Kwa wanaokumbuka, miaka ile ya themanini, halusi na sherehe zingine zilikuwepo, lakini ziliendeshwa tofauti na sasa hivi. Familia ya wahusika iliandaa sherehe, watu walialikwa bila kutoa michango,mwalikwa ulichotakiwa kufanya ni kuandaa zawadi.Kwa sababu hiyo, mahalusi walipata zawadi za kutosha na mtu hakutakiwa kutoa pesa kabisa.
Kamati za maandalizi ya sherehe zimekuwa dili,kuna watu kila anapoamka asubuhi anajiandaa kuongoza vikao vya halusi,mtu anaongoza vikao zaidi ya vitatu kwa siku.Asilimia kubwa ya michango ya halusi huwanufaisha wasiokusudiwa.Badala ya kuwaweka watu pamoja,sherehe zimeongeza mipasuko,matumizi mabaya ya michango huwa chanzo cha migogoro.
Nimeshuhudia vituko vingi baada ya sherehe,kuna sherehe ambazo wahasibu hukimbia na michango,kuna zile ambazo kamati hutoa tenda kwa watu dhaifu na hulipwa pesa nyingi mno,kuna sherehe ambazo mtu anachangia 100,000/-lakini anapata soda moja na bits basi wakati zawadi ya kamati ni 500,000/-huku baadhi ya viongozi wakivimba mashavu.
Sherehe nyingi, hasa halusi hufungwa usiku sana, hivyo mgeni mwalikwa analazimika kuandaa bajeti ya usafiri.Ili kurejesha dhima ya sherehe kuwa ni furaha na amani, upo umuhimu wa kurudia utaratibu wa miaka ya nyuma.Hakuna kamati ya maandalizi,sherehe inaandaliwa na familia,waalikwa mnatoa zawadi tu, na sherehe zote zinaisha kabla ya saa kumi na mbili jioni.
Nisisitize hapa,tunajadili sherehe,sio misiba,msiba ni tukio la dharula wakati sherehe huandaliwa. Ni muhimu na ni lazima kushiriki misiba kwa hali na mali lakini sio sherehe za harusi na nyinginezo. Naomba tena waziri atakayekuwa anasimamia ustawi wa jamii aingilie kati, atafute namna ya kukomesha tabia hii inayoanza kuwa kero katika jamii.