RIPOTI YA ZIARA YA MSTAHIKI MEYOR CHIEF A. KARUMUNA KATIKA KATA ZOTE (14) ZA MANISPAA YA BUKOBA KUHUSU MADHARA YALIYOTOKANA NA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI KAGERA – 11/10/2016.
UTANGULIZI
Mh. Mgeni rasmi Mbunge wa jimbo la Bukoba mjini Mh. Wilfred Muganyizi Lwakatare ambaye pia ni waziri kivuri wa Ardhi na Maendeleo ya makazi Bungeni, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa madhehebu ya dini, Wah. Madiwani wa baraza la madiwani Bukoba Mnispaa, ndugu wenyeviti wa mitaa na wajumbe wa serikali za mitaa, mabibi na mabwana, Mungu awe pamoja nasi.
Mh. Naomba kutoa taarifa kwamba nimetembelea jimbo zima kama tulivyokubaliana mimi na wewe na kupitia ratiba iliyopangwa na kamati ya fedha na uongozi, nimetembelea kata zote kumi na nne za Manispaa ya Bukoba, tumekutana na kamati za maendeleo za kata, wajumbe wa serikali za mitaa na wadau mbalimbali wa maendeleo ya Bukoba na wananchi kwa ujumla.
Ifuatayo ni taarifa fupi;-
1. Idadi kubwa ya wahanga waliobomokewa na nyumba zao na pia wapangaji bado wako nje bila hifadhi wala kinga yoyote baada ya kukosa misaada ya dharula ya makazi ya muda wakati wakisubili utaratibu wa ujenzi na ukarabati wa makazi yao ya kudumu.
2. Misaada iliyokwisha tolewa ya vyakula kama mchele, sukari, maharagwe, mahindi, biskuti pamoja na turubai, magodolo na neti za mbu, ni hafifu mno kiasi cha kutotosheleza mahitaji ya wahanga.
3. Kutokana na misaada hiyo iliyotolewa kuwa ya kiwango kidogo sana kulinganisha na wahitaji imesababisha marumbano makubwa kati ya wananchi na kamati za maafa za kata na mitaa.
4. Misaada hiyo kiduchu imekuwa ikipelekwa kwenye kata ili kugawiwa kwa wahanga katika muda ambao sio salama, yaani jioni jambo linalopelekea misaada hiyo kugawiwa mpaka nyakati za usiku sana ambapo usalama huwa ni mdogo sana, pamoja na wanaostahili kupata misaada hiyo kutojulikana na kujulishwa mapema hupelekea kundi kubwa la wananchi kusubili misaada asubuhi mpaka jioni katika ofisi za kata na misaada hiyo inapofika inakuwa ni kwa ajili ya watu wachache mno hivyo kuibua magonvi ya kugombania misaada hiyo hali ambayo ni hatari kwa wagawaji na wananchi wenyewe.
5. Kulingana na idadi ndogo ya misaada inayopelekwa kwa wananchi na maelekezo toka kamati ya wilaya ya maafa ya namna mbovu ya ugawaji limepelekea wananchi kuwa na uhasama na viongozi wa serikali za mitaa na watendaji kwa kuwatuhumu kuwa wanaihujumu misaada hiyo na kujigawia wenyewe jambo ambalo sio la kweli.
