Mwanamuziki maarufu nchini Tanzania, Ommy Dimpoz, amejibu rasmi tuhuma na maneno ya kashfa yaliyotolewa dhidi yake na msanii mwenzake Godfrey Tumaini, maarufu kama Dudu Baya, aliyemwita "chakula" (mshoga).
Ommy Dimpoz ameeleza kuwa hana mpango wa kuchukua hatua yoyote ya kisheria au ya kulipiza kisasi, badala yake amechagua kumwachia Mungu na kumsamehe.
Kauli hiyo imekuja kupitia mahojiano maalum ambapo Ommy Dimpoz alifunguka kuhusu namna anavyokabiliana na kashfa hizo zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Akifafanua mtazamo wake, msanii huyo alieleza kuwa jamii mara nyingi imekuwa ikiwazingizia watu mambo yasiyo ya kweli, kama vile kuwaita wizi au malaya na wahusika kushindwa kujitakasa, hivyo kuamua kuendelea na maisha yao.
Ommy Dimpoz alibainisha kuwa anamchukulia Dudu Baya kama kaka yake mkubwa na mmoja wa wasanii waliomshawishi kuingia kwenye tasnia ya muziki. Hata hivyo, alieleza kuwa Dudu Baya amechagua njia ya kutafuta umaarufu kwa kuwasengenya na kuwazungumzia wengine vibaya mtandaoni.
"Mimi sina cha kumfanya Dudu Baya kwa sababu anayenijua mimi kiundani ni Mungu tu. Yeye amechagua hayo maisha ya kuzungumzia watu kwa ubaya ili aweze kutrend," alisema Ommy Dimpoz, akiongeza kuwa anamwombea Msamaha kwa Mungu na ataendelea kuangazia maisha na kazi zake za muziki bila kuingizwa kwenye migogoro.