Mhasibu wa Benki ya BOA wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Martha Towa (30), amefariki dunia baada ya kutekwa na watu WASIOFAHAMIKA kisha kuchomwa moto kwa kutumia mafuta yanayodhaniwa ni petroli wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo akizungumza na gazeti la Nipashe ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Machi 3 mwaka huu, maeneo ya Mitamba mkoani Pwani, ambapo wasamaria wema walilijulisha Jeshi la Polisi kuhusu tukio hilo.
Alisema wasamaria wema walimkuta Martha, ambaye ni mkazi wa Kwa Mbonde akiwa na majeraha ya moto na kutoa taarifa polisi majira ya saa 4.30 usiku na polisi walikwenda na kumchukua kisha kumpeleka Hospitali ya Mkoa wa Pwani (Tumbi), Kibaha.
Alisema kuwa baadaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi na usiku wa kuamkia Machi alifariki dunia. Kamanda Lutumo alisema kutokana na mazingira yenye utata ya kifo hicho, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ikiwako kubaini sababu za kuchomwa moto.
Chanzo: Nipashe