Mpangilio mzuri wa meno siyo kwaajili ya muonekano au tabasamu zuri pekee yake, mpangilio mzuri wa meno unawezesha kuwa ana afya bora ya kinywa na meno, ikiwa ni pamoja na kuwezesha utafunaji mzuri wa chakula na kuweza kutamka matamshi /kuongea vizuri.
Kwa bahati mbaya watu wengi wana changamoto ya kuwa na mpangilio mbaya wa meno, hali ambayo isipotibiwa inaweza kuleta matatizo mengine ya meno mfano kuoza meno. Nini kinasababisha mpangilio mbaya wa meno?
katika mada hii tutazunguzia vitu vinavyopelekea mtu kuwa na mpangilio mbaya wa meno, ili ikusaidie namna ya kujikinga/ kuwakinga watu wengine wasipate tatizo hili na kama limeshatokea ujue ni nini unaweza fanya kutibu.
1. Kurithi kutoka kwa wazazi
Mtoto anarithi vitu vingi kutoka kwa wazazi, hivyo inawezekana akarithi mpangilio wa meno kutoka kwa wazazi wake. Siyo jambo la kushangaza kwani vinasaba vinarithiwa kizazi mpaka kizazi.
2.Kupoteza/ kung'oa meno ya utotoni kabla ya wakati wake.
Inawezekana umewahi kumpeleka mtoto kwenye kliniki ya meno ili akang'oe jino na kisha daktari akakwambia hawezi kuling'oa kwani muda wake bado. Binadamu ana seti mbili za meno ( ya utotoni na ya ukubwani) kwenye meno ya utotoni, kila jino linamuda wake maalumu wa kuota na kung'oka ili kupisha lile la ukubwani.
Ikitokea jino la utotoni limeng'olewa kabla ya wakati wake ile nafasi yake inaweza kuzibwa na jino lingine ambalo liko mdomoni na kuziba lile jino la ukubwani ambalo linakuwa bado halijaanza kuonekana mdomoni.
3.Tabia ya kunyonya vidole kwa muda mrefu
Watoto huwa na kawaida ya kunyonya vidole, tabia hii ikiendelea kwa muda mrefu mfano ikiwa mtoto ataendelea kunyonya vidole hata anapofikia umri wa zaidi ya miaka minne (4) anakuwa na hatari zaidi ya kupata mpangilio mbaya. Tabia hii hufanya taya la juu kuwa jembamba na hivyo kufanya meno ya juu na chini yasikutane
4.Magonjwa ya fizi
Magonjwa fizi ya muda mrefu yanaweza kupeleka meno kujipanga vibaya ikiwa hayatotibiwa, yamkini umekutana na mtu anakwambia sikuwahi kuwa na mwanya lakini siku zinavozidi kwenda napata mwanya na meno yameanza kuelekea upande lakini pia yanalegea.
5.Tabia ya kutumia mdomo kupumua
Kutumia mdomo badala ya pua kupumua inaweza kusababisha mpangilio mbaya wa meno kwani huathiri upana wa mataya. Kupumua kwa mdomo kunaweza kusababishwa na kuzibwa kwa njia ya pua kwasababu mbali mbali ikiwemo uvimbe kwenye tezi zilizopo kooni N.K , lakini pia inaweza kuwa ni tabia ya mtu tu (habitual mouth breathing)
UFANYE NINI KAMA TAYARI UNA TATIZO HILI?
Unatakiwa kumuona daktari wa kinywa na meno aliyekaribu na wewe, na kama upo Dar es salaam/ Pwani na Maeneo Jirani
unaweza kuwasiliana na daktari kwa namba hizi: 0658 950 085
Kupata suluhisho la tatizo hilo.