MCHAKATO KATIBA MPYA
Tusipoujadili muungano kwa makini, utavunjika II
Joseph Mihangwa
Toleo la 253
8 Aug 2012
Kelele za Zanzibar kama za Eritrea
KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya toleo lililopita, tuliona jinsi Muungano wowote wa nchi uliofikiwa bila ridhaa ya wananchi unavyoweza kuvunjika kwa urahisi, ukiwamo Muungano kati ya Uingereza na Ireland Kaskazini ambao Muungano wa Tanzania umenakili na kuiga mengi, ulivyoanza kuyumba.
Tuliona pia dalili zinazoashiria kuvunjika kwa Muungano wetu, zikiwamo, kukosekana nahodha makini wa kuendesha meli ya Muungano iweze kuvuka salama bahari iliyochafuka; kuanzishwa kwa Muungano wa kitaifa wa Wazanzibari ambao umefufua umoja wao wa kitaifa na kudai kurejeshewa hadhi yao kama nchi; na kuvunjika kwa mihimili mitatu iliyoshikilia Muungano, ambayo ni Rais dikteta asiyeambilika (imperial presidency), mfumo wa Chama kimoja, Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Kabla hatujaichambua kwa kina athari ya kuvunjika kwa mihimili hii mitatu, tuangalie kifananisho cha Muungano wa Ethiopia Eritrea ulivyovunjika kwa sababu, kama ilivyokuwa Eritrea kwa Ethiopia, ndivyo ilivyo Zanzibar kwa Tanzania. Eritrea ilijitoa kwenye Muungano kati yake na Ethiopia na kuwa nchi huru mwaka 1993.
Harakati za Zanzibar kujitoa kwenye Muungano, kama zilivyokuwa harakati za Eritrea kujitoa kwenye Muungano kati yake na Ethiopia kunatishia na kujenga hofu kwa Watanzania juu ya hatima ya Muungano, hasa baada ya kuundwa kwa Serikali ya Kitaifa (SUK) kwamba sasa hofu hiyo na yenye kuogofya ni dhahiri na yenye kuzua hofu.
Kwa mfano, nani alitarajia kabla ya hapo, kwamba siku moja Zanzibar itakuwa na bendera yake ya Taifa, Wimbo wake wa Taifa, Ngao ya Taifa, Jeshi la Taifa, Katiba yake yenye kulinda ukuu wa nchi na maslahi ya Wazanzibari bila kuingiliwa na Katiba wala taasisi yoyote ya Muungano?
Nani alitarajia siku moja Zanzibar itazuia rasilimali zake kutumika kwenye Serikali ya Muungano kama mafuta, ardhi na bahari, ila kwa matumizi na maslahi ya Wazanzibari pekee?
Nani alitarajia kwamba Zanzibar ingeweza kujiunga na Shirikisho la Mpira la Bara la Afrika (CAF) kama nchi nje ya Muungano wa Tanzania na sasa inataka ijiunge na Shirikisho/Jumuiya ya Afrika Mashariki kama nchi?
Yote haya yanatia hofu na kuogofya juu ya hatima ya Muungano, kama tu hatutarejea upya Mkataba wa Muungano kuona wapi unavunjwa na yapi wanayofanya ni sahihi tuwaachie waendelee, badala ya kuendeleza udikteta wa kizamani kuzima hoja sahihi. Kuna dhambi gani wananchi kupewa Mkataba wa Muungano wakasoma na kujiridhisha na yaliyokusudiwa kwenye Muungano huo?
Hofu hii juu ya SUK inaweza kufananishwa na hofu kama iliyozua Eritrea kwa Serikali ya Muungano wa Ethiopia Eritrea, pale Eritrea alipoanzisha harakati halali kutaka kujinasua kutoka kwenye Muungano huo, uliodumu tu kwa udikteta wa Mfalme Haile Selassie kama nahodha wa Muungano, na alipoondolewa madarakani, meli ya Muungano iliyumba na kuzama kwa nguvu ya tufani.
