Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
View: https://www.youtube.com/live/NMGmvwH9P-w
Waziri Kivuli wa TAMISEMI, Kulthum Mchuchuli anazungumza na Waandishi wa Habari, Septemba 25, 2026
Chama cha ACT Wazalendo kimepokea kwa masikitiko makubwa na kinapinga kwa nguvu zote operesheni zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini za kuwaondoa wamachinga na wafanyabiashara wadogo katika maeneo yao ya biashara. Operesheni hizi zinafanywa kwa ukatili mkubwa, ikihusisha kuvunjwa kwa vibanda na meza, uporaji na uharibifu wa bidhaa, kuwavamiwa, kuwapiga na kuwakamata, pamoja na matukio ya kuchomwa kwa masoko.
Tunafahamu kuwa operesheni hizi zinafanywa kwa baraka za Rais Samia. Sote tunakumbuka kuwa tarehe 2 Septemba 2026, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia na kupanga shughuli za wafanyabiashara wadogo. Alisema “Suala la wafanyabiashara wadogo tulikuwa tunalisimamia vizuri, lakini kwa sasa tumepunguza usimamizi hasa kwa majiji ya Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma....”
Tangu kauli hiyo itolewe, tumeshuhudia operesheni mbalimbali zikitekelezwa dhidi ya wamachinga katika miji na majiji mbalimbali nchini. Kwa mfano; Jiji la Dar es Salaam, fukuza fukuza inaendelea katika maeneo ya Tandika, Buguruni, Gongo la Mboto, Ilala Boma, Kigamboni, Tegeta, Msasani, Mbagala na Halmashauri ya Ubungo imetangaza operesheni ya kuwaondoa machinga kuanzia tarehe 29 Septemba 2026.
Kwa upande wa Mkoa wa Mwanza, tumeshuhudia wamachinga wakiondolewa katika maeneo ya Nyamagana na Ilemela, huku uongozi wa Serikali ukiwataka wamachinga kuhamia maeneo mengine. Maagizo hayo yameendelea kutekelezwa katika mikoa ya Tanga, Mbeya, Kilimanjaro na sehemu nyingine nyingi nchini.
Aidha, mbali na kuvunjwa kwa vibanda, meza, na mikokoteni, masoko ya wamachinga yamekuwa yakikabiliwa na mfululizo wa moto. Miongoni mwa matukio ya hivi karibuni, ni tukio la moto ulioteketeza zaidi ya vibanda 50 Machinga Complex Dodoma (20 Septemba 2026), pamoja na moto katika masoko ya Marangu (Moshi) na Mbao Sabasaba (Mwanza).
Ndugu wanahabari, hii ni mara ya pili operesheni hizi zikifanyika chini ya utawala wa Rais Samia na kuleta madhila makubwa. Mfumo huu ulianza tarehe 13 Septemba 2021 baada ya agizo la kwanza la Rais Samia akiwa Chamwino. Agizo hilo lilifuatiwa na kuvunjwa kwa zaidi ya vibanda 120 Vingunguti, kuondolewa kwa nguvu wamachinga wa Makoroboi (Mwanza) na Morogoro, pamoja na mfululizo wa moto katika masoko ya Kariakoo, Karume (ulioungua mara mbili), Ukwaju (Mwanza), Mashine Tatu (Iringa), na Kawe.
Katika matukio yote haya, yanaacha maumivu, hasara, unyanayasji, upotevu wa mitaji na wakati wengine hata msongo wa mawazao kwa wamachinga, Serikali haijawahi kutoa ripoti ya wazi kuhusu chanzo cha moto, hasara iliyopatikana, wala kuwafikisha mahakamani watuhumiwa. Badala yake, imekuwa ikitumia njama hizo za moto kuongeza kasi ya kuwahamisha, huku ikijidai kutenga fedha kujenga au kuboresha masoko bila kuwashirikisha waathirika. Kitendo hiki kinashiria kuwa majanga haya yanachochewa na mipango ya Serikali; kwani kama sivyo, ingekuwa imeshatoa majibu ya wazi na kuchukua hatua stahiki..