6. Utaratibu wa kubaini athari za tetemeko umefanyika katika namna zisizo za kuaminiana jambo litakaloleteleza kupingana kwa takwimu na kuzidi kucheleweshwa kwa huduma kwa wahanga kama zipo, awali serikali za mitaa zilipita kubaini waathirika, baadaye serikali za mitaa kwa kushirikiana na walimu, zoezi ambalo lilifanyika mapema sana na likafnikiwa kwa sababu watu wengi walikuwa bado wapo katika maeneo yao kutokana na taharuki ya tetemeko. Baada ya ripoti ya viongozi wa serikali za mitaa kwa kushirikiana na walimu, mkuu wa wilaya ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maafa wilaya aliliagiza jeshi la akiba(mgambo) kupita tena katika maeneo yote ili kuhakiki taarifa za awali, jambo hili limeonyesha kutoaminika kwa kamati za maafa za mitaa na walimu walioshirikiana nao kufanya zoezi zima kwa kujitolea na kwa uaminifu mkubwa bila chakula wala maji ya kunywa kutwa nzima, lakini pia zoezi la jeshi la akiba (mgambo) lilikuja kipindi ambacho baadhi ya watu walikuwa wamekwisha hama maeneo yao na kwenda kutafuta hifadhi mahala pengine na nyumba nyingine kutokuwa na wenyewe, lakini pia mgambo hawakuwa tiyari kumuandika aliyekwisha anza ujenzi kama muathirika, pia kuna maeneo ambayo mgambo hawakufika kabisa, kibaya zaidi watu hao mgambo waliopewa kazi nyeti ya kuhakiki kazi ya viongozi wa serikali za mitaa kwa kushirikiana na walimu, wengi wao hawajui kusoma wala kuandika. Matokeo yake takwimu za mgambo zitakinzana na takwimu za awali zilizokusanywa na viongozi wa serikali za mitaa kwa kushirikiana na walimu, na kwa vile watumishi wengi wanapenda kupanda vyeo kupitia migongo ya wengine ukiwa ni ukandamizaji watajitokeza na kusema serikali za mitaa ziliongeza waathirika hewa ili kujinufaisha, jambo ambalo sio la kweli hata kidogo na litakuwa linahatarisha ajira za watendaji hasa katika kipindi hichi cha kutumbuana bila kujitetea.
7. Watendaji wa kata na mitaa wamekuwa wakitekeleza maagizo ya kamati za maafa ya mkoa na wilaya na kutenda kwa garama zao wenyewe, nauli, kutoa nakala za nyaraka mbalimbali na gundi za kubandikia matangazo.
8. Ukosefu wa taarifa za mapato na matumizi ya mfuko wa maafa mpaka sasa ni tatizo linalohatarisha amani ya watendaji na viongozi wa kuchaguliwa kwa wananchi kuhisi misaada inatolewa kwa wingi na kuishia mikononi mwa watendaji na viongozi, jambo ambalo sio sawa hata kidogo.
9. Kutoshirikishwa kwa viongozi wa kuchaguliwa/wawakilishi wa wananchi Mbunge, Meya wa manispaa na balaza la madiwani katika kamati za maafa ya mkoa na wilaya kumesabisha zoezi hili la kuwahudumia wananchi kukosa ufanisi kwa sababu wanao wajua wananchi zaidi na namna walivyoathirika ni wawakilishi wao ambao kwa kutengwa kwao hawana majibu juu ya ni nini kamati ya maafa inafanya. Mkuu wa wilaya ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya maafa ameshindwa kuwaita Mbunge, Meya, madiwani, wenyeviti wa mitaa na wajumbe wao ili kuwaeleza utaratibu ulivyo na wao kupata nafasi ya kushauri. Jambo hili ni baya sana na linawachonganisha wawakilishi wa wananchi na wananchi wenyewe kwa kukosa imani na uwakilishi wao hasa linapokuja swala la migao ya misaada hafifu kwa wananchi jambo ambalo linazua pia magonvi.
10. Misaada imekuwa ikipelekwa moja kwa moja katika mitaa kwa kuwatumia Redcross na kuipeleka kuigawia katika makazi ya viongozi jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa viongozi hao.
11. Wakati alipokuja Waziri mkuu kuwafariji wananchi wa mkoa Kagera kwa madhara ya tetemeko la ardhi pamoja, na mstahiki Meya kama raia namba moja kwenye manispaa na kiongozi wa manispaa kunyimwa nafasi ya kuonana na waziri mkuu kuwawakilisha wananchi bado mkuu wa wilaya ya bukoba mjini kipindi hicho akikaimu nafasi ya mkuu wa mkoa alimkabidhi taarifa ya uongo mkuu wa mkoa na ikasomwa mbele ya waziri mkuu na watu wakazomea sana kwa sababu ripoti ilitaja kwamba wameishawapatia wananchi mahala salama pa kujihifadhi jambo ambalo halikuwa sawa hata kidogo, hali iliyoanza kupoteza imani kwa mwenyekiti huyo wa kamati ya maafa kwa ngazi ya wilaya, na kama waliweza kusema uongo mbele ya waziri mkuu mchana kweupe bado wananchi wana mashaka pia na taarifa zinazopelekwa kwa viongozi wa kitaifa na mataifa juu ya hali halisi ya wananchi wa mkoa Kagera ilivyo kwa sasa takrabani mwezi mmoja tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi.
