Maelezo yafuatayo yana historia nzuri sana ya muungano wetu. tafadhali tuchukue muda wetu kuyasoma
KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya, tuliona jinsi Muungano wa Tanzania ulivyofikiwa kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuunda Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyokuja kujulikana baadaye kama Tan-zan-ia, miezi sita tangu nchi hizo ziungane.
Tuliona pia mgawanyo wa madaraka chini ya Muungano huo kati ya Serikali ya Muungano na serikali za Tanganyika na Zanzibar kwa kuzingatia Hati [Mkataba] ya Muungano ya Aprili 22, 1964.
Mwisho, tuligusia juu ya malalamiko yaliyoanza kujitokeza miongoni mwa baadhi ya Watanzania juu ya marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yakiwamo mawili; moja ni lile la Katiba hiyo kutaja Zanzibar kuwa ni nchi yenye mipaka na yenye Serikali yake. Lingine ni lile linalompokonya Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka na uwezo wa kuigawa Zanzibar katika majimbo na mamlaka ya kuteua wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya Visiwani aliyokuwa nayo, kwamba yana lengo la kubomoa na kudhoofisha Muungano.
Katika sehemu hii ya pili ya makala, tutaona kama Zanzibar ni nchi au la, yenye mamlaka ya kufanya marekebisho iliyofanya, na kama imekiuka Katiba na matakwa ya Muungano.
Kipi kiliungana, Jamhuri au nchi?
Ibara ya kwanza ya Mkataba wa Muungano na utangulizi wa Sheria ya Muungano, Namba 22 ya 1964 ziko wazi kwa hili kwa maneno yafuatayo:
..It is therefore AGREED between the Government of the Republic of Tanganyika and of the Peoples Republic of Zanzibar as follows:-
(i) The Republic of Tanganyika and the Peoples Republic of Zanzibar shall be united in ONE SOVEREIGN REPUBLIC.
Kwamba, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zimekubaliana kuungana kuwa Jamhuri kuu [sovereign] moja kwa jina la [Jamhuri ya] Tanganyika na Zanzibar, na kwa masharti yaliyofafanuliwa kwenye Mkataba wa Muungano, mkataba ambao ndio msingi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Sheria mbili zilizoridhia Muungano za 1964; yaani Sheria ya Tanganyika ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Namba 22, na Sheria ya Zanzibar ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika, zilitambua na kuhalalisha Muungano huo kwa Masharti ya Mkataba wa Muungano ili kuupa nguvu ya kisheria kuweza kutumika katika nchi hizo.
Zilichojivua Tanganyika na Zanzibar [kama nchi huru] na kutoa kwa Muungano pekee, ni ile hadhi ya kuwa Jamhuri ili kuunda Jamhuri Kuu chini ya Mkataba wa Muungano. Kuanzia hapo hazikujulikana tena kwa jina la Jamhuri ya Tanganyika au Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, bali kama Tanganyika au Zanzibar tu, kama inavyothibitishwa na baadhi ya ibara za Mkataba huo na Sheria za Muungano; zikiwamo ibara ya 5 [Mkataba] na 2 [Sheria] zenye kusomeka: Sheria za Tanganyika [sio Jamhuri ya Tanganyika] na zile za Zanzibar [sio Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kama zamani] zilizopo zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo; au ile ibara ya 7 iliyompa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuitisha Mkutano wa Katiba wenye Wajumbe kutoka Tanganyika na Zanzibar. Hakuna mahali inapotajwa ama katika Mkataba wa Muungano, au katika Sheria za Muungano kwamba baada ya kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar zitafutwa au zitajifuta.
Nchi inaweza kuwa huru lakini si lazima iwe Jamhuri. Nchi huru bila kuwa Jamhuri maana yake ni kuwa chini ya himaya/uongozi au usimamizi wa Taifa au Serikali nyingine ya juu yenye nguvu zaidi.
Kwa mfano, Tanganyika ilipata uhuru Desemba 9, 1961 chini ya Katiba ya Uhuru ya 1961 iliyotungwa kwenye Ofisi ya Makoloni nchini Uingereza [London], na kutiwa sahihi na Malkia wa Uingereza. Chini ya Katiba hiyo, Tanganyika huru iliongozwa na Waziri Mkuu chini ya Gavana wa Uingereza akimwakilisha Malkia wa Uingereza kusimamia mambo kadhaa ambayo Serikali ya Wazalendo haikupewa mamlaka, lakini bado iliitwa nchi huru.
