Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Marietha Bosco Sagana (32) Mkazi wa Kitongoji cha Matarawe, Kijiji cha Marungu Kata ya Tingi Tarafa ya Mpepo, Wilaya ya Nyasa amefariki Dunia wakati anapatiwa matibabu baada ya kwa kunywa sumu ya kuulia Wadudu chanzo kikiwa ni wivu wa Mapenzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Marco G. Chilya amesema tukio hilo limetokea Novemba 8, 2023 Saa mbili usiku, ambapo mume wa marehemu alikuwa ameenda Shamba lakini alisahau simu yake nyumbani ndipo Marietha (marehemu) alivyoiona simu hiyo akaanza kuipekuwa.
Marietha alisoma meseji zote ikiwemo za WhatsApp na akafanikiwa kukuta jumbe za mume wake akiwasiliana na mwanamke Mwingine ndipo Marehemu alishindwa kuvumilia, hivyo akachukua Dawa ya Kuulia Wadudu ya Mahindi (ACTERIC) ambayo iliandaliwa kwa matumizi ya Shamba na kuinywa.
Baada ya kutenda tukio hilo majirani wanaoishi nae waligundua kitendo alichokifanya marehemu baada ya kuwaambia kuwa amekunywa dawa ya wadudu ambapo wakachukua uamuzi wa kumkimbiza Hospitali ya Mission Maguu ndipo akafariki Dunia wakati akipatiwa matibabu.