Na ndivyo ulivyo Muungano wetu, baada ya kuondoka madarakani kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyeshika hatamu zote za Muungano na kuuendesha kwa staili ya mpanda Farasi.
Zanzibar kama Eritrea kwenye Muungano
Eritrea ilitawaliwa na Wataliano kwa miaka 50 hadi 1941 waliposhindwa vita na Waingereza. Baada ya ushindi huo, Uingereza iliruhusu nchi hiyo kujitawala kama nchi huru chini ya usimamizi wake. Hapo vyama vya siasa na vya Wafanyakazi vikaanzishwa, pamoja na vyombo vya habari huru kwa ajili ya elimu kwa umma.
Mwaka 1952, wakati hatima ya Eritrea ilipojadiliwa kwenye Umoja wa Mataifa, Ethiopia ilitaka ipewe nchi hiyo kwa madai kwamba, kihistoria ilikuwa ni sehemu ya ufalme wa Ethiopia. Hapo kukatokea mzozo.
Wakati nchi jirani za Kiarabu zilitaka Eritrea iwe Taifa huru, Waeritrea wenyewe, ambao idadi yao wakati huo ilifikia 3,000,000, waligawanyika; nusu yao ambao ni wa madhehebu ya Kikristo, na wa kabila la Tigraya waishio maeneo ya milimani karibu na Mji Mkuu, Asmara, waliunga mkono Muungano na Ethiopia.
Kwa upande wa pili, nusu ya Waeritrea ambao ni Waislamu, wanaoishi sehemu za jangwa karibu na Bahari ya Sham na bonde la Magharibi, walitaka Eritrea ipewe uhuru.
Mwafaka ukafikiwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, wa kuunda Shirikisho la Ethiopia na Eritrea ambapo Serikali ya Ethiopia ilipewa kusimamia mambo ya Nje, Ulinzi, Fedha, Biashara, Bandari na Forodha.
Chini ya Muungano huu, ambao muundo wake unafanana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Eritrea, kama ilivyo kwa Zanzibar, iliruhusiwa kuwa na Serikali yake na Bunge huru kusimamia mambo yake. Tena, kama ilivyo Zanzibar ndani ya Muungano, iliruhusiwa kuwa na bendera yake, lugha zake za Taifa, ambazo ni Kitigrinya na Kiarabu.
Tangu mwanzo, Mtawala wa Ethiopia, Mfalme Haile Selasie, aliuona Muungano huo, kama ambavyo Rais Julius K. Nyerere alivyouona Muungano wa Tanzania, kuwa ni hatua ya mwanzo tu kuelekea Muungano kamili kwa kuunda nchi moja.
Kero na kelele juu ya Muungano zilianza kusikika pale Watawala wa Ki-ethiopia, kwa ubaguzi na kujuana, wakisaidiwa na wanasiasa Wakristo wa Kitigraya, walipoanza kuvuka mipaka ya mambo yaliyokubaliwa chini ya Mkataba wa Muungano, kwa kuongeza mambo kwa njia ya shinikizo, vitisho na udhibiti kwa Waeritrea.
Kwa njia hii, uhuru ambao Waeritrea walifurahia kwa muda baada ya ukoloni wa Kitaliano (na kabla ya Muungano), kama vile haki za kisiasa, vyama vya wafanyakazi na uhuru wa vyombo vya habari, vilidhibitiwa. Hapo tena, kelele juu ya Ethiopia kutaka kuimeza Eritrea, kama ambavyo Wazanzibari wanalalamikia kutaka kumezwa na Tanganyika, ikazua moja ya kero za Muungano.
Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa Aprili 26, 1964, ulibainisha mambo kumi na moja tu ya Muungano, baadhi yakiwa ni yale yale yaliyokuwa chini ya Muungano wa Ethiopia na Eritrea, tuliyoyaeleza hapo mwanzo.
Na kama ilivyokuwa kwa Ethiopia/Eritrea, Serikali ya Zanzibar iliachwa kusimamia mambo yote yasiyo ya Muungano, na vivyo hivyo kwa Serikali ya Tanganyika.