Ni pale tu ilipopigania haki ya kuwa Jamhuri, kwa maana ya Serikali na utawala wa nchi kuwa chini ya wazalendo kikamilifu chini ya Katiba ya Jamhuri ya 1962; ndipo Tanganyika ilipopata hadhi ya kuwa Jamhuri ya Tanganyika, na Gavana, Richard Turnbull, akaondoka nchini.
Vivyo hivyo kwa Zanzibar. Nchi hii ilipata uhuru wake Desemba 9, 1963 chini ya Serikali [ya mseto] iliyoundwa na Vyama vya Zanzibar Nationalist Party [ZNP] na Zanzibar and Pemba Peoples Party [ZPPP] ikiongozwa na Waziri Mkuu, kwa kuzingatia Katiba ya Uhuru kwa misingi ya makubaliano ya Lancaster House kabla ya uhuru.
Kwa misingi hiyo hiyo kama ilivyokuwa kwa Tanganyika, Zanzibar huru haikuwa Jamhuri mpaka yalipofanyika Mapinduzi, Januari 12, 1964, yaliyongoa Serikali mpya madarakani na Sultani ambaye alikuwa bado mtawala wa kilele, kama alivyokuwa Malkia wa Uingereza kwa Tanganyika huru kabla ya Jamhuri. Kufuatia Mapinduzi hayo, Zanzibar ilipata hadhi ya kuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Kwa hiyo, wakati zinaungana, Tanganyika na Zanzibar zilikuwa nchi huru na zenye Jamhuri, na pale zilipokamilisha Muungano kwa kutoa sadaka hadhi yake ya Jamhuri kwa Muungano, zilibakia nchi huru bila Jamhuri, zikajiongoza kwa Sheria zake pamoja na Katiba, huku dola ikihamia kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Muundo huu wa Serikali si mpya, hususan, kwa nchi za Jumuiya ya madola [Commonwealth]. Mfano mwingine mzuri ni nchi za Canada na Australia ambazo licha ya kuwa na Serikali zenye mamlaka chini ya Waziri Mkuu, lakini ziko chini ya Malkia wa Uingereza kwa sababu hazijawa Jamhuri.
Hata nchi kama Kenya; baada ya kupata Uhuru 1963, Rais wake, hayati Jomo Kenyatta, alipenda sana nchi yake isiwe Jamhuri, bali ibakie kama nchi huru chini ya Malkia wa Uingereza na yeye akiwa Waziri Mkuu na kiongozi wa Serikali ya Kenya. Alibadili mawazo na msimamo huo baada ya kushinikizwa na wanamapinduzi/wanaharakati kama hayati Tom Mboya, ndipo Kenya ikawa Jamhuri, na yeye [Kenyatta] akawa Rais Mtendaji wa Kenya.
Kwa mfumo huo, kulikuwa [hadi sasa] na Serikali tatu: Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar [ibara ya 1 na 4, ya Mkataba wa Muungano], Serikali ya Tanganyika [ibara ya 3 na 5], na serikali ya Zanzibar [ibara ya 3 (a) na 5]. Tofauti na Serikali za Tanganyika na Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano iko juu ya zote kwa sababu ni Jamhuri; na ndiyo pia inayobeba dola kuu kwa kuzipokonya Serikali hizo uwezo wa kujiamlia baadhi ya mambo makuu ya ndani, yanayojulikana kama Mambo 11 ya Muungano, tuliyoyataja katika sehemu ya kwanza ya makala haya, ambayo ndiyo yanayounda mamlaka ya Jamhuri ya Muungano.
Muundo upi wa Muungano uliokusudiwa?
Kwa kuwa Muungano haukuvunja Serikali za Tanganyika na Zanzibar, ni upi kati ya miundo minne inayotatiza, uliokusudiwa: Muungano wenye Serikali moja, Serikali mbili, Serikali tatu au Shirikisho?
Jibu la swali hili linaweza kupatikana kwa kutazama tu dhamira ya Waasisi wa Muungano kabla ya kuungana.
