BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
*Asema wingi wa mawaziri umelifanya Bunge kuwa butu
*Asisitiza badala ya kuisimamia serikali sasa linasimamiwa
*Alaumu viongozi wanaoheshimu wafadhili kuliko wananchi
*Alalamikia mahakama kutegemea fadhila ya Hazina
*Asisitiza badala ya kuisimamia serikali sasa linasimamiwa
*Alaumu viongozi wanaoheshimu wafadhili kuliko wananchi
*Alalamikia mahakama kutegemea fadhila ya Hazina
Andrew Msechu na Aziza Nangwa
SERIKALI imetakiwa kuhakikisha kuwa inaridhia mabadiliko ya kikatiba, kwa kuwa hakuna namna ya kuyakimbia kutokana na umuhimu wake kwa jamii ya Watanzania wa sasa.
Akifungua mkutano wa wadau wa vyama vya siasa na vya kijamii jijjini Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Wariob,a alisema mabadiliko hayo ni lazima kutokana na maendeleo ya kijamii yaliyofikiwa, ambayo yanaisukuma jamii kuipitia upya na kuiboresha zaidi katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema moja ya mambo muhimu yanayotakiwa kuangaliwa na kufanyiwa kazi kwa haraka, ni kulitenganisha Bunge na Serikali, ili kulipa Bunge nguvu ambalo sasa linaonekana kuipoteza baada ya kuelemewa na kuzidiwa nguvu na serikali.
Warioba alisema muundo wa serikali na idadi kubwa ya mawaziri waliopo bungeni umelifanya Bunge kushindwa kusimamia vyema uwakilishi wa mawazo ya wananchi, hivyo kujikuta likisimamia zaidi maamuzi ya mawaziri na serikali iliyopo madarakani na kulifanya Bunge kuwa la kupitisha hoja bila kupingwa.
"Suala la msingi ni kuangaliwa iwapo tunaweza kuliongezea Bunge madaraka, zaidi ni kuangalia uwezekano wa kulitenganisha Bunge na Serikali, idadi ya mawaziri na manaibu waziri ni kubwa, hali hii inaipa uwezo mkubwa serikali na hivyo serikali kusimamia na kuongoza Bunge na si Bunge kuongoza serikali, ndiyo maana kauli za sasa za wabunge ni 'tunaiomba serikali' na si 'tunaiagiza serikali' kufanya mambo kadhaa," alisema na kuongeza:
"Dalili hizi zinaonyesha kuwa sasa serikali ndiyo inasimamia Bunge na si wabunge kuisimamia serikali, tunahitaji pia kutazama aina ya wabunge na tujadili namna ambavyo uteuzi unaweza kufanyika."
Alisema ili kuboresha hali hiyo, ipo haja ya kufikia hatua ya kuwa na mawaziri ambao si wabunge, ili kutoa nafasi ya kuwa na Bunge huru, ambalo litakuwa na mamlaka kamili ya kuwakilisha mawazo ya wananchi na kuiwajibisha serikali.
Warioba alisema hata utaratibu wa muundo wa wabunge wa aina tatu, wakiwamo wa kuchaguliwa moja kwa moja kutoka majimboni mwao, wanaochaguliwa kwa viti maalum (wanawake) na wanaoteliwa na Rais, unaweka matabaka miongoni mwao.
"Utaratibu huu kikatiba unawagawanya, katiba inaeleza kuwa huwezi kuwa Waziri Mkuu kama si mbunge wa kuchaguliwa kutoka jimboni, hivyo kama umeteuliwa huna hadhi ya kuwa Waziri Mkuu hata kama una uwezo mzuri kiasi gani, huwezi kusema tuko sawa kisha viongozi wako ambao ni wabunge unawaweka katika matabaka, hawa wana hadhi ya juu hawa hadhi ya chini, hili si sahihi," alisema.
Aliongeza kuwa ipo haja ya kuangalia kwa makini utaratibu wa kuwatafuta wabunge katika njia iliyo sawa ili kuondoa tofauti zilizopo kikatiba na kuwafanya wote kupewa hadhi sawa katika macho ya Watanzania.
Akizungumzia suala la mahakama, Warioba alisema mhimili wa mahakama umekuwa haupewi umuhimu wa kutosha kikatiba, pamoja na kufanyiwa mabadiliko kutoka Idara hadi kuwa Mhimili wa Dola katika nchi, hivyo kuifanya kuendelea kuwa dhaifu.
Alisema wakati Mhimili wa Bunge ukiwa unapewa umuhimu, ikiwemo majengo na mazingira mazuri ya kufanyia kazi, mahakama imekuwa ikitengewa kiasi kidogo kabisa cha fedha na kuinyima madaraka na kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu, ikiwamo majengo.
"Wakati Bunge limepewa mamlaka ya kutosha, lakini unaweza kuona mpaka sasa Mahakama ya Rufaa haijajengewa jengo, haipo kwenye kipaumbele, suala la fedha na uwezo wa miundombinu inategemea fadhila au hiyari ya Hazina, sasa ni lazima tufike mahali katiba itoe mamlaka kisheria katika kuhakikisha miundombinu ya mahakama inaboreshwa," alisisitiza.
Alikitaja kipengele kingine kinachotakiwa kufanyiwa marekebisho ni juu ya mamlaka ya Rais katika suala la uteuzi wa nafasi mbalimbali, ikiwamo kumteua Waziri Mkuu na kumtaka kuwa lazima athibitishwe na wabunge huku ikiacha nafasi ya uteuzi wa mawaziri wengine mikononi mwake.
"Mabadiliko ya mwaka 1984 yalipunguza kwa kiasi madaraka makubwa aliyokuwa nayo Rais katika uteuzi, lakini bado kuna haja ya kuangalia madaraka ya uteuzi wa Rais kwa upande wa kisiasa, hata ikibidi mawaziri wengine ni lazima wathibitishwe na Bunge ili kuondoa uwezekano wa kuteuana kirafiki, hii inaweza kutuletea shida iwapo tutapata kiongozi asiyezingatia misingi ya uongozi bora," alisema.
Aliongeza kuwa kipengele kinachozungumzia juu ya Ujamaa na Kujitegemea hakina maana tena katika katiba kutokana na kukubali utandawazi, ambapo kutokana na kuzidi kwa matatizo ya kiuchumi kujiunga na taasisi za fedha za kidunia ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuliondoa uwezo wa kujiamulia mambo ya ndani.
Alisema misaada na mikopo inayotoka katika taasisi hizo na nchi tajiri imekuwa ikitolewa kwa masharti magumu.
Hata hivyo, Warioba alisema umefika wakati wananchi washirikishwe haraka katika kufanya mabadiliko ya katiba, lakini alielezwa wasiwasi wake juu ya hilo kwa kile alichosema ni kutoshirikisha wananchi katika mambo muhimu ikiwemo kusikiliza kero zao.
Alisema viongozi wengi wamekuwa wakisikiliza na kufanya maamuzi kwa kufuata mawazo ya wafadhili ambao kutokana na ufadhili wao, wamekuwa wakiwapa kipaumbele kuliko wananchi.