Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo, leo Mei 17, 2023.
Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kimataifa la Kariakoo wametoa malalamiko mbele ya Waziri Mkuu ambapo wameilaimu TRA kwa kutokufuata taratibu sahihi za utozaji kodi wakishirikiana na Jeshi la Polisi.
Mfanyabiashara mmoja akitoa malalamiko yake amesema kampuni yake imewahi kusumbuliwa na Askari wa Kituo cha Kamata akidaiwa kutokuwa na risiti halali za mizigo yake, jambo ambalo sio la kweli. Pia, amemtaja kwa jina moja Askari anayehusika na kashfa nyingi za hapo kuwa ni "Mpemba"
Aidha, mfanyabiashara mmoja aliyesimama kwa niaba ya wafanyabiashara wa Vitenge amemhoji Waziri Mkuu kama Serikali haitaki wanawake nchini wapendeze maana wamekuwa wanachukuliwa kama wanauza madawa ya kulevya.
Wamewalamumu pia watu wanaohusika na uzoaji wa taka kuwa wanadai pesa zisizotakiwa, kwani huenda hadi kwenye stoo zao. Pia, watu wa TRA wamekuwa wanawafata hadi majumbani wakitaka pesa. Mama huyo amehoji, "Kwa hiyo tukadange?, hapa sio mahali sahihi kwa kuongea, nitahatarisha maisha yangu. Nipe namba nije chemba tuzungumze"
Kuhusu sababu ya kufunga maduka, mfanyabiashara mmoja amesema walifanya hivyo kutokana na;
- Uwepo wa utitiri wa kodi usioendana na uhalisia, "Double Taxation"
- Kuhamia kwa maduka barabarani kwa jina maarufu la machinga, watu ambao wamekuwa wanatumiwa na wafanyabiashara wakubwa hivyo kubana biashara zao (wafanyabiashara waliosajiliwa). Duniani kote hakuna machinga kwenye vituo halisi vya kibiashara
- Adhabu za makosa ya kutolipa kodi zisizolipika sababu ya ukali wake hivyo kuweka mianya ya rushwa
Kero nyingine iliyotajwa ni maafisa wa TRA kuwa na mamlaka makubwa ya kukadiria faini za malipo pindi wanapowakatama wafanyabiashara kwa makosa mbalimbali, ambayo mengi ni ya kusingiziwa. Jambo hili huleta mianya ya rushwa kwa sababu TRA huwaalika kwa mazungumzo ya pembeni kinyume cha taratibu.
Pia, urasimu kwenye mamlaka za serikali hasa utoaji wa leseni, kupandishwa kila mwaka kwa makadirio ya kodi kwa lugha maarufu ya "Maelekezo kutoka juu", kodi kubwa ya stoo za bidhaa, mfumo mbovu wa kodi ya forodha bandarini pamoja na kamatakamata za aina mbalimbali zinazofanyika sokoni hapo.
Hoja nyingine iliyoibuliwa ni Matamshi ya Waziri Mwigulu Nchemba kudharau wabunge wengine ambao ni wawakilishi wa wananchi, amekuwa na kauli chafu zinazokatisha tamaa wafanyabiashara, mfano ni ile ya kuwa yeye ni daktari wa uchumi, hawezi kubishana na waganga wa kienyeji.
Mfanyabiashara huyo amesema jeuri yote ya TRA inasababishwa na Waziri wa fedha ambae ni bosi wao mwenye jeuri, hashauriki, haambiliki. Wamewahi kuzungumza nae mara kadhaa lakini hajawahi kutekeleza hoja za mazungumzo hayo. Pia, mfanyabiashara huyo amesema Waziri Nchemba hafai kuwepo kwenye nafasi yake.
Waziri wa Biashara amelaumiwa pia kwa kutosimama na wafanyabiashara hasa kwa kauli yake ya Bungeni kuwa hakukuwa na mgomo Kariakoo. Wafanyabiashara hao wamesema kuwa haijawahi kutokea hata mara moja Waziri huyo akasimama na wafanyabiashara.
Urasimu mkubwa wa mizigo inayotoka Zanzibar umetajwa kuwepo tofauti na wafanyabiashara wanaotoa mizigo nchi zingine kama Dubai n.k. Pia, kumekuwepo na watu wengine wanaotoza kodi baada ya kutoa mzigo bandarini, watu hao wanapaswa kuwepo bandarini ili kurahisisha uliopaji wa kodi na kuokoa muda.