STRAIKA wa zamani wa Yanga, Kipanya Malapa amewataka mashabiki kutomchukulia poa, akiwa kwenye harakati zake za kutafuta, badala yake amewataka kujua anaishi maisha yanayompa amani.
Staa huyo ambaye kwa sasa anafanya biashara za kuuza mishikaki ya mia mbili Buguruni, amesema anaipenda biashara hiyo na hafikirii kufulia kiuchumi kwenye maisha yake.
"Naomba wasinichukulie poa, nina mke mzuri ninayempa matunzo yote, nasomesha watoto, natoa michango mbalimbali ya kijamii, nachangia wachezaji wa zamani wanapopata shida mbalimbali, kama haitoshi nina uwezo wa kununua jezi ya Yanga inayouzwa Shilingi 50,000 alisema na kuongeza;
"Nina nyumba za kutosha hapa mjini, sasa wakiniona nauza mishikaki ya Shilingi 200 haimanishi sina maisha ama nimefulia kama wanavyofikiri, naishi maisha yanayonipa raha na siyo wanavyotaka wao."
Amewashauri mastaa wa zamani ambao wanashindwa kufanya mambo yao kwa sababu ya majina makubwa ambayo waliyapata wakati wanacheza Simba na Yanga nyakati hizo, akiwataka watoke mafichoni.
"Shida ya mastaa wengi wanashindwa kuishi maisha yao, wanataka kuwafurahisha watu na kugeuka watumwa, maisha yenyewe mafupi wabadilike waonyeshe uhalisia wao," amesema.
Amesema ili kuonyesha anaipenda kazi hiyo, anaitangaza kwenye mitandao yake ya kijamii ili kila mtu ajue anafanya nini.
"Kwanza sehemu ninayofanyia kazi nimeweka hadi TV watu wanaburudika kuangalia mpira hasa zikichezwa mechi za Simba na Yanga, sijaona tatizo kwenye hilo"
Ikumbukwe 1999/2000 bao lake aliloifunga Yanga akiwa Singida lilifanya Wanajangwani kukosa taji la Ligi Kuu Bara na ubingwa ikachukua Mtibwa Sugar.
S0urce: Mwananchi © 2023