Mwezi Julai 2025, wanafunzi na walimu 20 wa Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang waliwasili Port Elizabeth nchini Afrika Kusini, na kuwa wimbi jingine lisiloyumba la mawasiliano ya kielimu baina ya China na Afrika yaliyoanzishwa katika miaka ya hivi karibuni.
Wakati mwaka 2026 ni wa mawasiliano baina ya watu wa China na Afrika, chuo kikuu hicho kinadumisha uhusiano wake kwa kutuma takriban wafanyakazi 100 nchini Afrika Kusini kila mwaka huku makundi mapya ya Afrika yakiwasili kila muhula.
Kwa miaka mingi, ushawishi wa ushirikiano kati ya China na Afrika madarasani umekuwa ni wa zaidi ya nyanja ya elimu. Unasimama kama ushuhuda dhahiri wa ushirikiano ambao umewawezesha makumi kwa maelfu ya wanafunzi na kuzivuta pande hizo mbili karibu zaidi katika mabara yote. Mwaka uliopita ulikuwa ni wa maadhimisho ya miaka 10 ya lugha ya Kichina kuingizwa rasmi katika mfumo wa kitaifa wa elimu wa Afrika Kusini.
Kwa Musfirah Yasir, machaguo hayo kwake ni ya binafsi sana. Akiwa amezaliwa Pakistani na kukulia Johannesburg, sasa ni mwanafunzi wa kozi ya masoko duniani katika Chuo Kikuu cha Johannesburg. Baada ya darasa, anafanya mazoezi ya toni za Kichina mara kwa mara, kisha anajifunza miondoko ya uchezaji wa ngoma ya jadi ya Kichina mbele ya kioo.
Akitumbuiza katika hafla za kitamaduni zilizoandaliwa na Ubalozi wa China nchini Afrika Kusini, Yasir alihisi umbali kati yake na China ukianza kupungua. "China haikuwa ya kufikirika," alisema. "Bali niIlihisi kama ipo karibu zaidi."
Uzoefu wake unaakisi kazi ya Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Johannesburg katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Wanafunzi kutoka vyuo vikuu hukutana na lugha ya Kichina darasani, kisha hutoka nacho nje ya chuo kikuu yaani kwenye fursa za masomo nchini China au ajira katika makampuni yanayohusiana na China.
Programu za mazoezi ya kuzungumza kwa taasisi na biashara za umma zimesaidia lugha ya Kichina kuondoka darasani na kuhamia kwenye matumizi ya kila siku.
Kwa Yasir, mabadiliko haya yanamfunua akili. Kujifunza lugha, mazoezi ya kitamaduni na matarajio ya kitaaluma sasa yanaungana, ambapo ushirikiano wa kielimu kati ya China na Afrika si wazo tena, bali ni juhudi za kila siku, zinazopimwa katika mazoezi ya matamshi, kunengua ngoma kwa makini, na mustakabali unaoanza kuzingatiwa polepole.
"Kukiwa na zaidi ya wanafunzi 1,000 wanaojiandikisha kila mwaka, athari yake inaonekana," alisema Li Baosheng, mkurugenzi wa Kichina katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Johannesburg. "Lengo letu ni kuwasaidia vijana wengi zaidi kugeuza ujifunzaji wa lugha kuwa fursa halisi, na naamini kila taasisi ina dhamira hii."
Nait Si Youssef, ambaye hapo awali alichukua kozi ya lugha ya Kijerumani katika Chuo Kikuu cha Hassan II katika mji wa Casablanca nchini Morocco, alibadilisha shahada yake na kuchukua Kichina baada ya darasa lake la kwanza katika Taasisi ya Confucius ya chuo hicho.
Anasema uamuzi huo mmoja ulibadilisha maisha yake: Sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Taasisi ya Masomo ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal.
"Niligundua kuwa nilipenda toni na maandishi ya kichina, lakini muhimu zaidi, niliona mustakabali umeunganishwa nao," alisema Youssef.
Ndani ya miezi michache, alibadilisha kozi yake. Ndani ya miaka michache, alivuka mabara. Sasa akiwa anashughulikia utafiti wake kuhusu uhusiano wa China na Afrika, Youssef anatarajia kufuatilia mustakabali wake katika diplomasia baada ya kuhitimu na kusaidia kujenga uhusiano mpana wa kitamaduni kati ya China na Morocco. "Lugha hufungua milango," alisema. "Kuielewa inafanya iwe wazi."