Dhamira kuu ya jumla kwa Viongozi wote wa nchi za Afrika Mashariki Tanganyika, Kenya na Uganda kabla na baada ya uhuru, ilikuwa ni kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki kama hatua moja ya kufikia Shirikisho la Afrika. Mtetezi mkubwa wa Umoja wa Afrika kwa njia au mfumo wa kuanza na miungano ya kikanda [Shirikisho la nchi] alikuwa Mwalimu Julius K. Nyerere, akichuana vikali na Rais wa Ghana, Dakta Kwame Nkrumah, aliyeona Miungano midogo midogo ya kikanda au Shirikisho, ilikuwa ni kupoteza muda na kutaka Afrika iungane mara moja kabla Viongozi wa Afrika mpya hawajanogewa madaraka wakaona vigumu kuachia ngazi kwa Shirikisho.
Kuthibitisha kwamba aliamini alichotetea, Nyerere alinukuliwa wakati mmoja akisema, alikuwa tayari kuchelewesha uhuru wa Tanganyika [1961] hadi Kenya na Uganda zipate uhuru ili waweze kuungana kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki.
Dhamira ya Nyerere juu ya aina ya Serikali ya Muungano aliyotaka ilijitokeza wazi kwenye Mkutano wa pili wa nchi huru za Afrika [OAU] mjini Cairo, Julai 1964 alipokataa kata kata kwa nguvu ya hoja, Muundo wa Serikali moja kuwa haufai kwa nchi za Kiafrika.
Miezi michache baadaye, alielezea msimamo wake huo kwa njia ya makala ndefu katika jarida la African Forum [The Nature and Requirements of African Unity in Africa] Vol.1, 1965 pg. 46, na kunukuliwa pia katika kitabu chake Freedom and Unity, uk. 300 304, akisema:
Muungano unaotakiwa si wa kuunda Taifa [state] moja lenye Serikali kuu moja yenye nguvu; bali ni kuunda Serikali ya Muungano yenye mamlaka ya pekee katika maeneo kadhaa ya msingi. Zaidi ya hayo, kunaweza kuwa na Serikali zingine zenye mamlaka ya pekee madogo kuliko yale ya Serikali ya Muungano, yatokanayo na Katiba za nchi hizo, na siyo kutoka Serikali kuu [ya Muungano].
Mwalimu aliendelea kufafanua: Hii, kwa tafsiri rahisi, ni muundo wa Serikali aina ya Shirikisho, ambalo madaraka yake yamegawanyika kati ya mamlaka kuu na sehemu [nchi] zinazounda Muungano huo kwa mujibu wa matakwa ya waasisi na kwa vizazi vijavyo.
Mapema kabla ya hapo, dhamira na utashi wa Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki juu ya aina ya Muungano wa Shirikisho kuliko aina nyingine yoyote, ulidhihirika kwa njia ya TAMKO la pamoja kwenye Kikao kilichofanyika mjini Nairobi, Juni 5, 1963, kwa maneno yafuatayo:
Sisi, Viongozi wa Watu na Serikali za Afrika Masharikitunajifunga kwa kiapo [pledge] kuunda Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki. Mkutano wetu wa leo unaongozwa na hamasa na utashi wa Afrika moja na sio kwa ubinafsi na matakwa ya kikanda [soma: Azimio la Shirikisho la Serikali za Afrika Mashariki, Kumb. Na. 13/931/63 PDT/1/1]
Zanzibar haikuwamo, kwa sababu wakati huo ilikuwa ikijiandaa kwa ajili ya uchaguzi Mkuu wa Julai 1963, kuelekea kupata uhuru. Lakini hata hivyo, Wakuu hao hawakuisahau Zanzibar, licha ya kwamba ilikuwa bado kwenye mchakato kuelekea Uhuru; TAMKO hilo lilisema: Ingawaje Zanzibar haikuwakilishwa katika Mkutano huu, hili tunaliweka wazi kwamba, nchi hiyo inakaribishwa kushiriki kikamilifu katika Mkutano wetu wa kuunda Shirikisho mara tu itakapomaliza uchaguzi wake mwezi ujao, Serikali yake itaalikwa kushiriki kama mshirika katika kuunda Shirikisho tunalokusudia kuunda.
Mapinduzi Zanzibar yalitibua Shirikisho
Ukweli ni kwamba, wakati Mapinduzi ya Zanzibar yakifanyika Januari 12, 1964, Wakuu wa nchi za Tanganyika, Kenya, Uganda na Zanzibar [Serikali ya ZNP/ZPPP] walikuwa mjini Nairobi kuendeleza mazungumzo ya mradi wa kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki.
