Kitu kimoja , Mzee Mohamed Said amesaidia kuonyesha historia ambayo ilikuwa haikupewa nafasi sana. Udhaifu wake ni kuonyesha ulifanywa , kama waislam. Nafasi ya Nyerere ilikuwa muhimu kutokana na elimu aliyopata kule Edinburg na pamoja ujuzi wa kujua na kufuatilia hali ya kisiasa Tanganyika.
Wakati Nyerere yupo Edinburg - Abdul Sykes, Steven Mhando, Dr. Kyaruzi, DR . Seree , Mwapachu walitengeneza " Memorandum for Political Independence " hili dodoso waliloliwakilisha kwenye ofisi ya Umoja Wa Mataifa, inayohusu Makoloni, iliwaletea shida watu mbalimbali akiwemo, Mwapachu hadi akahamishiwa Ukerewe.
Hivyo Mwapachu, akamwandikia barua Nyerere akiwa Edinburg kuhusiana na hali nyumbani. Utagundua , Nyerere akiwa Edinburg vuguvugu la mabadiliko lilikuwa linaendelea nchini na kukaibuka viongozi mbalimbali kusongesha mapambano.
Saadani Abdu Kandoro, Said Maswanya na Bhoke Munanka kutoka maeneo ya Majimbo ya Ziwa ( Lake Province)
Kwa hiyo ukiangalia historia ya uhuru na mapambano ya Tanganyika , ilipita kwa michango wa watu tofautitofauti wa kada mbalimbali.. Tukitafuta kwenye historia zaidi, tutakuta makundi ya michango ya wafanyakazi, wakulima, wavuvi , wafanyakazi toka vyama mbalimbali na maeneo tofauti tofauti. Na makundi zaidi bado yapo .
Hii inanipa hamasa kuendelea kutafuta historia ya Tanganyika , ili kuweka mjumuiko mzuri. Kazi hii si ya kitoto au ndogo.. Na wakati tunaendelea na hayo na bado yataendelea sana, isifanye ionekane kuwa ni watu fulani wa madhehebu fulani, kutoka eneo fulani ndio waliochangia uhuru wa Tanganyika.
Newazz,
Hapakuwa na kitu kinaitwa, ''Memorandu for Political Independence,'' ila kulikuwa na ''Memorandum to Constitutional Development Committee,'' na hii iliandikwa na TAA Political Subcommittee Commitee ambao wajumbe wake walikuwa hawa wafuatao: Mufti Sheikh Hassan bin Ameir, Abdulwahid Sykes, Hamza Kibwana Mwapachu, Sheikh Said Chaurembo, Dr. Vedasto Kyaruzi, John Rupia na Steven Mhando.
Hii memorandum haikupelekwa UNO bali iliwasilishwa kwa Gavana Edward Francis Twining kwani yeye ndiye aliyeomba maoni kutoka kwa wananchi wa Tanganyika katika jumuia zao na TAA wakachukua nafasi hii pamoja na taasisi nyingine zilizokuwapo.
Hii memorandum ilijadiliwa mwaka wa 1954 katika mkutano ulioasisi TANU na mapendekezo ya hii memorandum ndiyo yaliyowasilishwa UNO na Nyerere mwaka wa 1955.
Kamati hii ilidai kwanza pawepo na uchaguzi wa kura moja mtu mmoja na Tanganyika ipewe uhuru baada ya miaka 13.
Serikali ilishtushwa sana na mapendekezo haya na ikaamua kuwaadhibu wale waliokuwa wafanyakazi wa serikali.
Dr. Kyaruzi akahamishiwa Kingolwira Prison, Hamza Mwapachu akapelekwa Nansio Ukerewe na Abdul Sykes manusra apoteze kazi yake kama Market Master, Kariakoo Market.
Hapa ndipo wazalendo hawa na wao wakaamua sasa ili kupambana na Waingereza mipango ianze ya kuunda chama cha siasa.
Hii ndiyo kamati ndani ya TAA iliyokiongoza chama hiki kuelekea kuunda TANU 1954 na uhuru ukapatika 1961.
Hii document ina sahihi ya hawa wanakamati wote.
Bahati mbaya hii document imepotea na inaaminika imetolewa kwa kunyofolewa katika nyaraka za TANU na katika nyaraka za Tanganyika National Archives (TNA).
Lakini hii document ipo Rhodes House, Oxford, Uingereza.
Katika watafiti wa historia ya uhuru wa Tanganyika ni waandishi watatu tu Judith Listowel (The Making of Tanganyika, 1965), ndiyo walioigusia katika vitabu vyao, Cranford Pratt (The Critical Phase in Tanzania, 1976) na mwandishi (The Life and Times of Abdulwahid Sykes...1998).
Hii document ni muhimu sana katika historia ya TAA.
Namaliza kwa kusema kuwa mtu aliyetoa mchango mkubwa katika kuitayarisha hii document alikuwa Earle Seaton mwanasheria kutoka Bermuda aliyekuwa rafiki wa Abdul Sykes.
Hotuba ya Mwalimu Nyerere UNO mwaka wa 1955 inatoka katika document hii.