Inatokea post namba 179;
Kufika Chalinze nikamwambia dereva, twende upande ule kuna mama nafahamiana nae wa Kisomali, atatupatia vitu unavyotaka kwa bei poa.
Dereva; kwa Sofi msomali?
Mimi; Ndio hapo hapo.
Dereva; hapo ndipo napokwenda mimi, nachukua mirungi kwake, ananipa na mzigo wake unaoenda Morogoro na Dodoma, bro hizi kazi ukitegemea kusafirisha magari tu haya ya transit hazilipi. Tunajitahidi kama hivyo kama zipo order hapo, napakia.
Basi tukaingia kwa Sofia tukamkuta hayupo, yupo mwanamke mwengine wa Kisomali, na yeye ni wa Tanga, anaongea Kitanga. Nikasalimiana nae, nikamuuliza Anti Sofia hayupo?
Msomali; Anti yako Sofia siku nyingi kahamia Dar, mimi ndio nipo hapa siku hizi, mimi ndugu yake, watoto wa baba mkubwa na mdogo. Kwa hio upo na Anti Halima sasa. Hujapita hii njia siku nyingi? Sijawahi kukuona hapa.
Mimi; kweli, mimi sio mtu wa kupita sana njia hii, isipokua babangu anapita sana.
Halima; Anaitwa nani?
Mimi; Nikamtajia jina la mzee.
Halima; Usinambieeeee, ndio naona hizi sura nimeziona wapi? babako na mamako tumekua wote Tanga, tunajuana sana.
Mimi; Ndio wao wamenijulisha kwa Anti Sofia.
Halima; Wewe mtoto wa nyumbani kabisa, ngoja nimpigie mamako akwambie.
Halima akaanza kupiga simu akawa anaongea, namsikia anamwambia mama, ngoja nikupe surprise we malaya wa Kidigo.
Mimi: Haloo.
Mama; eeeh upo Chalinze? kweli hii surprise ya mwaka, mimi najua saa hizi labda ushafika Dodoma.
Mimi; Tulisimama kwa muda njiani, dereva alikua na kazi zake.
Mama; Nipe huyo Halima.
Sijui wakaongea nini pale, mwisho namsikia Halima anamwambia "huyu leo haendi popote, nimemkosa babake, yeye simkosi, nipo tayari hata kutuma vijana watie pancha gari lao". Nenda zako huko niwache kwa raha zangu, usinimalizie salio langu, kwaheri bwana, baadae. Akakata simu.
Halima; Umeamini sasa kama mamako ni rafiki yangu? Wewe mwanangu, kaa hapo unywe chai. Nikamwambia kahawa Anti. Akasema kahawa kama babako? Ngoja.
Akamwita mtu kwa ndani, akaleta chupa ya kahawa vikombe na visheti. Dah mtoto alieleta alikua wa Kisomali lakini bomba kweli, ingawa kavaa madiraa ya Kisomali, lakini anaonesha moto kweli.
Halima; Huyu mtoto wa dadangu, amepita tu hapa akaona abaki siku mbili anisaidie. Anakwenda Tanga, anaishi Dar huyu. Wewe si unaishi Dar? Mimi; ndio.
Halima; hamjuani?
Mimi; sijawahi kumuona.
Yule bintiu akasema, mimi namjua huyu, yeye kanisahau, wewe si kakake Nisha? Akamtaja jina wife wangu. Nikamwambia, huyo mke wangu.
Binti; Nilisikia, kumbe ni wewe mumewe, mimi namjua mamako pia, namjua na babako. Ma Shaa Allah Handsome kama babako,
Wewe tukija kwenu hatukukuti, miaka mingi mimi napajua kwenu, Ilala.
Halima; Si nimekwambia, wewe mtoto wa nyumbani, leo huondoki unabaki hapahapa.
Mimi; Leo siwezi nimetumwa kuna gari ya watu huko inaningoja mimi.
Halima; ukirudi basi usisahau kupita nikupe mzigo wa mamako.
Mimi; Poa anti.
Mara dereva akaja, akasema alienda kupiga rakaa msikitini.
