Mabadiliko ya katiba Zanzibar yaidhinishwa
Saturday, 04 September 2010 20:18
Salma Said, Zanzibar
SHERIA namba 9 ya mwaka 2010 ya marekebisho ya 10 ya katiba ya Zanzibar ya 1984 ambayo inaitambua Zanzibar kuwa ni nchi na muundo mpya wa serikali ya umoja wa kitaifa imetiwa saini rasmi na Rais Amani Abeid Karume.
Sheria hiyo imetungwa baada asilimia 66.4 ya ya kura za maoni zilizopigwa Julai 31 mwaka huu kukubali mfumo mpya wa muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar baada ya uchaguzi ujao.
Habari ambazo zimelifikia Mwananchi Jumapili jana zimeeleza kwamba Rais Karume alisaini sheria hiyo Agosti 13, 2010 mwaka huu.
Kutokana na idhinisho hilo, sasa kipengele cha katiba kilichokuwa kinaeleza kwamba Zanzibar ni sehemu ya Tanzania, sasa kitasomeka: Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Marekebisho hayo ya 10 ambayo yamefunua mjadala mkali miongoni mwa wataalamu wa sheria nchini pia imempa mamlaka rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengine kwa kufuata utaratibu uliwekwa na sheria iliyotungwa na baraza la wawakilishi bila ya kuzingatia sheria nyengine.
Vile vile kabla ya marekebisho haya ya 10 rais wa Zanzibar alipaswa kushauriana na rais wa Jamhuri ya Muungano kabla ya kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengine kufuata utaratibu uliowekwa.
Gazeti hili limefanikiwa kupata nakala ya sheria hiyo ambayo pia inaainisha katika kifungu cha 39 (1) (2) kuwa kutakuwa na rais wa Zanzibar na makamu wawili wa rais ambao watajulikana kama makamu wa kwanza wa rais na makamu wa pili wa rais.
Makamu hao wa rais, wanaelezewa kuwa watatakiwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo ndani ya siku saba mara baada ya rais kushika madaraka.
Kwa mujibu wa sheria hiyo makamu wa kwanza wa rais atateuliwa na rais baada ya kushauriana na chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa rais.
Hata hivyo endapo ndani ya siku saba baada ya rais kushika madaraka, chama kinachostahili kutoa makamu wa kwanza wa rais kitashindwa kuwasilisha kwa rais jina la uteuzi wa makamu wa kwanza wa rais, basi rais ataacha wazi nafasi hiyo.
Makamu wa kwanza wa rais, kwa mujibu wa sheria, atakuwa ni mshauri mkuu wa rais na atatekeleza kazi zote atakazopangiwa na rais.
Nafasi ya makamu wa pili wa rais itatolewa kwa mtu ambaye atatoka chama kilichotoa rais na itakuwa imechukua nafasi ya waziri kiongozi.
source:
Mabadiliko ya katiba Zanzibar yaidhinishwa
NIONAVYO MIMI:
Tuache kulazimisha visivyowezekana, ni wakati muafaka sasa wa serikali tatu, maadam serikali ya Zanzibar sasa ina nguvu zaidi, iwepo ya Tanganyika, na pia ya Muungano...