Faida ipo kwenye pesa, haipo kwenye afya. Hata sumu zinazoweza kumwua mwanadamu zinauzwa. Hivyo ni wewe ndiye unayetakiwa kuamua ununue kitu chenye kukuletea afya njema au cha kukuua taratibu. Baada ya baadhi ya watumiaji kupata madhara makubwa ya kiafya na kugundulika kuwa yalitokana na uvutaji sigara, na kisha kuamua kuyashtaki makampuni yanayotengeneza sigara, na kisha makampuni ya sigara kulipishwa gharama kubwa, ndiyo sababu iliyofanya makampuni yote ya utengenezaji sigara kulazimika kuandika kwenye sigara, "sigara ni hatari kwa afya yako", hivyo ukipata madhara huwezi kuwashtaki watengenezaji kwa sababu uliambiwa wazi kuwa ina madhara mabaya kwa afya yako, nawe kwa uamuzi wako uliamua kuiharibu afya yako.
Lakini pia Serikali karibia zote Duniani, zimepiga marufuku uvutaji wa sigara hadharani, unatakiwa utafute eneo ambalo halina watu ndiyo uende ukavutie huko hiyo sumu yako. Hapa kwetu, japo sheria hiyo ipo lakini usimamiaji wake haupo vizuri. Kuna baadhi ya nchi ukipatikana unavuta sigara hadharani unakamatwa na kushtakiwa.