Mimi; Ungenambia na mimi tungeenda wote,
Dereva; usijali utasali safar. Bi Halima, mzigo upo leo?
Halima; Upo wa Moro tu, ngoja niwaambie wautoe, sogeza gari basi.
Dereva; Usijali, nanunua mananasi na machungwa nakuja kupakia huo mzigo wako kwanza, juu yake naweka mananasi na machungwa.
Akaenda kwenye mananasi,nikamfata, kumuona muuza mananasi nikamkumbuka na yeye akawa ananitazama kama kaniona mahali hivi. Nikamwacha yule dereva ananunua mananasi, mimi nikajiambia sina wa kumpelekea zawadi nitachukua matatu ya kula mwenyewe. Ngoja nikanunue machungwa.
Nikaelekea kwenye machungwa, nikamkuta yule mzee rafiki yake baba, kuniona kanitazamaaa akanikumbuka. Aaah Simba umekuja tena?Ulituwachia bonge la kasheshe hapa, hebu twende kwanza tukaongee pale kwenye kahawa, maana babako anasema yeye haelewi chochote.
Machungwa yako yapo usijali, wewe staff hapa. Unataka na mananasi mangapi? Nikamwambia matatu tu sio makubwa sana, ya kula mimi tu njiani, akanambia, hayo umepata usijali. Twende tukanywe kahawa kwa Sofia, aah siku hizi yupo ndugu yake anaitwa Halima lakini sisi tumezowea kwa Sofi.
Tukaenda tukawa tunakunywa kahawa, kaanza. Basi siku ile bwana wale wanawake hawakutoka ndani, wakajaa wachawi usiku kucha wamefanya kila njia wameshindwa kutoka, mpaka asubuhi watu wakasema waitwe polisi. ,Maana watu wameshajazana na hawajui kwanini wanawake wameshindwa kutoka, ndani, kila mmoja na lake.
Basi akatokea mwanamke mmoja akasema niwacheni niongee ngee nao, akaingia ndani akaongea nao kama nusu saa, hajaulikana kapitia wapi, wale ndio wakatoka ndani, hawakuonekana tena mpka leo Chalinze hii, na hapa ndio imekua dawa, wanga qnapaogopa kama ukoma. Hebu nambie, umerithi mikoba ya babu yako? Nambie kweli bwana.
Mimi; Sijui, labda baba, mimi sikufanya kitu.
Machungwa; Ndio inavyokua hivyo una mavitu ya babu yako makubwa makubwa,babako mimi angenambia, asingenificha kitu, kakangu ndio anasimamia mashamba ya bibi yuako Muheza, umezindikwa wewe zindiko la simba la Kidigo, tutazamie kama kuna wengine wamejileta leta, uwakomeshe, sisi tunataka amani hapa.
Mimi nikawa nacheka tu. mara dereva akarudi na mananasi, nikamwabi huyu hapa ukitaka kununua machungwa atakupa best. Yule dereva akamwambia nataka pakacha ndogo tatu, usinipige tikitaka lakini.
Machungwa: Wewe upo na mwamba huyu nani akuchezee tikitaka? Naleta pakacha nne, lipia tatu zako tu, moja zawadi ya huyu mwamba, nawaambia na wenye mananasi wamletee mnanasi yake. Nikaagana nae, nikaona nimeletewa mananasi matano badala ya matatu na machungwa pakacha moja kubwa. Nikamwabia aliyeyaleta mwambie ahsante sana, Akasema namwambia, lakini mwenye mananasi anakuja mwenyewe, anasema amekuona lakini alikusahau.
Kidogpo akaja mwenye mananasi. Dah kijana, weewe muokozi wetu, pokea zawadi ya mananasi kutoka kwangu matatu na kutoka kwa jirani yangu mawili, tena ukichelewa kidogo utazungukwa na watu sasa hivi, Kile kisa kila mtu anakihadithia mpaka leo. Ule mkasa mzito
Halima; Kumbe ilikua ni wewe, alinambia Sofia, akaanza kucheka, Wadigo wa Tanga mna mambo nyinyi. Hayasemeki. Lakini tumeambiwa umefanya la maanna sana, watu wanachezeana sana hapa.