Tangu 1964, wakati China ilipotoa ufadhili wa masomo kwa mara ya kwanza kwa wanafunzi wa Nigeria, zaidi ya Wanigeria 1,700 wamesoma nchini China kwa ufadhili kama huo. Kwa miaka mingi, wanafunzi wa China pia wamekuwa wakienda katika taifa hili la Afrika Magharibi.
Liu Hongwu, mwanzilishi na mkurugenzi wa Taasisi ya Masomo ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, sasa ana umri wa miaka 67. Akiwa miongoni mwa Wachina wa mwanzo kabisa kushiriki katika mawasiliano ya kitaaluma barani Afrika, alifika Chuo Kikuu cha Lagos kama msomi mgeni miaka 35 iliyopita. Akiwa huko, Liu alikwenda nje ya kozi yake, akiazimia kutembea kote Afrika.
Aligundua kuwa nchi nyingi za Afrika hazikuwa makini sana na historia; katika shule nyingi za msingi na sekondari, somo hilo halikufundishwa hata kidogo, na kuwaacha vijana wengi wa Afrika bila kujua historia yao.
Miaka kumi baadaye, akitumia mawasiliano na nyenzo alizokusanya, Liu alichapisha "Kutoka Jamii ya Kikabila hadi Jimbo na Taifa: Utafiti wa Maendeleo ya Taifa ya Nigeria." Toleo la Kiingereza, lililotolewa mwaka 2024, sasa linapatikana nchini Nigeria.
"Kazi hii ni mojawapo ya vitabu vyenye maelezo ya kina kuhusu historia ya Nigeria ambayo imeandikwa na mgeni," alisema Ikenna Emewu, mhariri mkuu wa Jarida la Uchumi la Africa na China. "Kitabu chake kinawafundisha Wanigeria historia ya Nigeria."
Kwa wengi nchini Nigeria, ujio wa kitabu hicho umemfanya Liu awe kama mtu aliyerudi nyumbani. Vijana kwa wazee wakafikia hadi kumwita "Lagos Boy," wakimsalimia kama mwanafamilia aliyepotea kwa muda mrefu, na kama ushahidi hai kwamba mawasiliano ya China na Afrika yanaingia moja kwa moja mioyoni mwa watu.
"Ninapenda jina langu la utani," Liu alisema. "Inamaanisha marafiki zangu wa Afrika wamenipokea." Kuanzia wakati alipokanyaga ardhi ya Afrika kwa mara ya kwanza, aliamini kila ushirikiano lazima ujengwe kwa uaminifu.
Akiongozwa na imani hiyo, Liu alianzisha taasisi ya kwanza ya masomo ya Kiafrika yenye makao yake makuu nchini China katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang mwezi Septemba 2007. Akianza mwanzo kabisa, alikusanya washirika wa chuo kikuu, serikali na Afrika ili kuanzisha utafiti wa China kuhusu Afrika namna ilivyo leo.
Afrika ya kisasa, iliyoathiriwa na uvamizi wa kikoloni, ilinyimwa kwa muda mrefu elimu nzuri ya ufundi. Baada ya uhuru, mataifa mengi hayakuweza kujenga mfumo wa elimu unaoweza kuleta maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia.
Liu alifupisha wazo hilo na kuwa wazo moja: kurekebisha elimu kulingana na hali halisi ya Afrika na kuiunganisha moja kwa moja na maendeleo.
Leo, vikao vya mafunzo vya kila mwaka vya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang vimevutia zaidi ya washiriki 4,000 wa Afrika.
Kutokana na mpango wake, taasisi hiyo iliungana na Baraza la Udhamini la China kufungua tawi la Afrika Magharibi katika Chuo Kikuu cha Ibadan cha Nigeria. Kila mwaka, wafanyakazi na wanafunzi zaidi ya 100 husafiri kwenda Afrika kwa ajili ya masomo, utafiti, au mawasiliano ya kielimu.
"Uhusiano wa watu na watu ndio msingi wa ushirikiano," Liu alisema. "Katika Afrika, mimi si profesa, si mkurugenzi, ni 'Lagos Boy' tu aliyerudi nyumbani."