Kortini zali tupu...Kisa Dito
2007-03-08 16:36:45
Na Mwandishi Wetu, Mahakama Kuu
Kama ilivyokuwa kule kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo tena ile kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzururi, imezua zali lingine katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Waliokuwepo mahakamani hapo wanadai zali lenyewe limetokana na kitendo cha mtuhumiwa huyo kupitishwa kwenye mlango ambao si maalum kwa washitakiwa.
Habari kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania zinadai kuwa Dito alipitishwa mlango wa majaji, kitu ambacho si cha kawaida hata kidogo.
`Majaji hawakupenda hali hiyo hata kidogo?ilibidi msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ahoji sababu za kufanya hivyo,` mmoja wa maofisa wa mahakama hiyo amemuambia mwandishi wa habari hizi aliyekuwa kortini hapo.
Dito ametinga Mahakama Kuu saa 2:54 asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali.
Eneo la mahakama lilikuwa na watu wengi huku baadhi ya ndugu zake wakionekana kuzama kwenye fikra nzito.
Kesi hiyo iliyo mbele ya Jaji Augusto Mwaringa ilikuwa ianze kusikiliza maombi ya dhamana ya mshitakiwa huyo jana, lakini ikakwama baada Ditopile kucheleweshwa kuletwa kortini.
Jaji aliahirisha kesi hiyo hadi leo saa tano asubuhi.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, Dito alikuwa bado `selo` ya mahakamani hapo akisubiri muda wa kuitwa kwa kesi yake.
Februari 15 mwaka huu wakati kesi hiyo ikiwa katika mahakama ya Kisutu, mawakili wa upande wa utetezi wa Dito na ule wa mashtaka, walisuguana vikali kisheria kuhusiana na ombi la upande wa mshtakiwa waliotaka Dito apewe dhamana.
Siku hiyo, jopo la mawakili watano wanaomtetea Dito, likioongozwa na Nimrod Mkono, liliiomba mahakama hiyo ya Kisutu impatie dhamana mteja wao kwa madai kuwa kisheria, kesi ya kudaiwa kuua bila ya kukusudia haimzuii mtuhumiwa kupata haki ya kuachiwa kwa dhamana.
Baada ya ombi hilo la upande wa mshtakiwa kutolewa, Hakimu Michael Luguru alisema kwa maoni yake, Mahakama ya Kisutu bado haikuwa na uwezo wa kutoa dhamana na badala yake, suala hilo linaweza kuamuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania iliyo na uwezo wa kuisikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo ilianza kuunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu tangu Novemba 6 mwaka jana.
Katika kesi ya msingi, inadaiwa kuwa Novemba 4 mwaka uliopita, saa 1:00 usiku, katika makutano ya barabara za Bagamoyo na Kawe wilayani Kinondoni, mshtakiwa alimuua bila kukusudia dereva Hassan Mbonde.
SOURCE: Alasiri