Drerva kaamka akasogeza gari kwa reverse, ukatiwa mzigo wa Halima halafu yakajazwa mananasi na mapakacha ya machungwa nyuma, tukaanza tena safari.
Inatokea post namba 181:
Tulivyofika mdaula, dereva akanambia mshikaji, kama unataka kusali, msikiti mzuri ule pale. Mimi nataka nile kidogo, ukisha sali njoo tule. Nikamwambia poa, twende nikaone kuna nini, mimi nimekula visheti vingi kwa Sofia.
Dereva: Kula mshikaji, mwili wako wa mazoezi huo unataka ule vizuri. Hapa kuna nyama nzuri sana, huyu Mwarabu anajua kutengeneza mbuzi, mie huwa napiga supu ya mbuzi hapa kila nikipita.
Tukaingia hoteli, ilikua imejaa watu, jamaa anaonesha ana chakula kizuri ingawa hoteli ni ya kizamani zamani. Nikaenda counter, jamaa yangu yeye kaagiza supu ya mbuzi na chapati, nikawauliza wana supu aina nyingine, wakanambia, ipo ya ng'ombe, nikamwambia mimi nitilie hiyo lakini naipiga kavu. Sitaki chapati. Akanambia kakae, nakuchagullia mwenyewe mnofu. Alikua mtu mzima hivi Mwarabu.
Tukawa tunakunywa supu pale, mara nikapigiwa simu, alikua yule dereva niliemuacha pale mbele ya kongowe. Akanambia nimeambiwa umetangulia bwana, bora bwana, ningekuchelewesha, mimi bado nipo, leo naona siondiki, si unajua waifu ytena, kanizuwia mpaka kesho. Ukifika nijulishe basi. Uko wapi sasa? Nikamwambia mimi ndio kwanza nipo Mdaula, tumekaa sana Chalinze. Sawa poa. Tutawasiliana zaidi.
Dereva; Mshikaji hebu nipe kisa, maana leo Chalinze nimeuziwa machungwa na mananasi kama bure. Kumbe unafahamiana sana na Sofi?
Mimi; Sio mimi, Sofi anafahamiana na wazazi wangu, mimi simjui sana.
Dereva: Yule ndio tajiri yangu, ana roho nzuri sana yule mama, hizi biashara mimi alinipa yeye, kuniona vile mtu wa mkeka, hata huyu tajiri nnaempelekea magari yake Burundi kaniunganisha nae yeye pia. Jana nilienda kumsalimia kwake na kumuuliza kama ana salamu zozote, akaniombea dua nifike salama. Mama poa sana yule, ndio maana Mungu anamfungulia. Yule mama nusu ya Chalinze alikua anaisaidia. Yule hata Kikwete anamjua, akipita hapa lazima anywe kahawa kwake. Mtu wake sana yule mama. Sofia maarufu sana, halafu yule mimi nakwambia sio Msomali yule. Yule hata sijui ana roho ya wapi, yeye kila mtu anacheka na kufurahi nae. Akija utafikiri kaja malkia. Watu wanavyojazana.
Dereva; Lakini mshikaji, kisa nilichokisikia juu juu pale kwenye mananasi, hebu nipe mshikaji wangu.
Tukamaliza kula ile tunaondoka tu, nambie ilikuaje mshikaji?
Mimi; Hata sikjui lakini kuna wanawake kumbe walikua mmoja anauza chakula uchi nje hapa, mmoja alikua na kiduka kidogo nae hivyo hivyo. Sasa siku hiyo bahati mbaya wakaumbuka na mimi nilikuwepo na mzee.
Ikawa huyu wa nje kaingia mule ndani dukani, ikawa anashindwa kutoka, sisi tumeondoka, ndio leo nimesikia walikaa mpaka siku ya pili asubuhi akaja mwanamke mwengine kuwatoa.