Ndg. Wanahabari
Mara zote Serikali inapotaka kuwaondoa wamachinga, imekuwa ikitumia hoja mbalimbali kuhalalisha hatua hizo. Miongoni mwa hoja hizo ni madai kwamba machinga wanafanya biashara katika maeneo hatarishi, wanachafua miji, wanazuia shughuli za wafanyabiashara wenye maduka, hawalipi kodi, wanasababisha msongamano na wanakiuka mipango ya miji.
ACT Wazalendo tunaona kuwa hoja hizi mara nyingi hutumiwa kama kisingizio cha kuhalalisha kuwaondoa machinga badala ya kushughulikia kwa kina chanzo cha matatizo hayo. Kwa mtazamo wetu, pale ambapo kuna changamoto ya usafi, usalama, msongamano au matumizi ya maeneo ya umma, Serikali inapaswa kutafuta suluhisho linalowezesha wafanyabiashara wadogo kuendelea na shughuli zao kwa kufuata utaratibu, badala ya kutumia nguvu na kuwaondoa katika maeneo yenye wateja.
Aidha, madai kwamba machinga hawalipi kodi yanapaswa kutazamwa kwa uhalisia wa mfumo wa biashara ndogo na taratibu zilizowekwa na Serikali yenyewe. Badala ya kuwatangaza wafanyabiashara hawa kama tatizo, Serikali inapaswa kuweka mfumo rahisi wa kuwatambua, kuwasajili na kuwawezesha kutekeleza wajibu wao wa kisheria bila kuwaongezea mzigo usio wa lazima.
ACT Wazalendo inasisitiza, hoja ya kupanga miji haipaswi kutumiwa kama hila au njama ya kuwaondoa wafanyabiashara wadogo katika maeneo yao ya biashara bila kuwapatia maeneo mbadala yenye wateja na mazingira yanayowezesha biashara zao kuendelea. Upangaji wa miji unaopuuza uhalisia wa maisha ya watu wanaotegemea biashara ndogo unaweza kuongeza umaskini na ukosefu wa ajira.
Tunasisitiza kwamba machinga si uchafu, wala si adui wa wafanyabiashara wenye maduka. Wao ni sehemu ya uchumi wa mijini na wanapaswa kutazamwa kama wananchi wanaotafuta riziki. Changamoto zinazohusishwa na biashara zao zinapaswa kutatuliwa kwa majadiliano, mipango shirikishi na kanuni za utu, badala ya operesheni za kuwaondoa na kuharibu mitaji yao.
Vilevile, ukweli mchungu ni kwamba wimbi kubwa la machinga linatokana na mfumo wa uchumi wa Serikali za CCM ambao umeshindwa kuzalisha ajira za kutosha, umeongeza pengo la kipato na kusababisha vijana wengi kukimbilia mijini kutafuta riziki. Sera hizo kama vile; uporaji mkubwa wa ardhi katika maeneo mbalimbali, kuuawa kwa viwanda mbalimbali nchini, kukithiri uwekeza uchwara unaotoa ajira chache, kupuuzwa kwa kilimo na serikali, na ongezeko la uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Hali hii imewachochea wengi kujiajiri kupitia umachinga, bodaboda, mama lishe, ufundi na biashara ndogo ndogo.
Kwa hiyo, badala ya kuwaondoa machinga, Serikali inapaswa kushughulikia chanzo cha tatizo kwa kubadili sera za uchumi, kuongeza ajira na kuweka mazingira bora ya uzalishaji na biashara ndogo.
Hata Hayati Mzee Benjamin Mkapa aliwahi kueleza namna sera za uchumi na ubinafsishaji zilivyochangia kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na watu kujikita katika uchuuzi. Katika mahojiano yake jarida la Business Mirror mwaka 2009, alisema:
“Tulibinafsisha kila kitu kilichokuwa mikononi mwa dola. Kila kitu kilinunuliwa na wawekezaji kutoka nje kwa sababu hatukuwa na mtaji wa ndani wenye uwezo wa kushindana. Makampuni ya nje yakafunga mashirika ya ndani kwa sababu hayakuwa na tija na yakayageuza mashirika haya kuwa wachuuzi wa bidhaa kutoka nje na kwa hivyo kuongeza watu wasio na ajira. Wataalam wa Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha walitabiri kwamba hivyo ndivyo ingekuwa, lakini wakatuambia: Uwekezaji kutoka nje utazaa taasisi za kibiashara za kisasa, zenye uwezo wa kushindana, na teknolojia ya kisasa, na kwa hivyo kujenga misingi ya kudumu ya maendeleo ya kisasa. Hakuna lolote kati ya hayo lililotokea nchini mwetu.”
