Kero za Muungano zitakwisha lini?
Salim Said Salim
MUUNGANO wa Tanganyika na Zanzibar uliozaliwa Aprili 24, 1964, leo umetimiza miaka 45.
Kuundwa kwake kulikuwa siri na tangazo la kutiwa saini mkataba wa Muungano kati ya Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, liliwashangaza watu wa Bara na Visiwani. Hii ilitokana na habari hizi kuwa za siri na watu wa pande hizi mbili za Muungano kutoshauriwa, kama vile hawakuwa na haki hio.
Hakuna aliyethubutu kuuliza ilikuwaje kwa vile kutoa mawazo au kuikosoa serikali wakati ule ilikuwa sawa na uhaini. Siku hizi lugha imelainishwa na mtu wa aina hio huitwa ‘si mwenzetu'.
Kumbukumbu zinaonyesha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Wolfango Dourado, na waliokuwa mawaziri katika serikali ya Rais Amani Abeid Karume wameeleza mara nyingi kuwa hapakuwa katika kikao kilichozungumzia suala hili.
Dourado aliwekwa kizuizini wakati wa utawala wa Rais wa Kwanza wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere, kwa kusema hakushauriwa Muungano ulipoundwa na kudai haukuwa halali. Lakini hakusema kama ulikuwa haramu!
Siku ile, Aprili 26, 1964 saa 10 jioni, nikiwa kijana wa miaka 18, nilikuwa nimekaa kwenye kijiwe kimoja maarufu cha mtaa wa Baraste Kipande, mjini Unguja, nikingojea zamu yangu ifike nicheze dhumna.
Alikuja mwalimu mmoja wa shule, Mohammed Shatry, na kusema kwa mujibu wa taarifa ya habari Zanzibar na Tanganyika zimeungana na mkataba wa Muungano umetiwa saini Dar es Salaam kati ya marais wawili - Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Sheikh Abeid Amani Karume (Zanzibar). Hapakuwa na sherehe za aina yoyote ile.
Siku chache baadaye palikuwa na mkutano wa hadhara na kila pembe alikuwapo askari aliyebeba silaha. Mzee Karume aliwauliza waliohudhuria kama walifurahia kuungana na kutakiwa waseme "ndiyo" na wao walitii amri. Hili neno "ndiyo" lilipendwa sana na Sheikh Karume na hata nyumba yake iliyopo Kisimamajongoo ameipa jina la "Ndiyo". Kama kweli ridhaa ya wananchi ilikuwa ina maana kwa nini isitafutwe kabla ya Muungano?
Muungano ulipoundwa ulikuwa zaidi na sura ya kisiasa na ulikuwa wa mambo 11, ikiwa pamoja na mambo ya ndani na nje. Mambo ya fedha, biashara, kilimo, mafuta, mawasiliano, madini na bahari kuu hayakuwemo katika orodha mambo ya muungano.
Ushirikiano wa kimataifa haukujumuishwa katika orodha asili ya mambo ya Muungano na huenda ndio iliyosababisha Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), kwa vile suala hili halikuwa la muungano, hali iliyoutikisa Muungano na kusababisha mzozo mkubwa.
Baadhi ya watu wa visiwani wanahisi kuingizwa ushirikiano wa kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje kulifanyika, si kwa lengo la kutafuta ufanisi bali kuibana Zanzibar isijiunge na jumuiya za kimataifa.
Nimekutana mara nyingi na mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi wa wakati ule, wakiwamo wawili walionisomesha shule - wote sasa marehemu - na kwa bahati mbaya sijui siku waliyokufa au katika mazingira gani na wapi walizikwa, na waliniambia wameshitukizwa tu na kuundwa kwa muungano.
Siku moja nilipomtembelea ofisini Dares Salaam, Mwalimu Abdulla Kassim Hanga (sasa marehemu ) wakati akiwa waziri anayeshughulikia mambo ya muungano, aliniambia licha ya wakati ule kuwa Waziri Mkuu wa Zanzibar (sasa Waziri Kiongozi) alikuwa hana taarifa ya kuundwa kwa Muungano.
Hanga ambaye alikuwa akipendwa sana Bara na Visiwani kwa vile baadhi ya wakati alikuwa akienda ofisini kwa baiskeli, aliniambia: "Ndiyo mambo".
Hata hivyo, kuundwa kwa Muungano, kama kwa Afro-Shirazi Party (ASP) kuungana na TANU mwaka 1977 na kuzaliwa CCM, kulionekana na baadhi ya watu wakati ule kama faraja, lakini iliyokuwa kama ya kutolewa kwenye chungu cha moto na kuwekwa juani.
Wapo waliofurahia kwa kueleza huo ulikuwa mwisho wa ‘kamatakamata' ya watu iliyokuwa ikiendelea visiwani na hata wengine kuuawa wakiwa wanazungumza katika vijiwe au wakifanya ibada msikitini. Waliofanya hayo walipewa majina kama ‘Mamba', ‘Sancho' na ‘Dracula'.