Hapa, tunaweza kuelewa kwa nini Rais Nyerere alimkaribisha mjini Dar Es Salaam, Sultani wa Zanzibar aliyepinduliwa, baada ya kukataliwa na Serikali ya Kenya kutia nanga Mombasa alikotaka kukimbilia. Inawezekana kabisa Nyerere, kwa dhamira thabiti ya kukamilisha mchakato wa Shirikisho la Afrika Mashariki, alikuwa amemkubali Sultani kama sehemu ya utawala Zanzibar, na kwamba kupinduliwa kwake lilikuwa pigo kwa mchakato huo.
Tunaweza kuelewa pia ni kwa nini Nyerere alikataa kuitambua Serikali ya Mapinduzi [hadi baada ya siku tano kupita], wakati Kenya na Uganda ziliitambua siku mbili tu kufuatia Mapinduzi. Nyerere alikataa kuitambua Serikali mpya kwa madai kwamba, hakuwa na uhakika kama ni kweli Karume alikuwa amechukua madaraka, jambo ambalo ama huenda halikumwingia kichwani, au alitaka kuhakikisha Karume ameshika madaraka badala ya Field Marshal John Okello aliyekuwa akitangaza redioni mara kwa mara kwamba yeye ndiye alikuwa Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi.
Nyerere alimkaribisha Sultani aliyepinduliwa mjini Dar es Salaam, Jumatano Januari 15, 1964 kwa kile alichokiita huruma ya kibinadamu, wakati huo wanamapinduzi Zanzibar wakiwa wameapa Sultan huyo kutokanyaga tena ardhi ya Zanzibar. Alikaa Dar Es Salaam kwa siku sita hadi Januari 20, 1964 alipokamilisha mipango yake ya kukimbilia uhamishoni London, Uingereza.
Hebu tujikumbushe kidogo jinsi tukio la Mapinduzi lilivyotibua kwa muda programu ya Mwalimu kuhusu Shirikisho kwa kukosa uhakika ni kiongozi yupi wa Mapinduzi Zanzibar ashirikiane naye kuweka mambo sawa. Kwa hili, inaonyesha dhahiri kwamba, Mwalimu hakujua mpango huo wa Mapinduzi hadi yalipotokea, vinginevyo angemtambua Karume au John Okello mara moja; na asingemkaribisha Dar es Salaam Sultan aliyepinduliwa.
Vivyo hivyo, niharakishe kutamka kwamba, Sheikh Abeid Karume hakujua mpango huo kwa sababu wanaharakati wa Mapinduzi [wa Umma Party na ASP] walimficha, kwa kuhofia kwamba angeyazuia kwa vile alikuwa mwoga na mtu asiyependa umwagaji damu. Ndiyo maana risasi ya kwanza ilipofyatuliwa usiku huo wa Mapinduzi aliogopa kwa kutojua kilichokuwa kinatokea na kukimbilia Dar es Salaam usiku huo.
Karume na Okello walijikabidhi kwa Nyerere
Jumapili usiku, Januari 12, 1964, Karume alikwenda kwa Nyerere Ikulu, naye [Nyerere] akamshauri [aache woga] arudi Unguja mara moja. Nyerere ndiyo tu alikuwa amerejea siku hiyo kutoka Nairobi kwenye kikao cha Shirikisho.
Kwa kukerwa na yaliyokuwa yakitokea Zanzibar, Jumanne, Januari 14 1964, Mwalimu alienda Nairobi kuonana na Waziri Mkuu wa Kenya, Jomo Kenyatta juu ya matukio ya Zanzibar na athari zake kwa mchakato wa Shirikisho, na kurejea Dar es Salaam siku hiyo hiyo na kumkaribisha Sultan wa Zanzibar aliyezuiwa kutia nanga Mombasa na Serikali ya Kenyatta.
Huko Zanzibar, Kiongozi wa Wapiganaji wa Mapinduzi, Field Marshall John Okello, tayari alikuwa ameunda Serikali yake na kujiteua Mkuu/Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi, na akamteua Karume kuwa Rais wa Zanzibar asiye Mtendaji. Na kupitia Redio Zanzibar ambayo alikuwa ameiteka na kuiweka chini yake, alimwita Karume bila kujua alikokuwa, akisema: Karume, popote ulipo, rudi Zanzibar haraka kuchukua nafasi yako.
