Kutoka kwa Askofu Bagonza
MAONI NA MAONO Vs
KURA NA KODI
Mchakato wa uchaguzi mkuu unaendelea nchini kote. Tunasikia mengi, tunashauri mengi. Usipojishauri, unashauriwa. Nina mawili:
1. Katika zoezi la upigaji wa kura za maoni, ni muhimu kuazima hekima ya wahenga wasiojulikana isemayo kwamba " wenye maono hawana nafasi na wenye nafasi hawana maono". Kura za maoni hazina uhusiano na maono na watia nia.
2. Nchi inaendeshwa kwa kodi zetu. Hata mikopo inayochukuliwa ni hela yetu. Tutalipa kwa muda mrefu. Hata wasiozaliwa bado watalipa mikopo hiyo. Usimpe kura mtia nia bila kumpa kodi. Kura yako iende na kodi yako. Kura bila kodi inawafanya watawala wetu kukusanya kodi kama hela yao binafsi. Wanatumia kodi kama fedha binafsi! Tuwe macho. Kodi bila kura inawafanya wapiga kura kuwa kama vibarua katika shamba la tajiri. Tuwe macho, tupige kura na kulipa kodi. Tukiishalipa kodi, tusiziombe, tuzidai.
Daima tukumbuke, uchaguzi huru na wa haki, huhamisha mamlaka kutoka kwa watawala kwenda kwa wapiga kura. Uchaguzi kiini macho, hukomba madaraka kutoka wananchi kwenda kwa watawala na koo zao.