Muungano huu umepitia misukosuko ya kila aina na dhoruba nyingi, lakini bado unanawiri ijapokuwa kwa mbali, wakati nchi nyingi za Kiafrika, Kiarabu na Asia zilizochukua hatua kama hii miaka ya nyuma zilishindwa kuuendeleza.
Wapo waliokuwa nchi moja na kutengana kama iliyokuwa Rwanda-Burundi sasa ni Rwanda na Burundi, India ilizaa Pakistan na Pakistan ilizaa Bangladesh na nchi nyingine kama Cape Verde na Indonesia zimekuwa na matatizo hayo.
Kwa Watanzania wengi, Bara na Visiwani, inaonekana wazi kuungana si tatizo. Kinacholeta ubishi na mivutano ni masuala gani ni ya Muungano na mambo gani yapo chini ya mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Malalamiko ni juu ya mfumo wa Muungano. Wapo wanaotaka muundo wa serikali mbili uendelee, lakini wapo wanaosema uwe wa serikali moja na wapo wanaopendelea mfumo wa shirikisho wa serikali tatu.
Kinachoshangaza ni kusikia viongozi wa serikali na CCM siku hizi wakisema wanapenda wananchi washirikishwe kutoa maoni yao katika mambo muhimu, kama mapendekezo ya kuunda serikali ya mseto Zanzibar, ili kumaliza mgogoro wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya miaka 15.
Lakini watu hawa hawa, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, hawazungumzii kura ya maoni juu ya Muungano au masuala nyeti ya nchi kama kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wanachoamua wao ndiyo hicho hicho na wengine waitikie "hewala".
Hata kuondolewa kwa matumizi ya hati za usafiri kati ya Bara na Visiwani hapakutakiwa kushirikishwa wananchi. Wapo pia wanaohoji kwa nini Rais wa pili mstaafu wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe, alipoondolewa madarakani hapakutakiwa kura ya maoni ya Wazanzibari?
Wakati Zanzibar na Tanganyika zilipoungana, Rais wa Zanzibar alitakiwa moja kwa moja awe Makamu wa Rais kama Rais atatoka Bara na pale Rais atakapotoka Visiwani mwenzake wa Bara awe Makamu wa Rais. Hili limeondolewa bila ya kura ya maoni.
Si siri kama utawaomba mawaziri wa Serikali ya Muungano na ya Zanbzibar waandikie orodha ya mambo ya Muungano katika karatasi moja na karatasi ya pili yale ambayo chini ya mamlaka ya Zanzibar, kitachotokea ni kichekesho kwa vile hutapata zaidi ya wawili watakaotoa maelezo sawa. Sijui kama Rais Kikwete na Rais Karume wanayo mawazo sawa juu ya mambo gani ni ya Muungano na mambo gani ni ya Zanzibar.
Muungano ulipoundwa ulikuwa na mambo 11, lakini sasa wapo wanaosema ni 29 na wengine hudai yamefikia 50. Kumekuwa na utata juu ya kuongezeka mambo ya Muungano na viongozi wengine wanasema mengi yameongezwa kinyemela.
Ukweli ni kwamba masuala ya Muungano si wazi na yanaamuliwa zaidi kwa maelewano ndani ya CCM kuliko kuheshimu mawazo ya Watanzania. Namna ambavyo mambo mapya yanaweza kuingizwa katika mfumo wa serikali ya Muungano umejaa mazonge.
Katiba haipo wazi kueleza vipi inarekebishwa. Jee ni kwa kupigiwa kura nyingi bungeni na wingi huo ni wa zaidi ya nusu au thuluthi mbili na je, wabunge wote watapiga kura kwa pamoja au wa Bara mbali na wa Visiwani mbali?
Je ,Bunge likisharidhia marekebisho ya katiba Baraza la Wawakilishi la Zanzibar litatakiwa kuridhia au haipo haja hio? Hili halizungumzwi kwa uwazi kama vile ni siri ambayo Watanzania hawana haki ya kuijuwa na bado tunaambiwa serikali zetu zinaendeshwa kwa ukweli na uwazi.
Mara nyingi husikika manung'uniko juu ya Muungano kutoka Visiwani. Ni kawaida nchi moja kubwa na nyingine ndogo zikiungana mdogo ndiye husikika akilalama - baadhi ya wakati bila ya sababu za msingi. Lakini upo wakati palisikika kundi la G55 liliodai bungeni kurudishwa Serikali ya Tanganyika kwa kusema Zanzibar ilikuwa inadekezwa ndani ya Muungano.
Katika kila upande wa Muungano wapo watu wanaodai wenzao wa upande wa pili wanafaidika zaidi kuliko wao. Vigezo wanavyotumia kufikia uamuzi huo wanavijua wenyewe.