Alhamis, Januari 16, 1964, Karume alikwenda kwa Nyerere mara ya pili kuomba msaada wa ulinzi wa muda, na akaahidiwa askari 300 wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia [FFU] waliofika Zanzibar Jumamosi Januari 18, 1964 ili kurudisha amani Visiwani, na pia kumlinda dhidi ya wanaharakati waliokuwa wamepania kumwondoa madarakani kwa sababu ya kushindwa kudhibiti madaraka.
Jumapili usiku, Januari 19, 1964, huko Ikulu Dar es Salaam, Mwalimu alikuwa na mazungumzo mazito na Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibari, Field Marshal John Okello, aliyedai kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kupumzika kidogo, na katika mazungumzo hayo Mwalimu akamshauri afanye kazi kwa imani pamoja na Karume. Kwa maelezo hayo, bila shaka Mwalimu alimtambua Okello kama Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi, na Karume kama Rais.
Saa chache baadaye usiku huo, saa 7.50 kuamkia Januari 20, 1964 Jeshi la Tanganyika [Tanganyika Rifles TR] liliasi dhidi ya Serikali ya Nyerere; na kwa siku mbili mfululizo, Serikali hiyo ilikuwa mikononi mwa Waasi. Haielezwi ni vipi au kama wakati maasi hayo yakitokea Okello alikuwa bado [alilala] Ikulu na vipi aliweza kutoka wakati askari walioasi wakiwa tayari wameizingira Ikulu.
Maasi ya Januari 20, 1964 yaliyoitikisa Serikali ya Tanganyika, yalizikumba pia Kenya na Uganda kwa askari wake kuasi, siku hiyo hiyo, wakati huo huo wa maasi ya Tanganyika na kwa staili hiyo hiyo. Hata hivyo, maasi yote yalizimwa kwa nyakati tofauti, lakini kwa gharama kubwa kisiasa.
Nimelazimika kuelezea matukio haya kwa kirefu kutokana na mazingira yaliyojenga na hatimaye kubadili hoja na mchakato mzima wa Shirikisho la Afrika Mashariki, na badala yake kuzaa hoja ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kwa vipi?
Mpango wa kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki ulibuniwa na kusimamiwa na Marekani na Uingereza wakati wa harakati za Uhuru wa Tanganyika, Kenya, Uganda na Zanzibar kwa lengo la kuziweka nchi hizo ndani ya kapu moja, kuweza kuzidhibiti kwa njia ya rimoti, japo zingeendelea kujiita nchi huru.
Moja ya hofu iliyotawala Mataifa hayo makubwa enzi hizo hata kubuni mchakato huo, ni pamoja na Zanzibar kuwa kitovu cha Ukomunisti Afrika Mashariki, ambapo China na Cuba ziliweza kupenyeza sumu ya Ukomunisti kupitia wanaharakati wa Kimapinduzi wa Chama cha Zanzibar Nationalist Party [ZNP], na baadaye Chama cha Umma Party [UP], wakiwamo kina Abdulrahman Mohammed Babu, Kassim Hanga wa ASP na wengine.
Kwa hiyo, madhumuni ya kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki yalikuwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, Zanzibar inajiunga na kumezwa ndani ya tumbo kubwa la Shirikisho na kukoma kuwa tishio kwa mataifa makubwa ya Kimagharibi nyakati hizo za vita baridi, kati ya mataifa ya Magharibi na mataifa ya Mashariki.
Jomo Kenyatta [Kenya] na Milton Obote [Uganda] walizigundua njama hizi za Marekani na Uingereza, na miezi miwili tu kufuatia Mapinduzi ya Zanzibar, walijitoa hima kwenye mchakato wa Shirikisho na kumwacha Nyerere mpweke, akiangalia mchakato huo ukimfia mikononi hatua za mwisho. Kenyatta alinukuliwa mahali fulani akisema, hakuwa tayari kumpigia magoti Nyerere.
Haijulikani kwa nini Kenyatta alisema maneno hayo, yenye kuashiria kwamba Nyerere alitaka kuongoza kwa nguvu Shirikisho hilo. Inawezekana hisia zake zilikuwa sahihi au hapana; lakini Mwalimu amekaririwa katika mahojiano kati yake na Mhariri Mkuu wa jarida la Africa Forum [Vol.1, No. 1] la 1991, Ad Obe Obe akisema, hakuwa na tamaa ya kuwa Kiongozi wa Tanganyika; ila alitamani kuiwakilisha Afrika Mashariki kama nchi kwenye Umoja wa Mataifa. Je, hilo ndilo lililomkoroga Kenyatta, ikizingatiwa kwamba Kenyatta huyo huyo, ambaye siku chache tu, ndiye aliyeonesha nia ya nchi yake huru kuendelea kuwa chini ya himaya ya Uingereza?
