Mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa amekataa kupanda gari la serikali lililopelekwa gerezani Segerea ili kumchukua baada ya kulipiwa faini.
Awali kulitokea mzozo kati ya wafuasi wa CCM wakiongozwa na Ndugu Humphrey Polepole ambao walitaka Msigwa apande gari ya serikali kwa madai kuwa amelipiwa faini yake na Rais JPM, lakini wafuasi wa Chadema wakamtaka apande gari aliloandaliwa na Chadema kwa kuwa chama hicho ndicho kimemlipia faini kupitia michango ya watanzania.
Wafuasi hao walidai kwamba wakati Rais JPM anapeleka fedha tayari Chadema ilikua imeshamlipia Msigwa na hivyo fedha hiyo irudishwe kwa Rais ili ikafanye shughuli nyingine za maendeleo.
Kufuatia mzozo huo wafuasi wa Chadema walizuiwa kuingia gerezani humo na wafuasi wa CCM wakiongozwa na Polepole waliingia wakiwa kwenye magari ya serikali tayari kumlaki Msigwa.
Lakini Msigwa alikataa kupanda gari ya serikali aliyoandaliwa na kutembea kwa mguu hadi nje ya gereza walikokuwa wafuasi wa Chadema ambao wamemlaki kwa shangwe na sasa anaelekea makao makuu ya Chadema, eneo la Kinondoni ili kufanya mkutano na wanahabari.!