Watu wasiopungua 40 wanahofiwa kufariki dunia kufuatia shambulio la bunduki kweye ukumbi mmoja karibu na Moscow, vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti.
Watu wasiopungua wanne waliovalia nguo za kijeshi wamefyatua risasi kwenye ukumbi wa Crocus City uliopo Krasnogorsk. BBC imethibitisha video zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii.
Video hii inaonesha watu wakijificha ndani ya ukumbi huku milio ya risasi ikisikika.
Paa la ukumbi huo, ambao ulikuwa na watu wakisubiri kutazama onyesho la muziki, limeghubikwa na moto na linaanguka, kwa mujibu wa chombo cha habari cha serikali cha Urusi.
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imeelezea tukio hili kuwa “shambulio la kigaidi”.
Polisi maalum wamefika katika eneo la tukio.
Picha za kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha watu wenye silaha ndani ya ukumbi, huku vyombo vya habari vikiripoti kuwa bado kuna watu ndani ya ukumbi huo.
Shirika la habari la Tass limesema robo tatu ya ukumbi huo unaungua na moto na paa karibu lote limeshika moto.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urusi Maria Zakharova ametaka jumuiya ya kimataifa kulaani tukio hili ambalo ameliita “la kinyama”
Vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti kuwa tiketi 6,200 zilikuwa zimeuzwa kwa ajili ya onyesho ambalo bendi ijulikanayo kama Picnic ilikuwa itumbuize.
Video Courtesy: BBC