Na kwa kuwa azma ya Marekani na Uingereza, ya kuona Zanzibar inamezwa ndani ya tumbo kubwa ilikuwa pale pale, mpango na mkakati mbadala wa kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar ukasukwa chini ya uratibu wa Mataifa hayo mawili.
Kwa kuanzia, Mwalimu Nyerere alituma Zanzibar ujumbe wa watu wawili Bibi Titi Mohamed [Mjumbe wa NEC ya TANU na Naibu Waziri] na Oscar Kambona [Waziri wa Mambo ya Nje], kwenda kumuomba Karume akubali nchi zao ziungane; lakini Karume alikataa kata kata kwa madai kwamba, alitaka kuweka kwanza nyumba [nchi] yake sawa kabla ya kufikiria jambo kama hilo.
Kabla ya kuondoka Zanzibar, Kambona na Bibi Titi walionana na Viongozi wa Zanzibar wenye ushawishi mkubwa Visiwani, Saleh Saadallah na Kassim Hanga, na kuwaachia jukumu la kumshawishi Karume akubali Muungano.
Ujumbe huo ulifuatiwa na ujumbe wa pili, wa Mawaziri Tewa Said Tewa na Job Lusinde. Hatujui Mawaziri hao walirudi na ujumbe gani kwa Nyerere kutoka kwa Karume; lakini Aprili 21, 1964, Karume, baada ya mazungumzo kwa njia ya simu na Nyerere siku hiyo, aliondoka ghafla Zanzibar kwa siri kwenda Dar Es Salaam kukutana na Nyerere, akifuatana na Maafisa Usalama wawili tu na Msaidizi wake, bila Wazanzibari wengi kujua, na kurejea Zanzibar siku hiyo hiyo.
Mara tu baada ya kurejea, Karume alimwagiza Msaidizi wake, Ali Mwinyigogo, kuandaa mapokezi ya Mwalimu Nyerere aliyetarajiwa kutua Zanzibar siku iliyofuata, Aprili 22, 1964.
Licha ya kwamba madhumuni ya safari, na mambo yaliyozungumzwa kati ya Nyerere na Karume alipokwenda Dar Es Salaam Aprili 21, hayakuwa wazi; lakini taarifa za uhakika zinaonyesha kwamba, Nyerere alimtaka Karume akubali Muungano, na alipoendelea kukaidi, Nyerere alitishia kuondoa askari 300 aliompa Karume kusaidia kurejesha hali ya amani Visiwani; naye [Karume], kwa kuona kwamba usalama wa Serikali yake na yeye mwenyewe ungekuwa mashakani, alisalimu amri na kukubali kuungana.
Itakumbukwa kwamba, siku tatu kabla ya Karume kuitwa na Nyerere, Dar Es Salaam, Nyerere alikuwa amemwita Mwanasheria wake Mkuu [AG], Roland Brown, na kumwagiza aandae kwa siri kubwa, rasimu ya Mkataba wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa Muundo wa uhusiano kama ule kati ya Uingereza na Ireland; naye [Brown] akafanya hivyo.
Huo ndio Mkataba wa Muungano ambao Nyerere na ujumbe wake, alitua nao mkononi Zanzibar, Aprili 22, 1964; na kutiwa sahihi kati yake na Karume siku hiyo hiyo kuashiria kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Walioshuhudia wino ukimwagwa kuthibitisha fungate ya ndoa hiyo, walikuwa ni pamoja na Mawaziri Bhoke Munanka, Job Lusinde na Oscar Kambona, kwa upande wa Tanganyika; na Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Ali Mwinyigogo, kwa upande wa Zanzibar.
Mambo muhimu Yaliyomo katika Mkataba, pamoja na Katiba iliyozaliwa kwa msingi wa Mkataba huo, nimeyaelezea mapema katika makala haya. Ni kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba huo wa Muungano, sasa Wazanzibari wameweza kufanyia marekebisho Katiba yao ya 1984, huku baadhi ya marekebisho yakizua tafrani miongoni mwa Watanzania kwamba yamekiuka matakwa na Katiba ya Muungano. Ni yapi hayo? Kuna ukweli gani kwamba marekebisho hayo yamedhihaki misingi ya Muungano?