John Joseph Pombe Magufuli kwa mara ya kwanza aliteuliwa na Raisi Benjamin William Mkapa kuwa Waziri mdogo wa Ujenzi mwaka 1995 hadi 2000 alipoteuliwa kuwa Waziri kamili wa Ujenzi. Wadhifa huo aliendelea nao hadi mwaka 2006 alipoteuliwa na Raisi Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Waziri wa Ardhi na Nyumba mwaka 2006.
Mwaka 2008 aliteuliwa kushika wadhifa wa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi hadi mwaka 2010 alipohamishiwa tena Wizara ya Ujenzi. Kwa kifupi ni kwamba John Pombe Magufuli ameshikilia nyadhifa mbali mbali ngazi ya Uwaziri kwa kipindi cha miaka ishirini katika awamu zote mbili toka tuingie kwenye mfumo wa vyama vingi.
Kwa miaka kumi na tano John Pombe Magufuli ameshiriki katika vikao vyote vya Baraza la Mawaziri na ameshiriki katika vikao vyote vya juu vya chama tawala CCM. Kwa maneno mengine ni kwamba hakuna maamuzi serikali ilichukua wala mikataba serikali iliingia bila ushiriki wa John Pombe Magufuli ama moja kwa moja au kwa kuwakilishwa.
Ni katika kipindi hiki cha miaka ishirini ndipo tumeshuhudia mambo ya ajabu kweli kweli ndani ya taifa hili, tumeshuhudia kashfa baada ya kashfa hadi neno hili limepoteza maana. Pia ni katika kipindi hiki tumeshuhudia uvunjaji wa katiba na vyombo ambavyo vilitakiwa kuilinda na kuitetea katiba lakini hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi ya wahusika.
John Pombe Magufuli kwa sasa ameteuliwa kuwa mgombea wa Uraisi kupitia CCM na moja katika ahadi zake za mwanzo kabisa ni kuendeleza walikofikia waliomtangulia. Sera anazoahidi kuzitekeleza ni zile zile za waliomtangulia lakini cha ajabu ni pale anapotuomba wananchi kumuamini kwa kuwa yeye, tofauti na waliomtangulia, ni mtendaji.
Mpaka hapo sina ugomvi na John Pombe Magufuli lakini ugomvi wangu naye unakuja pale anapoanza kushangaa kama vile hajawahi kuishi hapa nchini. John Pombe Magufuli anashangaa tulivyoweza kufika hapa tulipo, anashangaa chombo gani hicho kimetufikisha hapo na kwa nini wananchi tulikubali tufikishwe hapo na chombo hicho.
John Pombe Magufuli anashangaa tembo wetu kuuawa na pembe kusafirishwa kwa ndege kwenda China, anashangaa nchi kukosa hata kiwanda kimoja cha Kusindika nyama na samaki, anashangaa wauzaji wakubwa wa Tanzanite kuwa Kenya na India, anashangaa hospitali zetu kukosa dawa hadi viongozi wanakimbilia kwa babu kupata kikombe au Ulaya kwa matibabu...
John Pombe Magufuli hakushangaa alipokuwa Waziri, hakushangaa alipoenda Samunge kubugia kikombe, hakushangaa alipouza nyumba za serikali, hakushangaa ripoti ya CAG ilipomtuhumu na upotevu wa mabilioni, hakushangaa alipovunja makazi ya watu na kuwaacha "homeless", hakushangaa wezi wa EPA walipoombwa kurudisha walichokwiba, hakushangaa...
John Pombe Magufuli hakuweza kuuliza kulikoni akiwa kwenye Baraza la Mawaziri, akiwa na Mwenyekiti wake wa chama, akiwa na watendaji wenziwe serikalini na wizarani, akiwa kwenye kikao cha Kamati Kuu...hapana alisubiri siku anapewa upendeleo maalum kupeperusha bendera na kuomba kura zetu, ashangae waliyoyatenda wakiwa madarakani.
John Pombe Magufuli anataka kuwa Raisi wa nchi hii awamu ijayo, anataka tuamini kuwa wengine wote wanaoomba nafasi hiyo hawafai akiwatuhumu kuwa na uroho wa madaraka. Kwa miaka ishirini amekuwa sehemu ya uozo tunaotaka kuuondoa lakini leo ana ujasiri wa kutuomba tumuamini, anaahidi kutotuangusha na kweli wapo wanaopiga vigelegele!
Wanawakandia waliofunguka macho na kuachana na genge lao, wanawatukana wananchi waliowachoka, wanawakebehi wasiokubaliana na unafiki wao, wanaapa hawaachi madaraka hata kwa miaka mia, wanatamba vyombo vyote vya dola wanavimiliki na wanadai ushindi ni wao hata kwa goli la mkono! Wanachosahau ni ni kuwa historia haiko upande wao!