Ni matapeli wa kidini kupenda kupora sifa zisizo zao
HISTORIA YA KANISA B.
Kati ya mwaka 700 - 1054 kulitokea mgogoro mkubwa wa Kanisa ambao hatimaye ulikuja kuligawa rasmi Kanisa hapa duniani katika mapande makubwa mawili mwaka 1054. Upande wa Magharibi uliitwa Western Roman Catholic Church na ulikuwa unamtambua Askofu Mkuu wa Rumi (Papa) kama ndio kiongozi wao. Upande wa Mashariki uliitwa Eastern Othordox (Catholic) Church na ulikuwa ukimtambua Askofu Mkuu wa Constantinople (Patriarch) kama kiongozi wao.
Sababu zilizopelekea mgogoro na mpasuko ule zilikuwa nyingi zikiwemo: 1. Matumizi ya taswila na sanamu (images) katika ibada (the iconoclastic controversy). Kutokana na changamoto ya Uislamu eneo la Mashariki, mwaka 726, Mtawala wa Dola ya Byzantine alipiga marufuku matumizi ya taswira na sanamu (images) katika ibada. Askofu Mkuu wa Constantinople aliunga mkono. Kitendo kile kililaaniwa vikali sana na Askofu Mkuu wa Rumi (Papa) kwa sababu kuu mbili; mosi, Magharibi hakukuwa na Uislamu hivyo hawakuwahi kushutumiwa na Waislamu kuwa walikuwa wanaabudu sanamu kama walivyokuwa wamatuhumiwa watu wa Mashariki ambako tayari Waislamu walianza kuiteka. Pili, Papa alisisitiza kuwa watawala wa kisiasa hawakupaswa kuingilia maswala ya Kanisa. Suala hili lilikuja kupungua nguvu mwaka 843 baada ya Mkutano (Mtaguso) Mkuu wa Kanisa la Mashariki kupitisha matumizi ya picha tu lakini sio sanamu katika ibada. Hata hivyo, tayari umoja wa Kanisa ulikuwa umeathiriwa sana.
2. Mgogoro kuhusu asili ya Roho Mtakatifu (the Filioque Controversy). Mkutano Mkuu wa Nikea ulishatoa msimamo wa kiimani kuwa "Roho Mtakatifu atoka kwa Baba ...". Baadaye, katika Mkutano Mkuu ambao haukuwahusisha Kanisa la Mashariki, Kanisa la Magharibi lilifanya marekebisho katika tamko la imani (amendment) na kuandika kuwa "Roho Mtakatifu atoka kwa Baba na kwa Mwana ...". Kitendo hiki kilipelekea Kanisa la Mashariki kulituhumu Kanisa la Magharibi kwa uasi! Kwao maamuzi kama yale yalihitaji Mkutano wa Kanisa zima ambao ungehusisha Maaskofu wote. Hadi leo, Kanisa la Mashariki linaikiri Imani ya Nikea kama ilivyokuwa mwanzo pasipo mabadiliko wakati Kanisa la Magharibi (pamoja na matawi yake) limeendelea kuikiri Imani ya Nikea iliyobadilishwa kipengere hicho. Baadhi ya Makanisa siku hizi hutambua kiri zote mbili.
3. Ugomvi wa Madaraka. Askofu Mkuu wa Rumi (Papa) alitaka atambuliwe kuwa ndiye Mkuu kuliko wote wakati Askofu Mkuu wa Constantinople (Patriarch) aligoma kumtambua naye akisisitiza kuwa walikuwa na mamlaka sawa.
4. Hakukuwa na mpaka rasmi kati ya mamlaka ya Rumi na mamlaka ya Constantinople hivyo kuzua mizozo ya kiutawala.
5. Mashariki, Kanisa lilikuwa linatii mamlaka ya Watawala wa Dola (serikali) wakati Kanisa la Magharibi lilisisitiza kutokuingiliwa na Dola na lilisisitiza viongozi wa Kanisa kuwasimamia viongozi wa serikali kuhusu maadili, nk.
6. Tofauti za kitamaduni: Magharibi walikuwa wakizungumza Kilatini wakati Mashariki walikuwa wakizungumza Kiyunani (Kigiriki). Pia kulikuwa na umbali wa maili 1000 kati ya Rumi na Constantinople.
7. Tofauti za ki-Liturgia: Hizi zilihusu mambo madogo madogo kama kutumia au kutokutumia mikate iliyochachushwa au isiyochachushwa katika sakramenti au ekaristi, kula mkate au kutokula mkate pamoja na divai wakati wa meza ya Bwana; Makasisi/Mapadre kunyoa au kutokunyoa ndevu na kuoa au kutokuoa, nk.
Mgogoro huo uliendelea hadi mwaka 1054 wakati Askofu Mkuu wa Rumi alipoandika waraka wa kumtenga Askofu Mkuu wa Constantinople kwa kutotii, naye Askofu Mkuu wa Constantinople akaandika waraka wa kumtenga Askofu Mkuu (Papa) wa Rumi. Hivyo Maaskofu Wakuu wa Makanisa Makuu ya Rumi na Constantinople wakawa wametengana na ndio Kanisa likawa limegawanyika rasmi. Kanisa la Magharibi liliendelea kugawanyika na kuzaa matawi kwa mfuatano ufuatao kuanzia lipi lilianza; Waldensian, Moravian, Lutheran, Mennonite, Presbyterian, Baptist, Anglican, Methodist, Assemblies of God, nk. Kanisa la Mashariki halijwahi kukumbwa na migogoro au migawanyiko ingawa lina matawi mengi kama vile Ethiopian Church, Coptic Church (Kanisa la Misri), Greek Orthodox, Russian Orthodox, Eastern Orthodox, Syrian Church, nk.
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula - Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania (KMUT).