12. Mpaka sasa kuna wajumbe na wenyeviti wa mitaa na watumishi wa umma ambao nao walipoteza makazi na mpaka sasa hawajapata msaada wowote kisa tu ni viongozi, na kwa sababu ya misaada kutoendana na uhitaji ikionekana mjumbe au mwenyekiti amepewa mgao basi inaweza kuzuka vita ya ajabu, kuwa kiongozi mwakilishi wa wananchi hakukuondolei uhitaji kama raia, ukizingatia wajumbe na wenyeviti wa serikali za mitaa huwa hawalipwi popote pale.
13. Serikali kupitia kamati ya za maafa ya mkoa na wilaya zimeanza ukarabati wa shule bila kutoa taarifa kwa ngazi yoyote ya eneo husika, Diwani, watendaji, wenyeviti wa mitaa na wajumbe, kamati za shule mpaka walimu hawana taarifa na huo ukarabati unaofanyika kwenye hizo shule wa kuziba nyufa, na kwa taarifa zilizopo ni kwamba hata hizo nyufa hazizibwi katika namna nzuri ya kuimarisha bali kinachofanyika ni kiziba nyufa zisionekane kwa kuchapia udongo juu ya nyufa, kitu kitakachokuja kuleta maafa mengine siku za mbeleni.
14. Kupingana pingana kwa kauli za viongozi wa serikali juu ya huduma zinazopangwa kutolewa kwa wananchi kumeleta shaka kubwa sana kwa wananchi, Mh. waziri mkuu akiongea katika viwanja vya Kaitaba alisema watu watagawiwa mifuko ya simenti na bati, baadaye amekuja Mh. Raisi anasema serikali haitawajengea watu nyumba, sababu ya kupingana kwa kauli hizi ni nini kilichopo hapo!!?
15. Pamoja na vyombo vya habari kutangaza kila siku kwamba misaada bado inapokelewa lakini wananchi wameshindwa kujua mpaka sasa ni kiasi gani kimechangwa na misaada ya aina gani na kwa kiwango gani na kutoka kwa nani, kimsingi mapato na matumizi, lakini pia kuna michango hii ya kupitia mitandao ya simu, mbona haisemwi mpaka sasa imekusanya kiasi gani.
16. Serikali na raia walipiga picha makazi ya watu masikini na kuzisamba dunia nzima ili kuonyesha hali halisi ya madhara ya tetemeko la ardhi ili atakayeguswa na hali ile mbaya awiwe kuchangia kwa hali na mali kuwanusuru watu na hali mbaya waliyokuwa nayo, shukurani ziwaendee mataifa rafiki, taasisi na mashirika mbalimbali, na watu binafsi walioguswa na kuamua kutoa chochote kwa ajili ya watu wa Kagera, Mungu awabariki sana na awarejeshee pale walipotoa. Serikali ikaamua kuweka kila msaada katika kapu moja yaani mfuko wa maafa kagera bila kumuuliza kila aliyetoa msaada alitoa kwa kuguswa na nani ama eneo lipi, na kuweka marufuku kwa mtu yeyote kufungua akaunti na kuchangisha misaada yoyote na marufuku pia katika kugawa moja kwa moja misaada kwa wananchi bila kibari na kuambatana na kamati ya maafa ya mkoa, mwisho wa siku serikali inawatangazia wananchi kwamba haitajihusisha na ujenzi wala ukarabati wa makazi yao na badala yake michango yote itaelekezwa katika ujenzi wa taasisi kama mashule, zahanati na miundo mbinu ya barabara vilivyoathiliwa na tetemeko la ardhi.
17. Kuna kila dalili za mambo ya kisiasa katika utekelezaji wa ukarabati wa taasisi, wananchi wanahoji ni vigezo gani vimetumika kuipa kipaumbele shule ya Omumwani inayomilikiwa na jumuia ya wazazi badala ya Mugeza ama shule zingine nyingi za serikali na zenye idadi kubwa ya wanafunzi na ziko katika hali mbaya sana?