Lakini kama ilivyokuwa kwa Ethiopia/Eritrea, kadri Muungano wa Tanzania ulivyopiga hatua mbele, mambo ya Muungano yalizidi kuongezwa kwa njia ya Amri za Rais (Decrees) kinyume na matakwa ya Mkataba wa Muungano, na kufikia 23.
Katiba ya muda ya 1965 (ibara ya 12), ilimpa Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya utendaji kwa mambo yote (11) ya Muungano na kwa Tanganyika; kwa maana kwamba, Rais wa Muungano alikuwa sasa ndiye Rais wa Muungano na hapo hapo Rais wa Tanganyika.
Vivyo hivyo, ibara ya 49 ya Katiba hiyo, ilitoa mamlaka ya kutunga sheria kuhusu mambo ya Muungano na kwa ajili ya Tanganyika, kwa Bunge la Muungano. Ndiyo kusema kwamba, Bunge hilo la Muungano sasa lilikuwa ndilo Bunge la Tanganyika pia.
Mwaka 1967, Bunge lilitunga Sheria Na 24 ya 1967, iliyompa Rais wa Muungano na Rais wa Tanganyika uwezo wa kupachika jina Tanzania katika sheria zote popote pale jina Tanganyika liliposomeka hivyo.
Hii ilimaanisha kwamba, Tanganyika sasa ndiyo iliyogeuka kuwa Tanzania, na Tanzania ndiyo Tanganyika, lakini Zanzibar ikabakia kama Zanzibar.
Ni kwa misingi hii kwamba, Sheria ya Tafsiri za Vifungu vya Sheria (Interpretation of Laws and General Cluses Act), Namba 30 ya 1972 (kifungu cha 3), iliweza kutafsiri neno Jamhuri kumaanisha Jamhuri ya Tanganyika, inayojumuisha Jamhuri ya Muungano.
Tanganyika ndiyo Tanzania?
Sheria Namba 24 ya 1967, iliyofuta jina Tanganyika kwenye vitabu vya Sheria; na Sheria Namba 30 ya 1972 iliyotafsiri Jamhuri ya Tanganyika kujumuisha Jamhuri ya Muungano zilitoa tafsiri mbaya na mitazamo potofu kuwafanya Watanganyika kuamini kwamba nchi yao Tanganyika ilipandishwa hadhi kuwa Tanzania, kama mshirika mwandamizi kwa Zanzibar katika Muungano; wakati ukweli Tanganyika na Zanzibar zina hadhi sawa ndani ya Muungano.
Katiba ya kudumu ya 1977 inayotumika sasa ilitibua mambo zaidi na kuongeza utata na mtafaruku kwa Muungano.
Tunafahamu kwamba, Mkataba wa Muungano (ibara ya 5, 6 na 7) kwa Sheria ya Muungano Namba 22 ya 1964 (kifungu 5, 7 na 8) zinatamka bayana kuendelea kuwapo kwa Serikali za Tanganyika na Zanzibar baada ya nchi hizo kuungana kuunda ubia wa mambo kumi na moja ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa maana ya kuwapo Serikali tatu: Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.
Kwa mfano, ibara ya tano ya Mkataba huo inasema: Sheria za sasa za Tanganyika na zile za Zanzibar, zitaendelea kuwa na nguvu katika maeneo (territories) ya nchi hizo.
Na kifungu cha 8 (1) cha Sheria ya Muungano kinasema:
.. Kuanzia siku ya Muungano na baada ya hapo na kuendelea, Sheria za Tanganyika na za Zanzibar zitaendelea kuwa Sheria za nchi za Tanganyika na Zanzibar
.. na hazitaathirika au kuathiriwa kwa namna yoyote ile kwa kukoma kutumika kwa Katiba ya Tanganyika kwa Serikali ya Tanganyika kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano inayojiongoza na kujitawala
...