Tangu kuundwa kwa Muungano tumeshuhudia wanasiasa wengi, walipokuwa serikalini walikuwa watetezi wakubwa wa Muungano, lakini walipotoka tu kwa sababu mbalimbali wakawa mstari wa mbele kuukataa au kuulalamikia Muungano.
Wengine wakishapewa vyeo, hasa vya kuwa mawaziri, hubadilika haraka kama kinyonga na kusema "Muungano ni mzuri na unafaa kuenziwa". Wengi wa watu hawa wapo Zanzibar na kwa kiasi fulani wamekuwa wakiwakoroga vichwa watu.
Miaka imepita na mengi yamefanyika na kusikika. Leo utasikia hili na kesho jengini kuhusu Muungano na panapotokea mjadala juu ya kero za Muungano viongozi husema wapo mbioni kupata suluhisho la kudumu.
Si siri kuwa Muungano hutumiwa kama karata ya mwisho na baadhi ya watu, hasa wa Zanzibar, kulazimisha jambo wanaloliona linawanufaisha kisiasa kwa kutishia kuvunja Muungano pale wanapoona hoja zao zinawekewa vikwazo ndani ya CCM.
Wanaposakamwa kwa kufanya mambo yasiokubalika katika mfumo wa kidemokrasia, utawasikia tuachieni Zanzibar yetu na nyie mkae na Bara yenu. Lakini wanapobembeleza kura za maoni za Bara utawasikia wanausifu Muungano.
Kinachosikitisha ni kuona baadhi ya wazee, kwa vile walikuwa waasisi wa Muungano, ijapokuwa ulipoundwa hawakushauriwa, wanahisi vijana wa leo hawana haki ya kuuliza lolote isipokuwa kukubali kila kilichoamuliwa na kinachoakubaliwa na wakubwa. Huu sio mwendo mzuri katika dunia ya leo.
Huu ni Muungano wa Watanzania wote na si viongozi na si jambo la busara mambo muhimu ya Muungano kutekwa nyara na wakubwa na wananchi kutokuwa na haki kuyajadili na kuyatolea maamuzi.
Kwa kiwango fulani unaweza kusema suala la Muungano kupata ridhaa ya wananchi kwa sasa halina uzito, lakini kama zipo kelele za kudai haki ya kura ya maoni ambayo serikali ya Rais Kikwete imeanza kuona umuhimu wake basi ifanyike.
Kinacholeta mzozo ni mfumo mzuri wa Muungano na namna shughuli za Muungano zinavyoendeshwa. Rais Kikwete, tofauti na viongozi waliomtangulia, alionyesha dalili za kuchukua hatua kurekebisha kero na malalamiko yaliyopo juu ya Muungano, lakini matokeo yake ni povu la soda na hakuna moja lililonekana kutatuliwa. Badala yake ndiyo balaa kubwa zaidi inazukuja kila kukicha.
Sasa zinasikika kelele kutoka Visiwani kutaka masuala ya uchimbaji na biashara ya mafuta na bahari kuu yatolewe katika orodha ya Muungano. Mamlaka ya Kodi ya Mapato pia inalalamikiwa. Sijui kesho tutasikia malalamiko gani.
Ni vizuri pakachukuliwa hatua za uhakika na si propaganda kumaliza kero za Muungano na watu wa upande mmoja wasihisi wenzao wa upande wa pili wamependelewa. Vile vile ieleweke kuwa kama ilivyokuwa mkubwa hana haki ya kumuonea mdogo na mdogo naye hana haki ya kudeka ili mwenzake mkubwa amuonee imani.
Ukiuangalia juu juu utaona muungano wa Tanzania ni mfano mzuri wa maelewano kwa watu wa Bara la Afrika, lakini chini kwa chini kunafuka moshi ambao ukiachiliwa utakuja kujitokeza moto mkubwa na matokeo yake hayatakuwa mazuri.
Ni vizuri kusikia matatizo ya Muungano yanapigiwa kelele kuliko kukaliwa kimya, kwani kimya kingi huwa na mshindo mkuu na mara nyingi wa hatari.
Si vizuri kuyafumbia macho masuala ya Muungano, kwani kuficha au kudharau maradhi ni ugonjwa hatari. Ni vizuri kila Mtanzania aweke maslahi ya taifa mbele na viongozi waonyeshe njia na sio kuwa na sauti ya mwisho juu ya Muungano.
Muungano una matatizo, lakini unaweza kukarabatiwa isipokuwa unataka mafundi stadi na waadilifu. Tukiwa tumetimiza miaka 45 tuifanye kazi hiyo kwa uadilifu na tuache kupiga kelele za kuwa mbioni wakati tumebweteka na hatufanyi lolote kumaliza matatizo ya Muungano.