18. Wakati wa harambee iliyoendeshwa na Mh. Waziri mkuu kupitia vyombo vya habari kuna wafanya biashara walijitolea kuzijenga shule za sekondari za Ihungo na Nyakato, iweje serikali iendelee kuzitaja kama mzigo wake na kuelekeza nguvu ya ujenzi maeneo yale? Lakini pia serikali ya Japan iliomba kufanya ukarabati wa taasisi zingine, nini ufafanuzi wa mambo haya ili kujua kama michango mingine inaweza kuelekezwa katika ujenzi na ukarabati wa makazi ya watu.
19. Tathmini ya gharama ya ukarabati na ujenzi wa makazi ya wananchi waathirika wa mkoa Kagera inazidi kupandishwa mara dufu na vyombo vya habari kila siku, kinyume na taarifa iliyosomwa bungeni na Mh. Waziri mkuu, jambo hili linaleta mashaka kwamba serikali inataka kuiaminisha dunia kwamba kuwasaidia wananchi wa mkoa Kagera juu ya swala la makazi ni jambo gumu sana na lisilowezekana, kitu ambacho sio sawa hata kidogo.
20. Pamoja na mamlaka waliyonayo mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya kama viongozi wa kamati ya maafa ya mkoa na wilaya lakini hata mara moja hawajawika kuitembelea mitaa wakati wowote kujionea madhara na uhalisia wa maisha ya wananchi na hifadhi zao hasa katika kipindi hiki cha majira ya mvua, familia ziko nje, mari za watu ziko nje zikinyeshwewa na mnvua, watoto wanapigwa na baridi kali na matokeo yake wameanza kuugua maralia na magonjwa mengine kama arumonia, lakini pia kwa maeneo kama kata Hamgembe miundombinu ya vyoo iliharibika sana na katika majira haya ya mvua kutakuwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira na sasa tujiandae tena kukikabili kipindupindu kama hatua za haraka hazitachukuliwa kwa kutelekeza miundombinu ya makazi ya watu.
21. Lilipotokea janga la kuzama kwa meli ya Mv. Bukoba Mh. Raisi wa kipindi hicho W.B. Mkapa aliwahutubia wana Kagera katika uwanja wa Uhuru mjini bukoba, katika kuwapa pole wafiwa ilifika mahali akashindwa kuendelea baada ya hisia kali na kutokwa na machozi, pamoja na mkoa Kagera kwa ujumla lakini manispaa ya bukoba imeathiriwa na tetemeko la ardhi kwa asilimia kubwa sana na vifo takrabani 16 kati ya vifo vilivyolipotiwa kwa mkoa Kagera, ni jambo la kuumiza sana wananchi wa manispaa hawajapata kumuona kiongozi wao wa nchi akileta walau maneno ya faraja kwao mpaka sasa yapata mwezi mzima badala yake zinakuja taarifa kwamba Mh. Raisi alituma msaada katika wilaya ya Karagwe na kumsaidia mjane aliyekwisha anza kujisaidia katika ujenzi, lakini je mkoa Kagera una wajane wangapi wa aina hiyo!? Na wote watafikiwa na kutendewa kama yule alivyotendewa, au nia hasa ya kitendo kile ilikuwa ni nini?
22. Pamoja na misaada mingi kutolewa, na kuhodhiwa na serikali, bado wananchi hawajasikia mchango wowote wa serikali toka kwa mamlaka ya Mh. Raisi na Waziri mkuu, lakini pia ule mfuko wa maafa wa serikali unaotengewa bajeti kila mwaka uko wapi na unafanya nini?
HITIMISHO.
Wito wetu kwa serikali.
1. Serikali itambue kuwa tetemeko la ardhi hasa katika manispaa ya bukoba halikuathiri vyakula, wala vyombo vyakupikia, kama ni njaa ya chakula basi ilikuwepo hata kabla ya tetemeko la ardhi na hakuna aliyewahi kuiomba serikali msaada wa vyakula katika manispaa ya bukoba, kuendelea kuleta misaada ya chakula tena kwa uchache wa kiwango cha watu 20 kati ya 700 kwa mtaa mmoja kutaleta visa na magonvi makubwa kati ya wananchi na viongozi wao na wananchi wao kwa wao lakini pia inaweza kuwafukuzisha kazi watendaji wetu wa maeneo husika kwa lugha ya kisasa ya kutumbuana, ukimtumbua aliyeko chini yako ndipo uonekane unajua kufanya kazi na upande cheo.