Tofauti na Mkataba wa Muungano; pia tofauti na Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya 1965, iliyotambua kuwapo kwa Serikali za Tanganyika na Zanzibar, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 inayoendelea kutumika sasa haiundi au kutambua kuwepo kwa Tanganyika; wala haimpi mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano, au mtu au watu wowote wale, kuitawala Tanganyika kwa mambo yasiyo ya Muungano.
Hapa, upungufu huu unazua dhana potofu kuwa, Tanzania ndiyo Tanganyika, na Tanganyika ndiyo Tanzania; na kwa sababu hiyo kwamba hapana haja ya kuwa na Serikali zaidi ya moja kwa Tanzania nzima!.
Vivyo hivyo, kama ambavyo uhuru na uwapo wa vyama vya siasa na vya wafanyakazi ulipigwa marufuku kwa AMRI ya Mtawala wa Ethiopia nchini Eritrea (1959), na bendera ya nchi hiyo kufutwa (1958); ndivyo vivyo hivyo mwaka 1977 hapa kwetu, Chama cha ASP kiliunganishwa na Chama cha Tanganyika National Union (TANU), kuunda Chama cha Mapinduzi CCM, kama moja ya mikakati ya kuimarisha Muungano, wakati ukweli mambo ya Vyama vya siasa si moja au sehemu ya mambo chini Mkataba wa Muungano, wala sehemu ya Sheria za Muungano (Acts of Union) kwa utekelezaji.
Kelele za Wazanzibari kama za Waeritrea
Ni kwamba, kelele za Eritrea, kama zilivyo kelele za Zanzibar juu ya kero za Muungano, hazikuwa za uongo, kwani ubabe wa Ethiopia (kaka mkuu ndani ya Muungano, kama ilivyo Tanganyika) ulianza kujionyesha dhahiri kwa kushinikiza mambo yasiyo ya Muungano.
Kwa mfano, mwaka 1958, bendera ya Eritrea ilifutwa; ambapo mwaka 1959, Sheria za Ethiopia zilishinikizwa pia kutumika Eritrea; vyama vya siasa na vya Wafanyakazi navyo vikapigwa marufuku.
Ubabe huu ulikwenda mbali zaidi kwa kudhibiti habari na vyombo vya habari, lugha za Taifa za Kitigranya na Kiarabu zikapigwa marufuku, na nafasi yake kuchukuliwa na lugha ya Kiethiopia ya Amhari, kama lugha ya Taifa.
Kana kwamba hayo yalikuwa hayatoshi, mwaka 1962, Bunge la Eritrea lilishinikizwa kukubali kufutwa kwa Shirikisho, na Bunge hilo kulazimishwa kujifuta lenyewe ili Eritrea imezwe na Ethiopia. Kuanzia hapo, Eritrea ilihesabiwa na kupewa hadhi duni kama moja tu ya majimbo 13 ya Ethiopia.
Kwa miaka yote ya 1960, Serikali ya Haile Selasie ilikabaliwa na maasi pande zote. Kwa mfano, maasi ya Wa-Oromo katika Jimbo la Bale upande wa Kusini, yalidumu kwa miaka sita; nao Wasomali waasi wa Ogaden, waliunda Chama chao cha Ukombozi The West Somali Liberation Front (WSLF) kuwafukuza Waethiopia Ogaden ili kurudisha Serikali ya Kisomali.
Huko Eritrea, vikundi vya wapiganaji wa msituni vilianzisha vita ya ukombozi ambapo Serikali ya Selasie ilitumia silaha nzito na ukatili mkubwa kujaribu kuizima. Ukatili huu ulidhalilisha utaifa wa Waeritrea, wakaapa kutorudi nyuma hadi uhuru upatikane.