Hata hivyo, Serikali ya CCM imeendelea kutekeleza sera hizo hizo za uchumi ambazo zinazaa wachuuzi na ukosefu mkubwa wa ajira.
ACT Wazalendo tunatambua kuwa CCM imeshindwa kuendesha uchumi wa nchi hii, imezalisha wimbi kubwa la ukosefu wa ajira na matabaka makubwa ya kipato. Na haiwezi kabisa kubadilika, hairekebishiki. Mara zote imejitokeza kuwa kinyume na upande wa wananchi wa kipato cha chini. Njia pekee wanayoitumia ni kuwaondoa wananchi kwenye biashara zao, kuchoma masoko yao au kutumia mitutu ya bunduki kuwaangamiza kama ilivyotokea Oktoba 29, 2026.
Ndugu wana Habari, msimamo wa ACT Wazalendo kuhusu suala la wamachinga upo wazi, ni kuwa lazima kujenga miji ya wote kwa maslahi ya wote. Yaani miji itakayowezesha kukuza na kuimarisha ustawi wa watu kwa kuruhusu shughuli za uzalishaji na huduma ili watu waweze kujipatia kipato chao. Wafanyabishara wadogo nao ni sehemu ya jamii ya mijini hawapaswi kunyanyaswa na kubughudhiwa kila uchao. Masuala ya fukuza fukuza ya wamachinga ni kufikiri kizamani bila kujali aina ya uchumi tulionao ambao huzaa wamachinga wengi.
Inachofanya Serikali ya Rais Samia si kuwapanga wamachinga, bali ni kuharibu biashara zao, kuwapora mitaji yao na kuwafukarisha na Matendo haya ya Serikali ya Rais Samia hayaathiri tu machinga, bali yanaathiri mamilioni ya familia zinazowategemea.
Kwasababu hiyo, tunaitaka Serikali ichukue hatua zifuatazo;
- Mosi, isitishe mara moja kinachoitwa kuwapanga wamachinga na badala yake kwa sasa ikae nao ili kuwasikiliza na kuhakikisha wanafanya kazi zao katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu, ambapo ndipo yalipo masoko yao ya asili.
- Pili, Serikali itangaze marufuku ya matumizi ya askari na migambo ya jiji katika kuvunja na kupora mitaji ya machinga, kuvunja meza na kuharibu sehemu zao za biashara. Hili si jambo la kijeshi, ni jambo la kijamii na linapaswa kushughulikiwa kiraia na maafisa wa maendeleo pamoja na maafisa biashara.
- Tatu, Bunge liunde kamati kupitia Kamati ya kudumu ya serikali za mitaa kuchunguza matukio yote ya kuungua kwa masoko nchini na hatua zichukuliwe maramoja.
- Nne, Serikali ianzishe utaratibu wa masoko ya jioni katika miji na majiji yote nchini ili kuruhusu machinga kufanya kazi zao na kuwafikia wateja wao.
- Nne, Serikali itunge sheria na taratibu rasmi zitakazowapa machinga hadhi na kuwalinda kisheria katika shughuli zao za kila siku. Mamlaka ya Mapato na Halmashauri za miji na majiji ziweke taratibu rafiki za kisheria za kuwatambua na kuwalinda katika shughuli zao.
Hivyo, mamilioni ya wamachinga wanapaswa kuungana na kushikamana katika makabiliano na adui huyu, ambaye anaweza kuwachomea biashara, kuwafukuza au kuamuru matumizi ya risasi watakapodai haki zao. ACT Wazalendo tunaendelea kufuatilia kwa karibu matendo haya na tutachukua hatua zaidi.
Imetolewa na;
Ndg. Kulthumu Jumanne Mchuchuli,
Waziri kivuli TAMISEMI na Maendeleo Vijijini.
ACT Wazalendo
25 Septemba 2026.