2. Uhitaji wa waathirika wa tetemeko la ardhi ndani ya manispaa ya bukoba ni ukarabati na ujenzi wa makazi yao na sio vyakula.
3. Kuendelea kupeleka vyakula kama mchele, mahindi, maharagwe, sukari na biskuti na majani ya chai tena kwa uchache wa kiwango kinachotolewa na kuchukua kumbukumbu za picha kwamba serikali inawahudumia wananchi wake ni udharirishaji mkubwa na ikiwezekana ukatishwe mara moja na badala yake vyakula hivyo vikabadilishwe na bidhaa za ujenzi na zigawiwe kwa watu, watu wakisharejea katika makazi yao wataendelea na shughuri zao za kujitafutia chakula.
4. Serikali ikiwezekana iwasiliane na kila aliyetoa msaada, mkubwa kwa mdogo iwahoji kuhusu angependa msaada alioutoa uelekezwe wapi, kwa wananchi moja kwa moja au kwa taasisi za serikali? Ufafanuzi huo wa kila aliyetoa msaada uisaidie serikali kufungua vikapu viwili, cha kwanza kiitwe maafa kagera kwa ajili ya taasisi na kikapu cha pili kiitwe maafa Kagera kwa ajili ya makazi ya wananchi na misaada hiyo iwekwe kwenye vikapu hivyo kulingana na aliyetoa ameguswa na eneo lipi, inasikitisha sana watu wametoa misaada kwa ajili ya ndugu zao na kufuata utaratibu uliopangwa leo hii unawaeleza wananchi kwamba hawatofikiwa na michango hiyo moja kwa moja kwa ajili ya makazi na kujistili na familia zao!! Jambo hili si jema na serikali ilitafakari upya.
5. Pamoja na kama serikali itawiwa kupeleka misaada ya vifaa vya ujenzi lakini tunatoa wito pia serikali ione sasa umuhimu wa kuleta hali ya dharula kwa mkoa kagera katika nyanja zote za maswala ya ujenzi kwa kipindi cha muda flani kama lilivyokuwa pendekezo la Mh. Mbunge Wilfred Muganyizi Lwakatare katika uwanja wa Kaitaba mbele ya Mh. Waziri mkuu na mbele ya wananchi kwamba vifaa vya ujenzi kama simenti, nondo, misumali na mabati viondolewe kodi na vije katika mifuko yenye nembo maafa kagera ili kuwapa mwanya wananchi wa Kagera kurejesha makazi yao haraka sana iwezekanavyo, pia katika kipindi hichi mamlaka za madini zisitishe kwa muda utozaji wa kodi katika material za ujenzi kama mawe, kokoto na udongo ili kuwapa nafuu wananchi kwa kipindi cha muda flani, vivyo hivyo kwa watu wa maliasiri na mazao ya misitu. Hali hii na misamaha hii ya kodi haitakuwa ya kudumu bali kwa kipindi cha muda flani ili kuwasaidia hawa masikini kujijengea makazi yao.
6. Ikiwa mambo haya yatawagusa na kuionea jamii hii ya kimasikini wa wana Kagera huruma tunaomba takwimu iliyochukuliwa na viongozi wa serikali za mitaa ambao kisheria ndiyo kamati za maafa za mitaa na wakashirikiana na walimu tena ndani ya kipindi sahihi ambacho watu walikuwa bado katika maeneo yao, takwimu hizo ndizo zitumike katika kuwahudumia wananchi na ikiwa kutakuwa bado kuna kutoziamini takwimu hizo, zoezi maalumu linaweza kuandaliwa hata kwa siku tatu mfululizo zikiwahusisha timu maalumu ya viongozi wa serikali za mitaa, wenyeviti na wajumbe, jeshi la akiba, watumishi wa umma na mjumbe toka kamati ya maafa ya ngazi ya mkoa na wilaya ili kujiridhisha na kuchukua takwimu sahihi zisizokuwa na walakini japo changamoto zake zitakuwa kwamba kuna makazi nyufa zake zimeisha zibwa na wenye uwezo wa kufanya hivyo, na viongozi wa serikali za mitaa wanawajua fika wakazi wote wa maeneo yao na kinachoendelea katika maeneo yao.