Septemba 12, 1974, Mfalme Haile Selasie, alipinduliwa na Kanali Mengistu Haile Mariam, ambaye naye hakuweza kuzima vita ya ukombozi ya Wa-eritrea. Si hivyo tu, itikadi na sera zake za Ki-karl Marx/Ki-Lenin, zilimletea maasi mengine ya ndani na juu ya vita ya Eritrea, kufuatia zoezi lake la utaifishaji wa njia kuu za uchumi kwa kasi ya kutisha; kuanzia na Makampuni ya Bima na Mabenki (Januari 1975), Viwanda vikubwa na Makampuni ya biashara (Februari 1975), ambapo Machi 1975, alitaifisha ardhi yote na hivyo kuharibu kabisa nguvu za kiuchumi za utawala uliopita na masalia yake.
Kwa mfano, katika jimbo la Tigray, waasi waliunda Jeshi la ukombozi la Tigray Peoples Liberation Front (TPLF) kwa msaada wa Wa-eritria.
Na huko Ethiopia ya Kusini, Wa-Oromo walikuwa na Jeshi la Oromo Liberation Front (OLF) likiungwa mkono na Wasomali, ambao nao walifufua Jeshi lao la ukombozi The Western Somali Liberation Front (WSLF) ili kurejesha ardhi yao iliyopotea.
Hatimaye, Mei 1991, Kanali Mengistu Haile Mariam alizidiwa nguvu na muungano wa Majeshi ya waasi wa Eritrea na Tigray na kukimbilia uhamishoni.
Matokeo ya kura ya maoni iliyoitishwa Julai 1991 chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, kujadili hatima ya Eritrea, yaliwezesha Eritrea kurejeshewa uhuru kamili mwaka 1993, na hivyo kufunga ukurasa wa miaka 30 ya Vita kwa nchi hiyo.
Hatuwezi kuyapuuza malalamiko ya Wazanzibari juu ya uendeshaji wa Muungano wetu wenye kuzua kero. Kama ambavyo Serikali ya Ethiopia ilivyoutumia utengano wa Waeritrea milioni tatu kushinikiza mambo yake yasiyo ya Muungano, na hatimaye Eritrea kumezwa ndani ya Ethiopia; ndivyo nasi tulivyo na kila sababu ya kuhofu juu ya SUK, iwapo Wazanzibari wataungana na baadaye kutaka tafsiri sahihi ya Muundo wa Muungano wetu, ambao kwa muda mrefu, kero zake zimekosa utashi wa kuzitafutia ufumbuzi.
Na ingawa SUK haiwezi kuzua mtafaruku mkubwa kwa sasa kwa Muungano wetu kama ilivyokuwa kwa Ethiopia na Eritrea, lakini lazima tujiandae kwa mazingira mapya Visiwani chini ya SUK, ambayo kwa vyovyote vile, yatagusa mustakabali wa Muungano
Tusikubali kwenda serikali tatu. Kwa vile tumekatazwa kutaka kuvunja Muungano - japo waliotukataza hawana uwezo huo - na kwamba tunaweza kujadili "muundo" bora wa Muungano. Ninawasihi watu wa bara kudai "Serikali moja, taifa moja, na nchi moja". Haya mambo ya serikali mbili nchi mbili au serikali tatu nchi mbili hayaingii kichwani na ni jitihada za kujaribu kuibeba Zanzibar. Wakati umefika tudai uwepo wa serikali moja tu ya kitafa kwenye nchi moja.
Ninafahamu kabisa matokeo ya watu wa bara kutaka hili. Jambo pekee ambalo tusikubali kuuziwa (CCM na upiinzani wanataka hili) ni serikali tatu. Serikali tatu ni mzigo ambao hatuwezi kuubeba na wala hatupaswi kuubeba. Nawasihi wenzangu tukate kuongezewa mizigo. Tuwe na serikali moja, taifa moja na nchi moja. Sasa kama hili lina maana Zanzibar iwe "serikali moja, taifa moja na nchi moja" na bara iwe "serikali moja, taifa moja na nchi moja" basi na iwe.
Tuwasaidie Zanzibar watoke kwenye Muungano kama hawataki serikali moja kwani mbili hawataki na tatu tutajipa mzigo zaidi!
SAY NO TO SERIKALI TATU!!
Iambie tume ya Warioba - hatutaki serikali tatu!!