nikawasikiliza kwa makini. Nilichosikia kilinitetemesha. Vijana hawa hawazungumzi mambo ya kusadikika, wanazungumzia hali halisi mitaani, mambo ambayo yanafanyika kila siku, kwenye kila kona ya miji yetu. Wanazungumzia jinsi ambavyo baadhi yao wamekosa mwelekeo, si kwa sababu ya ugumu wa maisha tu, bali kwa sababu ya tamaa ya kipuuzi, uvivu wa kufanya kazi za heshima, na msukumo wa marafiki waliotangulia kwenye upotovu.
Wamebaki wanyonge, wanakosa sauti ya kuwakemea na kuwaokoa. Na miongoni mwao kuna wavulana waliowindwa na mabasha—wanaume wazima, wenye pesa, wanaowashawishi kwa maisha ya starehe ili wawaharibu. Mabasha hawa hawafanyi hivi kwa bahati mbaya. Wanawatafuta wale walio safi, wale wasiokuwa na historia ya kufanya mambo haya, kwa sababu wale waliokwisha kubuhu katika tabia hizi wana magonjwa sugu. Wanaogopa hatari ya kuambukizwa, hivyo wanaamua kuharibu wale waliobaki na usafi wao. Huu si uvumi. Haya ni mazungumzo yanayofanyika mitaani, hadithi zinazotolewa na wahanga wenyewe. Na sisi tunafanya nini? Tunalalamika kwenye mitandao huku tukikaa kimya mtaani?
Hili ni giza kubwa. Vijana wanasema kwamba sasa si ajabu kuona kijana wa kiume akimuomba mwanaume mwingine bia kwenye baa. Hili lilikuwa jambo lisilofikirika zamani. Mwanamke kufanya hivyo kunaeleweka kwa sababu kuna namna za "kulipia" hiyo bia. Lakini kwa mwanaume? Malipo yake ni nini? Hili linapaswa kututisha sote, kwa sababu linamaanisha kuwa thamani ya kijana wa kiume imeporomoka hadi kiwango cha kutisha.
Na vipi kuhusu bodaboda? Kazi ambayo ilipaswa kuwa ya heshima, imekuwa chanzo cha upotovu kwa vijana wengi. Mashoga wamekuwa wateja wao wa kawaida, na kutokana na mazingira ya kazi yao—kukutana na watu wa kila aina kila siku—wamejikuta wakiingizwa taratibu katika mtindo wa maisha wa giza bila hata wao kuelewa kilichowapata. Hakuna anayewasaidia. Hakuna anayekemea. Jamii inakaa pembeni ikiwatazama vijana hawa wakiharibika.
Na sasa tunaambiwa kwamba Kariakoo imegeuka kuwa moja ya vituo vikuu vya kuzalisha mashoga na mabasha. Vijana wanajisifia hadharani kwa "mahusiano" yao na mashoga wa mjini. Wanajiona kuwa wao ni wa kisasa, wamefunguka, wameshajua "siri ya maisha rahisi." Hivi wazazi wa vijana hawa wako wapi? Viongozi wa jamii wanafanya nini? Mababa wa kiroho wanafanya nini?
Hatuwezi kujifanya kwamba haya mambo hayapo. Hatuwezi kuficha vichwa vyetu mchangani kama mbuni tukiamini kuwa mambo yatatengenea yenyewe. Haya mambo hayatatengenea yenyewe. Kama hatutasimama sasa, kama hatutapaza sauti, kama hatutakemea, basi tutajikuta tumezalisha kizazi cha vijana waliopoteza heshima yao kwa nafsi zao, waliokata tamaa, na waliokubali kupelekwa na upepo wa starehe za muda mfupi kwa gharama ya utu wao.
Hili ni janga. Na janga hili halitatatuliwa kwa mazungumzo ya mtaani au mijadala mitandaoni pekee. Tunahitaji vitendo. Tunahitaji ujasiri wa kusema, “Hapana! Hili si sahihi!” Tunahitaji wazazi walioko macho, walimu wenye msimamo, viongozi wa jamii walioko tayari kupambana, na vijana wenye uwezo wa kusema "hatutaki kuwa sehemu ya uovu huu!"
Hali ni mbaya. Na ikiwa hatutasimama sasa, itakuwa mbaya zaidi.