7. Kama zoezi jipya la uhakiki litafikilika kufanyika basi lifanyike wakati ambapo vifaa vya ujenzi vitakuwa tiyari vikisubili takwimu hizo, tofauti na hapo hamna haja ya kuwasumbua tena watu ambao wanajitolea kufanya hizi kazi bila chakula wala maji ya kunywa kutwa nzima lakini wakiambulia matusi na lawama kila wapitapo toka kwa wananchi waliojikatia tamaa baada ya kuona serikali yao inawatenga.
8. Tunatoa wito pia ifike mahala mkuu wa wilaya aheshimu mamlaka za serikali za mitaa na kuzishirikisha katika majadiliano ya namna bora ya kutoa huduma kwa wananchi kwa sababu Meya kama raia namba moja katika mji na mkuu wa wilaya kama mtendaji namba moja ni lazima Meya apewe nafasi ya kueleza ni nini wananchi wenzake wanataka kupitia balaza la madiwani na mkuu wa wilaya aeleze ni nini anapanga kuwapelekea wananchi, mambo haya ya kujificha na kutukwepa yakiendelea hatutakubaliana na hali hii hata kidogo lazima tukae meza moja na tujadili namna bora ya kuwahudumia wananchi.
9. Kazi yetu kama wawakilishi wa wananchi kwa kuchaguliwa ni kuibana serikali na kuhakikisha inatoa huduma kwa wananchi zinazostahili, na kazi hii tumeilia kiapo na hatutokaa kimya hata mara moja tukiona wananchi wenzetu wakipuuzwa hata katika vipindi vya maafa kama hivi.
10. Nitoe wito kwa ndugu wananchi wenzangu kwamba sisi kama halmashauri kwa kushirikiana vyema na ofisi ya Mbunge bukoba mjini tumejitahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha wananchi wanapata hifadhi kwa kushawishi michango kupitia viongozi wa kisiasa na kidini mashirika na taasisi mbalimbali na watu binafsi na kwa michango yetu wenyewe na kwa kuheshimu utaratibu uliowekwa wa kudumbukiza kwenye kapu moja la maafa mkoa kagera.
11. Sasa umefika wakati wa kuieleza serikali kwamba watu wanahitaji hiyo misaada iwafae wakati ambapo maafa mengine kama magonjwa kwa watoto na kipindupindu kwa wote hayajawafika. Na tutalifanya hilo kwa garama yoyote pamoja na kutengwa na kukwepwa.
12. Niwaombe ndugu wananchi mtupe muda kidogo tutekeleze wajibu wetu kama viongozi wawakilishi wenu na majibu mtayaona, na wasipotekeleza tutatarudi kwenu na tushauliane upya namna nyingine ya kudai haki zetu.
13. Na ni fursa pia nadhani ya kuifundisha serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania namna bora zaidi za kutoa huduma kwa wananchi wakati wa maafa kama haya.
14. Lakini pia ni fursa ya kuikumbusha serikali na kuueleza ulimwengu mzima vipindi vigumu ambavyo mkoa Kagera umevipitia toka kuwa kati ya mikoa tajiri Tanzania na mpaka sasa kuwa kati ya mikoa masikini Tanzani, kuanzia VITA VYA KAGERA, UKIMWI, MNVUA ZA ELNINO, KUZAMA KWA MELI YA MV. BUKOBA, MNYAUKO ULIOUA MIGOMBA, KIFO CHA ZAO LA BIASHARA KAHAWA KUPITIA VYAMA VYA USHIRIKA NA SASA TETEMEKO LA ARDHI. Ni vyema sasa serikali ikautizama mkoa Kagera kwa jicho la huruma na la kipekee kuunusuru mkoa Kagera kuzidi kudidimia katika wimbi la umasikini.
MWISHO
Wenu mtiifu
CHIEF KARUMUNA
MSTAHIKI MAYOR
BUKOBA MANISPAA.
NAKALA KWA;-
DC Bukoba (Mwenyekiti wa kamati ya maafa (w) Bukoba)
Mkuu wa mkoa Kagera (M/kiti wa kamati ya maafa Kagera)
Mkurugenzi wa Maafa Taifa.
Waziri ofisi ya waziri mkuu (anayeshughulikia maafa)
Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Viongozi wa madhehebu ya Dini.