Drereva: Hilo litakua kubwa lao hilo, lina maujuzi kweli kweli. lakini mshikaji watu wote wanaamini wewe ndio ulifanya mambo, wanasema wale wanga wenyewe walikua wanalia wanaomba urudishwe uje kuwafungua.
Nambie mwanangu manake kwetu huko wanga na wachawi wengi sana. Mimi kinachonisaidia ibada mwanagu.
Mimi: Hakuna zaidi ya ibada.
Dereva; mwanagu mimi siachi kusali na kila siku lazima nisome Qur'an, Nashukuru wazazi wangu walitusisitiza tusome madrasa. Sisi nyumbani bwana amabae hajasoma sana ni mimi, lakini msahafu haunipi shida kabisa kuusoma Kiarabu, sema wenzangu wale wamefika mbali, maana madrasa ipo hapo hapo kwetu. Pale pale ulipopanda, kuna kijiji ka ndani kidogo, sio mbali na barabara, ndio kwetu, ukipita siku yoyote pita uwaone wazee, uone na tunavyoishi, ndio kujuana kwenyewe hivyo.
Mimi; Nakuahidi nitapita hata kama wewe haupo mradi kuna madrasa, nitakwenda nipate dua za watoto, dua za watoto nzuri sana, wanakua wanaomba kwa nia kabisa.
Dereva; Poa mshikaji, Pita tu wakati wowote, halafu si naliona lile afande lanajigonga gonga kwako, Nuksi kweli yule, anajiona sana kwa lile kalio lake. Nasikia mali ya mkubwa wa TRA pale checkpoint ndio piga ua handishwi pale ulipomkya, wenzake wote wanaondoshwa yeye yupo, mpaka katujua sura zetu wote. Usinwache yule, anahela kama nini, yule kila gari ikipita pale lazima imwachie kitu,, na ukijifanya mbishi anakucheki unaelekea wapi, anapiga simu bele huko, utakoma ubishi, hapingwi na mtu yule. Lkini mshikaji leo kakukubali yule mpaka kajifanya mshikaji wangu, si amekupigia unayo namba yake?
Mimi; Ndiyo.
Dereva; Ujiko huo, usimwache kabisa yule.
Mimi; Mimi mshikaji nina mke wangu halafu yule sio sampuli yangu kabisa.
Dereva; Yule kishakudondokea, lina hela lile, wewe lile unalichuna tu. Yule usimuone vile, ana daladala zake zinapiga Mbezi Mlandizi. Mshikaji ana hela yule halafu anaogopewa hata na maaskari wenzake. Mie nakwambia usimwache yule.
Mimi; Sasa mshikaji wewe mtu wa ibada unanifundisha usheatani?
Dereva; Wewe hujui anavyotupa tabu yule.
Mimi; Nitaongea nae usijali, chukulia hasumbui tena.
Dereva; Nakuaminia mwanangu. Halafu yule dada anaonesha mshikaji wake sana, yule tumemshusha mlandizi, Sijui na yule askari mwenzake?
Mimi; Yule kanambia anajuana nae tu, aliniombea lifti tu. Kuna dereva wa lori kaniwacha pale, Isingekua yule dada ningehangaika sana.
Dereva; Wewe ukiona mambo yanakunyookea hivyo inatakiwa usali kwa kumshukuru Mungu, wewe ni mtu mwema mwanangu, si unaona Chalinze mwenyeji kuliko mimi ninaepita siku zote pale. Muombe Mungu sana akuzidishie kua mwema.
Ya yule mwanamke nilikua naongea kwa hasitra tu, usinisikilize mshikaji, usifanye kuzini, wewe una mke bwana.
Mimi; Poa poa, naona hasira zimekwisha.
Dereva; Hivi nikiwafikiria wanavyotuhangaisha, wewe utaona, mpaka tufike tutasimamishwa zaidi ya mara mia, na leo bahati yetu wale wa mdaula naona wametuona tunatoka kula wametuwacha tu.
Mimi: Au yule afande kawapigia simu?
Dereva; Yule ujanja wake unaishia Mlandizi. mungu katusaidia.
Itaendelea.